Wednesday, 24 April 2019

RC akagua maendeleo ya Vitambulisho vya wajasiliamali


Na. Enock Magali Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge amefanya ziara katika Wilaya ya Kongwa,yenye lengo la kukagua maendeleo ya utoaji wa vitambulisho vya wajasiliamali ambapo amekutana na changamoto ya baadhi ya wajasiliamali kugoma kufanya usafi kutokana na wao kuwa wamelipia kitambulisho.

Akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya hiyo Deo Ndejembi, Dkt Mahenge amefika na kuzungumza na baadhi ya wajasiliamali wanaofanya biashara zao katika eneo la mji mdogo wa Kibaigwa,ambapo Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa minadani na magulioni wilaya ya Kongwa Charles

Magimba,amesema baadhi ya wafanyabiashara waliopo minadani suala la usafi kwao limekuwa ni shida kufanyika kutokana na madai kuwa wamekwisha lipia vitambulisho.

"Tulichukua jukumu la kusema kwamba usafi tutajishughulisha wenyewe na tukaamua kuwa kila mtu atachangia shilingi mia mbili,lakini kumekuwa na changamoto kwa viongozi wetu kusema kuwa watu wasichangishwe gharama yoyote kwa sabau Rais kasema kila kitu bure,sasa hata usafi tusijihudumie?, Alihoji

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Deo Ndejembi ,amesema kuwa ni kweli walitoa maelekezo kuwa watu wasichangishwe gharama yoyote lakini kama wamejipangia uataratibu wao ni sawa.

"Tulitoa maelekezo kwa mji mdogo ya kuwa mjasiliamali yoyote asibugudhiwe,lakini walikubaliana wenyewe nje ya mfumo wetu wa serikali na kutuletea,suala la usafi ni sawa ili mradi wamekubaliana wao wenyewe"Alisema

Akitolea ufafanuzi suala hilo Mkuuwa Mkoa wa Dodoma Dkt.Mahenge yeye amesema kuwa usafi ni wajibu wa kila mtu na kama wao wamekubaliana wenyewe kuchangishana suala hilo halina tatizo.

"Ningeomba Mkurugenzi utusaidie kwa sababu hapa ni mji mkubwa lazima kuwe na utaratibu unaojulikana wa usafi,kwaiyo lazima uje ukae hapa na watalamu wako muangalie utaratibu mzima wa usafi ukoje ,mpitie,mkubaliane na muone kinachofanyika"Alisisitiza

Katika zoezi hilo wajasiliamali hao wamekiri kuwa vitambulisho hivyo vimekuwa na msaada mkubwa katika uendeshaji wa biashara zao kwani kwa sasa hawabugudhiwi kama hapo awali.

No comments:

Post a Comment