Tuesday, 10 September 2019

Waendesha Bodaboda Arusha, kuanza rasmi kupambana na Ukatili dhidi ya Watoto
Viongozi wa umoja wa waendesha bodaboda Arusha (UWABA), wamekubaliana kuanza rasmi, kuwajibika katika kulinda haki na usalama wa watoto, wakiwa katika kazi zao, kufuatia mafunzo waliyoyapata ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto yenye ujumbe usemao, 'Bodaboda Usafiri Salama, Tulinde Haki za Watoto'.
Waendesha Bodaboda hao, wamekubaliana hayo, baada ya kupata mafunzo ya siku moja, yaliyohusu wajibu wao,  katika ulinzi na usalama wa mtoto,  mafunzo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, halmashauri ya Arusha, kwa udhamini wa shirika la CWDC la Jijini Arusha.
Madereva hao wamekiri kuwa awali, hawakufahamu sana, juu ya ulinzi na usalama wa mtoto na kuwa wao wanahusika sana kuwalinda, kutokana na ukweli kuwa, wamekuwa wakiwapakia watoto kwenye kazi zao, bila kuelewa kuwa wanajukumu la kuwalinda na kuwahakikishia usalama wao wakati wote.
Wamesema kuwa, wanaishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wa kundi hilo, na kuanza kulishirikisha kwenye mambo ya kijamii, kwa kuwapa mafunzo mbalimbali yanayowezesha kundi hilo kujitambua, kujithamini na kuanza kuthaminika na jamii kwa sasa.
Mwenyekuti wa UWABA Arusha, Goodluck Ndibalema, amesema kuwa, ameanza kuona mabadiliko makubwa ya kitabia kwa vijana waendesha bodaboda, kutokana na ushirikishwaji unaofanya na Serikali ya awmu ya tano kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali, hali iliyowafanya vijana wa kundi hilo, kujitambua na kujiona kuheshimika na kuthaminika na jamii inayowazunguka licha ya changamto mbalimbali zinazowakabili.
"Kundi la waendesha Bodaboda, limekuwa likidharaulika kutokana na kundi hilo kutengwa na kutokushirikishwa kwenye mambo ya kijamii, na kuonekana kama ni kundi la wahalifu, ninakiri kwa sasa kutokana na ushirikishwaji unaofanywa Serikali ya awamu ya tano, waendesha Bodaboda wamebadilika na kujitambua kuwa, wanajukumu kubwa kwa jamii" amesema Rugemalila
Naye mkurugenzi mtendaji, halmashauri ya Arusha,Dkt. Wilson Mahera, amewahakikishia madereva Bodaboda hao kuwa, Serikali ya awamu ya tano, inatambua huduma wanayoitoa kwa jamii, na kuwataka kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kwa kuwalinda na  kutoa taarifa pindi wanaposikia au kuona watoto wakifanyiwa ukatili.
Amesema kuwa, kuanzia sasa Bodaboda uwe usafiri salama na kuzuia ulatili kwa watoto, kwa kuwa, baadhi yao wamekuwa wakishutumiwa kutumia usafiri wao kuwashawishi watoto wa shule na kuwasababishia mimba na ndoa za utotoni.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha, mhe. Noah Lembris, amewasisitiza madereva hao, kufuata sheria za usalama barabarani, wanapoendesha pikipiki zao, ili kuzuia ajali, zinazosababisha vifo na pengine ulemavu, kwa kufanya hivyo ni kuzuia ukatili kwa watoto kwa kuwa vifo hivyo husababisha watoto wengi kubaki yatima.

Akieleza lengo la kukutana na waendesha Bodaboda hao, mkurugenzi wa Shirika la CWCD, Hindu Mbwego, amesema kuwa, lengo kuu ni ushirikishwaji na kuwapa mafunzo ya Ulinzi na usalama wa mtoto, yatakayowawezesha kushiriki katika kuzuia ukatili kwa watoto, kwa kuwa, baadhi ya waendesha Bodaboda wamekuwa, wakilaumiwa kwa kutumia vyombo hivyo kuwarubuni wanafunzi na kutumia usafiri huo kuwapeleka kwenye matukio ya ngono.
Amewataka madereva hao, kuona thamani ya watoto hao, na kuacha tabia ya kutumika kuwapeleka watoto kwenye nyumba za wagenj, na badala yake kushiriki kuwalinda watoto, pamoja na kutoa taarifa za matukio hayo, ili kuifanya jamii kuona Bodaboda ni Usafiri salama unaozuia ukatili dhidi ya watoto.
Awali, Mafunzo hayo, yamekuwakutanisha Viongozi wa Vituo vya Bodaboda, kutoka halmashuri mbili za Jiji la Arusha na Halmashauri ya Arusha na yaliambatana na maandamano ya kuzunguka jiji la Arusha, yakiwa na Kauli mbiu ya BODABODA USAFIRI SALAMA, ZUIA UKATILI DHIDI YA WATOTO.

No comments:

Post a comment