KAMISHNA Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini (CPG) Phaustine Kasike wa kwanza kushoto akiwa ameshika matofali wakati wa ziara ya kukagua mradi wa Ujenzi huo katika Magereza ya Isanga na Msalato yaliyopo jijini hapa (katikati) ni Mkuu wa Magereza mkoani Dodoma Kenneth Mwambije,

Na.Alex Sonna, Dodoma.

KAMISHNA Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini (CPG) Phaustine Kasike amewaagiza maofisa wa jeshi hilo nchini kote kuhakikisha wanatekeleza agizo la Rais Dk John Magufuli la kujenga nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya stafu wa jeshi hilo kupitia nguvu Kazi walionayo ili kuipunguzia mzigo Serikali.

Jeshi hilo linakabiliwa na tatizo la uhaba wa nyumba za maofisa hao katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Hayo aliyasema  wakati wa ziara ya kukagua mradi wa Ujenzi huo katika Magereza ya Isanga na Msalato yaliyopo jijini hapa Kamishna Jenerali Kasike amesema kuwa jumla ya nyumba 9000 zinatakiwa kwa ajili ya kumaliza changamoto hiyo ambapo kila mkoa kupitia nguvu Kazi walionayo katika Magereza wanatekeleza mradi huo.

Amesema kuwa upande wa mkoa wa Dodoma zinatakiwa nyumba 340 katika gereza la Isanga lakini hadi sasa tayari nyumba 137 zipo katika hatua ya mwisho ya Ujenzi huku zikisalia 203 ambazo nazo zinatakiwa kukamilika ndani ya muda ili ziweze kuanza kutumika kwa maofisa hao.

“Nawapongeza sana maofisa wa Magereza kwa jitihada wanazofanya katika kusimamia Ujenzi huo nimeona Dodoma wako vizuri na mikoa mingine fanyeni hivyo ili tufikie lengo ikiwemo kutekeleza agizo la Rais,” amesema Kamishna Jenerali Kasike.

Hata hivyo amesema kuwa  jitihada wanazofanya kupitia nguvu Kazi,wanaimani Serikali itaweka nguvu ya ziada jambo ambalo watafanikiwa kumaliza tatizo hilo kabisa.

“Nahakika hadi sasa tumepunguza gharama za Ujenzi ambazo Serikali ingetoa bila Jeshi hilo kubuni mradi huo,zikikamilika gharama halisi ya ujenzi itajulikana kiasi gani kimetumika na kipi kimeokolewa kama wangetumia wakandarasi “, amesisitiza Kamishna Jenerali Kasike.

Akitolea mfano Gereza la Isanga lililopo jijini hapa amesema nyumba 20 tayari msingi imeshawekwa huku nyumba 14 zimefikia katika hatua ya lenta na sita zilizosalia katika gereza hilo zinaendelea kujengwa.

Alisema Magereza hayo wamefanya vizuri kwa sababu wametumia muda na nguvu Kazi iliopo kuhakikisha wanafanikiwa kumaliza tatizo la uhaba wa nyumba za maofisa wa jeshi hilo.

Alisema kutokana na kutumia vyanzo vyao bado wanaimani watakamilisha ndani ya muda waliojiwekea.
Naye Mkuu wa Magereza mkoani Dodoma Kenneth Mwambije alisema Jeshi hilo mkoani Dodoma wako mstari wa mbele katika usimamizi wa mradi huo ili kutimiza lengo la kukamilisha Ujenzi huo pamoja na kutatua changamoto ya tatizo hilo.

Mwambije alisema lengo ni kuona idadi ya nyumba zinazotakiwa katika mkoa wa Dodoma kwenye Magereza husika zinakamilika kwa wakati ili kurahisha ufanyaji Kazi wa askari wa jeshi hilo.

“Tunashkuru Kamishna Jenerali kutembelea mradi huu wa Ujenzi tutahakikisha usimamizi unafanyika kifasaha na nyumba zitaendelea kukamilika,” alisema Mwambije.

Kwa upande wa wakuu wa Gereza la Isanga na Msalato jijini Dodoma kwa nyakati tofauti walimshkuru Kamishna Jenerali kwa kutembelea mradi wa Ujenzi na  kumuhakikishia wataendelea kusimamia ili kuhakikisha nyumba hizo zinakamilika kwa wakati.

Huruma Mwalije ambaye ni Mkuu wa gereza la Msalato alisema lengo lao ni kuona idadi ya nyumba walizopangiwa zinakamilika.

Kwa upande wa Mkuu wa gereza la Isanga John Daud alisema Kamishna asiwe na wasiwasi Kazi aliyowakabidhi itafanyika kwa mujibu wa sheria Na maelekezo waliopewa.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: