Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema dhamira ya serikali ya kumuenzi baba wa Taifa Mwalimu Jullius K Nyerere kwa kuwa na Chuo Kikuu Cha kilimo, Sayansi na Teknolojia, (MJUNAT) iko palepale.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo akiwa Wilayani Butiama mkoani Mara mara baada ya kutembelea   Chuo hicho kwa lengo la kukagua Miundombinu yake, pamoja na kuzungumza na watumishi wanaofanya kazi chuoni hapo.

Akizungumza na Watumishi wa Chuo hicho pamoja na viongozi wa Mkoa na wale wa Wilaya ya Musoma na Butiama   amesema hivi sasa Serikali iko katika hatua za mwisho za makabidhiano ya Miundombinu hiyo  kutoka kwa aliyekuwa mmiliki wa majengo hayo Nimrod Mkono .

Waziri Ndalichako amesema lengo  la kuwa na Chuo Kikuu Cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia ni kumuenzi baba wa Taifa kwa kutambua mchango wake katika suala la kilimo na  kuwa suala hili pia limeanishwa kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi.


“Mchakato huu ulianza mwaka  2016 na kuwa hapo awali majengo haya yalikuwa yanamilikiwa na Nimrod Mkono, hivyo Serikali haiwezi kujenga au kuboresha bila kuwa na maandishi ya kisheria ya umiliki halali. Napenda kueleza kuwa makabidhiano yako katika hatua za mwisho ili serikali iweze kuendelea na taratibu nyingine” alisema Ndalichako.

Imetolewa na:
Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
27/10/2018
Share To:

msumbanews

Post A Comment: