Wednesday, 19 June 2019

Waziri Jafo amtaka Mkuu wa Idara ya Elimu kuandika barua ya kujielezaWaziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo ameagiza Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kuandika barua ya kujieleza kwanini amekaidi kutekeleza miradi ya Elimu kwa kutumia Force Account.

Akizungumza katika ziara yake Wilayani humo Mhe. Jafo amemtaka Afisa Elimu Nelson Milanzi ambaye yuko Mtwara kwenye UMISETA kurejea kwenye kituo chake cha kazi, kurejesha fedha za safari alizopewa kwa siku ambazo alitakiwa kuwepo kwenye mashindano hayo ya michezo ya shule za sekondari ambayo yatamalizika mwishoni mwa wiki hii na kuandika barua ya kujieleza kwanini asichukuliwe hatua.

Jafo amesema haiwezekani Miradi ya Elimu kukwama kwa sababu ya Afisa Elimu kutofautiana na uongozi kwa maslahi  binafsi kwa kutaka kujenga miundombinu ya shule kwa kutumia mkandarasi na sio mafundi wa jamii (Force Account) kama ilivyoada ya miradi ya Halmashauri.

“Fedha zimeletwa tangu January 2019 kwa ajili ya shule ya Sekondari Sejeli na Kongwa kujenga Mabweni, bwalo la chakula, maabara, madarasa pamoja na nyumba za mwalimu lakini mpaka leo hii ujenzi wa majengo hayo ndio kwanza uko katika hatua za msingi huu ni uzembe wa hali ya juu;

"Kazi hii imeanza asubuhi ya leo baada ya kusikia nakuja ziara, hata haya matofali hayajauka, mchanga ndio unashushwa na inaonekana mafundi mmewakusanya huko kijijini ili ujenzi uonekane unaendelea vizuri ila kiuhalisia kazi hii ilikua imesimama kabisa hili ni tatizo kubwa na mnamuangusha Spika kwa Bunge la Tanzania Mhe. Job Ndugai ambaye anawapigania wananchi wake ili wapate miradi lakini watendaji mnakwamisha," alisema Jafo.


Akizungumzia ucheleweshaji wa miradi hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dr. Omary Nkulo amesema pamekuwa na mvutano wa namna ya kutekeleza miradi hiyo wakati Afisa Elimu akitaka kazi hizo apewe mkandarasi baraza la madiwani waliamua itumike force account hapo ndipo pakawa na ucheleweshaji sababu Afisa Elimu alikua anachelewesha kupitisha baadhi ya vitu  kwa sababu mapendekezo yake hayakukubalika.

Dr. Nkulo aliongeza kuwa halmshauri  inachangamoto ya wahandisi wa ujenzi kwa namna kubwa wanatakiwa kusimamia miradi hiyo na aliyepo ni fundi mchundo(Technician)  ambaye ndiye anayesimamia miradi yote inayotekelezwa hapa Kongwa hiyo pia imekuwa ni miongoni mwa sababu ya kuchelewa kwa baadhi ya miradi.

Miradi hiyo ya Elimu imetakiwa kukamilika mapema Mwezi August,2019 ili iweze kuchukua wanafunzi wa bweni na miundombinu mingine itumike kama ilivyokusudiwa.

No comments:

Post a Comment