Na Ferdinand Shayo,Arusha.
Viongozi wa dini kutoka makanisa mbalimbali mkoa wa Arusha wamehitimu mafunzo ya udereva na  usalama barabarani yaliyotolewa na  Chuo cha Wide Institute of Driving lengo ikiwa ni kudhibiti ajali zinazosababisha vifo na majeruhi.
Mkufunzi wa Chuo hicho Faustine  Matina amesema kuwa mafunzo hayo yalifanyika kwa umakini mkumbwa kwa viongozi hao wa dini ili waweze kuwa mabalozi wa masuala ya usalama barabarani na kuokoa maisha ya watu.
Matina amesema kuwa viongozi hao wa dini wamehitimu mafunzoyao na kupatiwa vyeti hivyo kukidhi matakwa ya serikali ya kuwataka madereva kuwa na vyeti vya shule ya udereva pamoja na leseni kama vigezo muhimu kwa madereva.
Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani mkoani Arusha Joseph  Bukombe amewataka viongozi hao wa dini kuhubiri masuala ya usalama barabarani katika makanisa yao ili kuokoa maisha ya waumini wao ambao wengi ni madereva.
“Nawaomba msikae kimya mkazungumze huko makanisani badala ya kusema nendeni kwa amani muwaambie kuwa wasisahau kufunga mkanda wanapokua kwenye magari yao kwa kufanya hivyo tutaokoa maisha yao” Alisema Bukombe
Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha  ambaye ni Mrakibu wa polisi Makao Makuu ya polisi Arusha Namsemba Mwakatobe amesema kuwa jeshi hilo litashirikiana na viongozi wa dini katika kutatua changamoto za usalama barabarani pamoja na kutoa elimu kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa Mkoani Arusha ,Askofu Stanley Hotay amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia Viongozi wa dini kuwa na uelewa mkubwa na kujifunza vitu vingi ambavyo walikua hawavijui kuhusu usalama barabarani.

Share To:

Post A Comment: