Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amewaongoza mamia ya waombolezaji kutoka Mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mwanza , Dar es Salaam na maeneo mengine nchini, katika mazishi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Marehemu Brigedia Jenerali Mstaafu, Dkt. Yohana Daudi Balele, ambayo yamefanyika Mei 09, 2019  katika eneo la Malinoni Mtaa wa Kidinda Mjini Bariadi.


Akizungumza na waombolezaji hao kabla ya kuaga mwili wa Marehemu Dkt.Balele, Mtaka amesema mkoa wa Simiyu unatambua mchango wa Marehemu katika jitihada za kuanzisha mkoa wa Simiyu na mapinduzi makubwa aliyoyafanya katika Elimu na kuahidi kuweka alama yake katika mkoa kumuenzi.

“Uongozi wa Mkoa kwa kutambua mchango wa Marehemu Dkt.Balele katika kuanzisha mkoa huu na katika mapinduzi ya Elimu aliyoyafanya wilayani Bariadi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, tunaweka alama ya maisha yake kama kumbukumbu katika Shule ya Sekondari Majahida ambayo itabadilishwa Jina kuwa Dkt.Balele Sekondari na Barabara moja katikati ya Mji wa Bariadi itaitwa Barabara ya Dkt.Balele”  alisema Mtaka.

Akisoma Wasifu wa Marehemu,  Kapteni Zaharani Masimba wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) amesema marehemu amelitumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa zaidi ya miaka 32 na kutunikiwa medali mbalimbali, ikiwemo ya Vita, Kagera, miaka 20 ya JWTZ, Miaka 40 ya JWTZ, Utumishi wa muda mrefu na Utumishi uliotukuka.

Naye mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo, Brigedia Jenerali, Robson Mboli Mwanjela amesema, licha ya Marehemu kustaafu Jeshi, alitumia vizuri taaluma yake ya Udaktari kuwasaidia watu mbalimbali na kuwataka wananchi wa Simiyu kuiga mema mengi aliyoyafanya.

“Marehemu atakumbukwa daima kwa mchango wake mkubwa alioutoa wakati wa utumishi wake  jeshini na kwa Taifa kwa ujumla, katika vyeo na madaraka mbalimbali aliyopewa wakati wa utumishi wake na hata baada ya kustaafu; aidha atakumbukwa kwa umakini wake wa kutibu binadamu na ufundishaji wanafunzi katika kada ya afya ” alisema Brig. Jen. Mwanjela.

Nao baadhi ya viongozi waliofanya kazi na Marehemu Dkt. Balele wamemuelezea kuwa alikuwa mwaminifu, mchapakazi, hodari na mwenye Upendo huku wakitoa wito kwa wananchi Mkoani Simiyu na hapa nchini kwa ujumla kuyaenzi mema yake.

“Dkt.Balele alikuwa kiongozi halisi alitumia uwezo na ushawishi wake kuwafanya watu wake wawe kama anavyotamani wawe, alipenda sana Elimu alitaka watu wasome na pengine hata zaidi yake, ndiye aliyehamasisha Wafanyabiashara kujenga Biashara Sekondari hapa BARIADI, naomba wana Simiyu tumuenzi kwa kuwekeza katika elimu” alisema Mbunge wa Bariadi, Mhe. Andrew Change

“Marehemu Dkt.Balele alikuwa mdau mkubwa wa Elimu, katika kipindi chake alifanikiwa kuanzisha shule za Sekondari 44 Wilaya ya Bariadi na Itilima ambayo pia kipindi hicho ilikuwa sehemu ya Bariadi, lakini pia wakati wa mpango wa kuugawa mkoa wa Shinyanga alikuwa na mchango mkubwa wa kuanzisha mkoa wa Simiyu na makao makuu kuwa Bariadi, naomba tuendelee kuenzi mema yake” Baraka Konisaga, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mstaafu.

Marehemu Dkt.Balele ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga mwaka 2006 hadi  mwaka 2011 alizaliwa Desemba 28, 1948 katika Kijiji Cha Kasoli wilayani Bariadi na alipatwa na mauti Mei 02, 2019 katika Hospitali ya Lugalo jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: