Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, amewataka wakazi wa mkoa huo,  kuotesha miti kwa wingi, ili kutunza mazingira yanayowazunguka na yale ya vyanzo vya maji, kwa lengo la kurejesha uoto wa asili ambao tayari umeharibiwa kwa kiasi kikubwa katika maeneo mengi.
Akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa juma la kupanda miti kitaifa, mkoa wa Arusha, uliofanyika katika shule ya sekondari Ekenywa, kijiji cha Osunyai kata ya Olturoto mapema jana, Gambo amewataka wakazi wa mkoa huo, kuchukua tahadhari na kuanza juhudi za kurejesha uoto wa asili wa mkoa huo kwa kuotesha miti kwa kasi kubwa.
Amewasisitiza wakazi hao, kuifanya Arusha kuwa ya kijani, kama kauli mbiu inavyosema, 'Arusha ya Kijani inawezekana'  kwa kila mmoja katika eneo lake kuhakikisha anapanda miti, na kuirejesha Arusha kwenye asili yake ya kijani kwa vitendo.
"Endapo kila mkazi wa mkoa wa Arusha atapanda miti na kuitunza Arusha itakua ya kijani na uoto wa asili ulioharibika utarejea kama ilivyokua hapo awali" amesema Gambo
Aidha amewakumbusha wananchi kutambua kuwa, ukataji wa miti ovyo unasababisha ukame na vyanzo vya maji kupungua na hatimaye kukauka, madhara ambayo tayari yameanza kuoneka na kuwataka wananchi wote kuchukua tahadhari kwa kuotesha miti kwa kasi kubwa na kwa wingi zaidi.
Wilium Kivuyo mkazi wa kijiji cha Osunyai kata ya Olturoto, ameiomba serikali kupitia halmashauri ya Arusha, kuzuia uvunaji miti holela kwa kuwa ndio chanzo cha kuruzorotesha  juhudi za upandaji miti zinazofanywa kila mwaka.
"Wako watu ambao hukata miti kwa kutumia mashine (Cheinsaw) ambayo hukata miti mingi kwa muda mfupi, hii ndio inarudisha nyuma zoezi hili linalofanyika kila mwaka na kuhatarisha mazingira yetu" amesema Kivuyo.
Naye mkurugenzi mtendaji, halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson Mahera, ameahidi kusimamia utunzaji wa miti hiyo iliyooteshwa na kuwataka wananchi kuendelea kuitunza miti waliyopanda kwa mikono yao, ili hapi badaye iweze kuwa kumbukumbu ya kihistoria ya kujivunia katika maisha yao.
Uzinduzi wa juma la  kupanda miti kitaifa mkoa wa Arusha, ulinakshiwa na kauli mbiu ya 'Arusha ya kijani inawezekana tupande miti kwa maendeleo ya viwanda', halmashauri ya Arusha inategemea kupanda jumla ya miti 6,000 kupitia wananchi, mashirika na taasisisi za binafsi na zile za serikali.

PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA UZINDUZI WA JUMA LA KUOTESHA MITI MKOA WA ARUSHA.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: