Sunday, 14 July 2019

MSAKO WA MIFUKO YA PLASTIKI WAENDELEA WILAYANI KOROGWE

 Mkaguzi wa Mazingira na Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga Abdallah Lungo (kulia) akiwa ameshikilia mfuko wa plastiki ambapo Adinan Omar (kushoto) alikuwa anautumia kuhifadhi nguo zake akiingia kazini kubeba mizigo. Omar ni kuli kwenye maghala ya kubeba mizigo ya mfanyabiashara Ally Mcharo. (Picha na Yusuph Mussa).
Mkaguzi wa Mazingira na Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga Abdallah Lungo (kushoto) akionesha stoo inayohifadhi mifuko inayokusanywa kutoka wilaya za Korogwe, Lushoto, Handeni na Kilindi. Stoo hiyo ipo Soko la kisasa la Kilole katika Halmashauri ya Mji Korogwe. Kulia ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Usafishaji na Mazingira, Ruvu Bi. Balbina Semgomba. (Picha na Yusuph Mussa)
NA YUSUPH MUSSA,KOROGWE.

BAADHI ya wananchi bado wanatumia mifuko ya plastiki kwenye Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga, ni baada ya timu ya uhamasishaji usafi wa mazingira kufanya zoezi la kutembelea maeneo ya biashara ikiwemo maduka, stendi na shughuli za kijamii.

 Mkaguzi wa Mazingira na Afisa Mazingira katika Halmashauri ya Mji Korogwe Abdallah Lungo aliongoza zoezi hilo lililofanyika jana Julai 13, 2019 kwenye kata za Majengo, Old Korogwe na Kilole, ambapo baadhi ya watu  waliokutwa na mifuko hiyo walipigwa faini, huku wengine wakipewa onyo, na elimu ya mazingira.

 Kuli wa kubeba mizigo kwenye maghala ya mfanyabiashara Ally Mcharo, Adinan Omar alikutwa amehidhi nguo zake kwenye mifuko ya plastiki minne, hivyo alipigwa faini ya sh. 30,000 na mifuko hiyo kuchukuliwa na kwenda
 kuhifadhiwa kwenye stoo ya kukusanya mifuko hiyo kwa Ukanda wa Usambara wenye wilaya za Lushoto, Korogwe, Handeni na Kilindi.

 Stoo hiyo ipo kwenye Soko la kisasa la Kilole, ambapo baada ya kukusanywa, na kutokana na maagizo ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), mifuko hiyo itapelekwa kunakohusika ili kutengenezewa bidhaa nyingine.

 "Zoezi letu limekwenda vizuri, na kama ulivyoona mwandishi tumekushirikisha mwanzo hadi mwisho. Nia ni kuwapa wananchi elimu bila kuwabughudhi wala kuwanyanyasa, na hayo ni maagizo tuliyopewa. Lakini nataka kusema, bado hatutakiwi kulala kwa kuamini kazi imekwisha, kwani baadhi ya wananchi, aidha hawajaelewa somo ama wanafanya makusudi.

 "Umeshuhudia baadhi ya wananchi bado wamewekea bidhaa baadhi ya mifuko ya  plastiki, na wengine wamebadilisha vifungashio vya mikate kuwa vibebeo vya bidhaa nyingine. Tumejaribu kuwaelimisha, huku tukiwataka wasirudie, na mmoja wapo Adinan Omar ambaye ni mmbeba mizigo, yeye tumempiga faini ya
 chini kabisa ya sh. 30,000, ambayo anatakiwa kuilipa ndani ya siku 14 tangu kuandikiwa adhabu hiyo" alisema Lungu.

Kwenye ziara ya Naibu Waziri wa TAMISEMI wilayani Korogwe, Mwita Waitara, na hasa alipokuwa anazungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji Korogwe  hivi karibuni, alisema kuna mabadiliko makubwa sana kwenye masuala ya usafi  katika Mji wa Korogwe, kwani wakati yeye ni Katibu wa UVCCM Mkoa wa Tanga  katikati ya miaka ya 2000, mji huo ulikuwa unakabiliwa na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.

 Lakini kwa sasa jitihada kubwa zimefanyika, na kwa sasa mji wa Korogwe upo safi, huku kukiwa na uhakika wa magari ya kuzoa taka ngumu na maji taka.

 "Tutaendelea na zoezi letu la kuwatembelea wananchi wetu mara kwa mara na kutoa elimu hadi hapo watakapoelewa mifuko ya plastiki ina madhara, na ni tishio kwa mustakabali wa nchi yetu, hivyo wawe tayari kubadilika bila shuruti, na kuweza kusaidia maendeleo ya nchi yetu" alisema Lungo.

 Naye Mwenyekiti wa Kikundi cha Usafishaji na Mazingira Ruvu, Balbina Semgomba, ambaye alishiriki zoezi hilo, alisema wataendelea kutoa elimu kwa wananchi hadi watakapoona kuwa mifuko ya plastiki sio salama kwa mazingira kwani tayari walishaona mifuko hiyo ndiyo utamaduni kwa matumizi ya kila siku, na hiyo ni kutokana na kuitumia kwa muda mrefu.

 MWISHO.

No comments:

Post a Comment