Serikali imetoa fursa kwa wanafunzi waliofaulu kidato cha nne mwaka 2018 na wanaotegemea kujiunga na kidato cha tano pamoja na vyuo kwa mwaka 2019 kubadilisha Tahsusi(Combination).

Akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo Serikali ya Awamu ya Tano inawapa wahitimu hao fursa ya kufanya mabadiliko ya machaguo ya Tahasusi (Combination) na kozi mbalimbali walizozichagua kwenye fomu ya “F4-Selform.

Amesema Fursa hii itawawezesha wanafunzi kurekebisha machaguo yao kulingana na ufaulu waliopata kwenye matokeo ya Kidato cha Nne 2018 yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania, NECTA.

“Kwa mara ya kwanza Wanafunzi watakuwa na uwezo wa kubadili machaguo au kuchagua kutoka Kidato cha Tano kwenda Chuo au Chuo kwenda Kidato cha Tano kwa kadiri ya mahitaji yake na jinsi alivyofaulu mitihani yake” alisema Jafo na kuongeza;

"Unajua wanafunzi hujaza Fomu za F4-Selform kabla ya kufanya mitihani sasa matokeo huweza kuja tofauti na vile alivyojaza lakini mwanafunzi huyo amefaulu hivyo ni wakati sasa kwa kubadilisha machaguo kwa kadiri ya ufaulu wake na anavyopendelea mwenyewe "

Aidha Waziri aliongeza kuwa : "Ofisi yangu imetoa fursa hii kwa wahitimu kubadili machaguo yao ili kutoa mwanya zaidi kwa mwanafunzi kusoma fani au Tahasusi itakayomwandaa kuwa na mtaalam fulani katika maisha yake ya baadaye kwa namna ambayo anatamani yeye mwenyewe au kwa kushauriwa na wazazi au walezi wake; Hii ni kutokana na ukweli kwamba baadhi ya wanafunzi hawakujaza kwa uhakika Tahasusi au Kozi zao kutokana na kutokuwa na uhakika wa ufaulu katika masomo yao."

Aliongeza kuwa zoezi la awali la kuingiza taarifa zilizo kwenye “Selform” za wanafunzi kwenye kanzidata ya Ofisi ya Rais - TAMISEMI, kama zilivyojazwa wakiwa shuleni kabla ya kuhitimu limekamilika na sasa wanafunzi wataweza kufanya mabadiliko kwa njia ya mtandao, (online) na baada ya wanafunzi kufanya marekebisho yao, kanzidata hii ndiyo itakayotumika kuwachagua na kuwapangia kidato cha Tano na Kozi za Vyuo.

Waziri Jafo aliwakumbusha wahitimu wote  kuwa, endapo wanapenda kurekebisha machaguo ya Tahasusi na Kozi au kuhama kutoka Chuo kwenda Kidato cha Tano kulingana na ufaulu wao katika masomo wanatakiwa kuingia kwenye mfumo wa Selform unaopatikana katika anuani yawww.selform.tamisemi.go.tz na   maelekezo ya jinsi ya kufanya mabadiliko watayapata kwenye video ya mafunzo  inayopatikana kwenye tovuti ya TAMISEMIwww.tamisemi.go.tz

Pia alifafanua kuwa Ili mhitimu aweze kuingia kwenye mfumo itabidi kutumia namba ya mtihani wa kuhitimu Kidato cha Nne mwaka 2018, jina lake la mwisho, mwaka wa kuzaliwa na alama ya ufaulu aliyopata kwenye somo atakaloulizwa na mfumo au swali lolote atakaloulizwa. 

Zoezi hili la kubadilisha Tahasusi litafanyika kuanzia tarehe 01/04/2019 hadi tarehe 15/04/2019.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: