Monday, 9 September 2019

VUDEI YAJENGA MADARASA KOROGWE TANGA.

 Mkuu wa wilaya ya Korogwe akitembea na viongozi wengine kwenda kupokea majengo ya shule.MKUU wa wilaya ya Korogwe Kisa Kasongwa, amempongeza Mkurugenzi wa taasisi ya Vuga Development Initiative (VUDEI) Azid Rama Kaoneka kwa msaada wa kujenga madarasa matatu, ofisi na vyoo katika shule ya sekondari Lutindi wilayani Korogwe.

Akitoa pongezi hizo katika makabidhiano ya awali baada ya kukamilika madarasa hayo, Mkuu wa wilaya hiyo alisema taasisi hiyo imeunga mkono jitihada zake katika elimu za 'Nivushe Nitimize Ndoto Zangu'.

Amesema kujengwa kwa madarasa hayo, kutasaidia kuinua elimu kwa wakazi wa kata Lutindi ambapo awali watoto walikuwa wakitembea umbali mrefu kwenda kusoma sekondari katika kata jirani ya Lewa.

"Shule hii ni ukombozi mkubwa kwa watoto wetu, walikuwa wakitembea umbali mrefu kwenda Mashindei Sekondari iliyokuwa kata ya Lewa iliyokuwa jirani ya Lewa," alisema Kasongwa.

Alisema hata ufaulu katika shule ya sekondari Mashindei umekuwa mdogo na kusababisha ishike nafasi ya mwisho katika matokeo ya Kitaifa, lakini sasa sekondari hiyo mpya itaondoa sifuri waliyokuwa wakipata kila mwaka.

Kwa upande wake Kaoneka ambaye shule hiyo wameijenga kwa ushirikiano na taasisi ya Canada ya A Better Would (ABW), aliitaka jamii kujitolea kwa hali na mali kufanya shughuli za msaragambo kusaidia kazi zinazohusu jamii.

"Tupo nyuma sana, tunahitajika tujitoe katika kazi zinazotuhusu, ujenzi huu umechukua muda mrefu sana kwasababu hamkuwa mkifanya kazi za msaragambo," alisema Kaoneka na kuongeza;

"Kila muomba mboga lazima awe na iliyochacha,".

Taasisi hiyo imejenga vyumba vitatu vya madarasa, ofisi ya walimu na vyoo matundu 12 chini ya usimamizi wa fundi Athumani Kaoneka.

 
Majengo yaliyojengwa na Kaoneka.

Kaoneka ambaye amekuwa akishiriki shughuli mbalimbali za maendeleo wilayani Korogwe, alisema shule hiyo wameijenga kwa gharama ya sh. 75,486,000 ukiondoa gharama za madirisha ya vioo ambayo haikuwepo awali.

" Tunapenda kuwasisitiza wananchi wafadhili wetu wanapenda kuona mmekusanya mawe, kokoto, mchanga, mbao na vitu vingine watawasaidie hata maabara mnayotaka kujenga," alisema.

Diwani wa kata ya Lutindi Nicolaus Shemsanga, alimshukuru Kaoneka kwa msaada wa kujenga sekondari hiyo ambayo aliielezea kwamba italeta ukombozi mkubwa wa elimu katika kata hiyo.

Kwa upande wake diwani wa viti maalumu wa tarafa ya Bungu Elizabeth Singano alisema jukumu kubwa walilokuwa nalo kwa sasa ni kujenga chumba cha maabara ili watoto watakaosoma waweze kujifunza vizuri masomo ya sayansi.

Ofisa Mtendaji wa kata ya Lutindi Meshack Luka Logani, alisema ujenzi huo ulikumbwa na changamoto ya wananchi kushindwa kushiriki kazi za msaragambo.

" Kiukweli licha ya mfadhili kujitolea kujenga sekondari lakini changamoto ilikuwa wananchi wanashindwa kuleta mawe, mchanga, kokoto na maji," alisema.

No comments:

Post a comment