Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng'anzi akitoa mada juu ya Mwanamke na Uongozi katika ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili ya Mtandao wa Polisi Wanawake (TPF NET) mkoa wa Arusha iliyofanyika wilayani Monduli.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ( SACP) Ramadhani Ng'anzi katikati akiwa katika picha ya pamoja na wawezeshaji wa mafunzo ya kumwezesha askari wa kike mkoa wa Arusha pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya kuwajengea uwezo askari Polisi wa kike Inspekta Halima (Mwenye mtandio kichwani) akichangia mada huku wenzake wakimsikiliza kwa umakini

Na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha

Askari Polisi wa kike mkoani hapa ambao pia ni wanachama wa TPF NET wamepongezwa kutokana na utendaji wao wa kazi katika nyanja mbalimbali ndani ya Jeshi la Polisi.

Hayo yameelezwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi alipokuwa  anafungua mafunzo ya siku mbili kwa ajili ya kuwajengea uwezo  katika Chuo cha Mafunzo cha Cyprus Hill kilichopo Monduli.

Kamanda Ng’anzi alisema kwamba askari hao wameweza kushika nyazifa mbalimbali ikiwemo kuwa wakuu wa upelelezi  na wakuu wa vituo ngazi ya wilaya mfano Monduli na Arumeru na hata katika ofisi mbalimbali ambapo wamefanya kazi kwa uaminifu na uadilifu.

 Alisema kwamba mifano hiyo itawafanya askari wa vyeo vya chini waweze kujiamini zaidi na semina hiyo itakuwa chachu ya kuwaongezea maarifa katika utendaji wao wa kazi za kila siku pamoja na kuwawezesha kutoa maamuzi sahihi wakati wote.

Kamanda Ng’anzi alisema kwamba askari hao wa kike si bora tu kwenye utendaji wa kazi za ndani ya nchi lakini pia baadhi yao wamewahi kuiwakilisha vyema nchi yetu kulinda amani katika nchi mbalimbali ikiwemo Sudani

Aliwataka askari hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili waweze kuzidi kusonga mbele zaidi kimadaraka huku akitolea mfano wa baadhi ya Makamanda wa Polisi wanawake katika baadhi ya mikoa lakini pia Kamishna Mstaafu wa Jeshi hilo (CP) Alice Mapunda.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtandao huo mkoani hapa, Mrakibu wa Polisi (SP) Namsemba Mwakatobe alisema kwamba lengo la mafunzo hayo ambayo yalihudhuriwa na washiriki 45 toka wilaya zote za mkoa huu ni kukumbashana wajibu wao katika utendaji wa kazi za kila siku lakini pia kubadilishana uzoefu ili kila mmojawao atimize wajibu wake ipasavyo.

Alisema Mtandao huo pia umeweza kuanzisha mfuko wa kusaidiana pindi mmojawao anapopata matatizo ambapo askari wengi wa kike wanajitokeza hali ambayo inaonekana kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwao.

Aidha kwa upande wa Madawati ya Kijinsia na Watoto Mwenyekiti huyo alisema kwamba wameweza kufanya vizuri hasa katika utoaji wa elimu juu ya unyanyasaji lakini pia kuwadumia wananchi kwa kiwango bora katika ofisi zao.

Naye Mtaalamu wa Jamii ambaye anahusika na mafunzo katika kituo cha Cyprus Hill cha shirika la Masai Stoves Bi. Meesha Kingolyo alisema kwamba, wao waliamua kujitolea kusaidia mafunzo hayo ili baadae jamii ipate elimu na kuondokana na mfumo dume ambao kwa kiasi kikubwa umewaaathiri wanawake na watoto ambapo baadhi yao hawapati masomo.

Alisema anaamini mara baada ya mafunzo haya jamii itakuwa na muamko juu ya usawa wa jinsia ambapo pia itasaidia wanawake na watoto wapate haki zao za kimsingi lakini pia anategemea kwamba kesi zitakazofikishwa Polisi zitasimamiwa vyema.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: