SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana Ubalozi wa India chini ya Taasisi ya utengenezaji viungo bandia BMVSS imewafuta machozi watu wenye ulemavu wa miguu nchini kwa kugawa  miguu ya bandia kwa zaidi ya Watu 600.

Hayo yamejiri mapema leo katika hafla ya utoaji vifaa tiba saidizi kwa watu wenye ulemavu katika taasisi ya mifupa (MOI) iliyoongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu.

Waziri Ummy amesema kuwa licha ya kuwepo changamoto ya upungufu wa miguu bandia kwa ajili ya wenye ulemavu, Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea na juhudi za kuhakikisha wenye uhitaji wa miguu hiyo wanapatiwa msaada.

“Tulitangaza watu 500 waombe, lakini watu walioomba wamezidi 900 ambao wamejisajili, huku miguu ambayo imepatikana ikiwa ni 600, inamaana watu 300 hatutaweza kuwafikia, Serikali kupitia Wizara ya Afya itaangalia nanmna gani itawafikia hao 300” alisema Waziri Ummy.

Aidha, waziri Ummy amesema kuwa ajali za barabarani zimekuwa chanzo kikubwa kwa Wananchi wengi  kupoteza viungo, hivyo kuleta janga la ulemavu hali inayorudisha nyuma jitihada za kuleta maendeleo  nchini.

“Ukizunguka katika hospitali za Wilaya na Hospitali za Rufaa za Mikoa unaona idadi kubwa ya watu waliopata ajali za barabarani. Mwaka 2014 Hospitali ya Moi ilipokea wagonjwa wa ajali kati ya 200 mpaka 300, sasa hivi wanapokea wagonjwa wa ajali za Barabarani takribani 500 mpaka 600” alisema Waziri Ummy.

Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa Serikali iko kwenye mpango wa kupeleka muswada Bungeni kuhakikisha moja ya masharti ya kuwa dereva wa pikipiki ni lazima uwe na umiliki wa Bima ya Afya ili kujihakikishia uhakika wa matibabu pindi ajali inapotokea.

Mbali na hayo Waziri Ummy ametoa maelekezo kwa wadau na viongozi mbali mbali kufuata taratibu za kiafya ikiwemo kupata vipimo kabla ya kugawa viungo hivyo kwa jamii jambo litalosaidia kulinda afya zao.

Nae, Mkurugenzi Mtendaji  wa Taasisi ya MOI, Dkt. Respicious Boniface ameishukuru Serikali za kuiwezesha Taasisi ya Moi kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi, ikiwemo upatikanaji wa fedha za kununua vifaa vya kisasa jambo lililosaidia kupunguza idadi ya wagonjwa waliotakiwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

MWISHO.


Share To:

msumbanews

Post A Comment: