Thursday, 26 September 2019

Serikali yakemea wazazi wanaowafanya watoto wa kike kuwa mitaji


Serikali imewataka wazazi kuacha tabia ya kuwageuza watoto wao hasa wanafunzi wa kike kuwa mitaji ya kipato chao ikiwemo kuwaozesha, na badala yake wawasaidie katika kupata elimu.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha alipokuwa katika ziara ya kikazi wilayani Itilima mkoani Simiyu baada ya kukagua ujenzi wa mabweni ya wasichana shule ya sekondari Nkoma, ofisi ya wathibiti ubora na jengo la veta linaloendelea kujengwa katika kijiji cha Kanadi wilayani humo.

Amewataka wazazi kuwasomesha watoto hao ame ili wawe msaada mkubwa wa baadaye.

Amewataka wazazi kuwekeza zaidi kwenye elimu ili kuwa na mtaji mzuri baadae huku akisisitiza kuwa mtoto wa kike ana haki sawa ya kupata elimu sawa na mtoto wa kiume ambapo katika jamii nyingi bado hazijawapa kipaumbele cha kupata elimu.

"Kuna baadhi ya wazazi bado wanashawishi watoto wao kufanya vibaya katika mitihani yao ya mwisho ili wasiendelee na masomo, niwaombe msishawishi watoto wa kike na kuwatilia vikwazo vya kukatisha masomo mtoto wa kike ana nafasi ya kupata elimu sawa na mtoto wa kiume na pia mtoto wa kike ni wa serikali, hivyo mnaowakatisha masomo  mtakiona cha moto,’’ amesema Naibu Waziri Ole Nasha.

No comments:

Post a Comment