Serikali imewataka walimu wote nchini   kuacha kufanya vitendo vya udanganyifu wakati wa mitihani huku ikiwataka   wanafunzi kuhakikisha wanatoa  taarifa kuhusu vitendo vya udanganyifu vinapokiwa vinatokea.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati wa sherehe za Kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa shule ya sekondari Don Bosco Didia iliyopo mkoani Shinyanga.

Waziri Ndalichako amesema serikali inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na Mashirika ya kidini katika kuwaandaa vijana kitaaluma na kinidhamu na ndiyo maana hakuna vitendo vya udanganyifu katika mitihani kwenye shule hizo kwa kuwa wanafunzi wanaandaliwa vya kutosha pia wanamaadili.

“ Nichukue fursa hii Kuwasihi sana walimu nchini kote kuacha kufanya vitendo vya udanyifu wakati wa mitihani kwa sababu tunawaharibu watoto na na tunatengeneza vijana ambao hawana uwezo kitaaluma, kama tunawafanyia mitihani wakijakupata Kazi pia tutawafanyia Kazi?

“Nimependa Moto wa shule hii ya Don Bosco Didia kuwa ni kulea, kuwafunza nidhamu watoto kwa lengo la kutimiza ndoto zao naunga mkono juhudi zinazofanywa na viongozi wa shule hii sasa pia ni vyema na shule nyingine zikaiga,”alisisitiza Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako ameihakikishia Shule ya Sekondari ya Don Bosco kuwa serikali iko  pamoja kushirikiana na shule hiyo kwa kuwa mambo wanayoyafanya wanaunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya Tano.

Kwa upande Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga  Zainab Telack ameisifu shule hiyo ya Don Bosco kwa kuendelea kufanya vizuri katika mitihani ya kidato Cha nne na kuwa mkoa unajivunia sana kuwepo kwa shule hiyo ambapo amewasisitiza wanafunzi kuhakikisha wanaendelea kushirikiana ikiwa ni pamoja na kusoma kwa makundi pamoja na kuwasaidia wale ambao uwezo wao ni mdogo.

Katika kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 1993  Baba Vicent alisimikwa  rasmi kuwa Baba wa kiroho kwa ajili ya shule hiyo ya Sekondari.

Imetolewa na:
Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
6/10/2018
Share To:

msumbanews

Post A Comment: