Mahakama ya Rufaa imetengua mauzo ya hisa za kampuni ya Mic Tanzania Limited (Tigo), zilizouzwa kwa kampuni ya Golden Globe International Services Limited.

Golden inayodaiwa kumilikiwa na mfanyabiashara Yusuf Manji ilinunua hisa34,479 za Tigo zenye thamani ya Sh13 bilioni mwaka 2014. Mauzo hayo yalikuwa utekelezaji wa hukumu katika kesi iliyofunguliwa na raia wa Uingereza, James Alan Russel Bell.

Uamuzi wa kutengua mauzo ya hisa hizo ulitolewa jana na jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo; Stella Mugasha (kiongozi wa jopo), Rehema Mkuye na Jacobs Mwambegele.

Mahakama ya Rufaa ilifikia uamuzi huo kutokana na mapitio iliyofanya baada ya kampuni ya Millicom (Tanzania) NV kumwandikia barua Jaji Mkuu ikilalamikia uuzwaji wa hisa hizo na madai mengine, ikidai kulikuwa na vitendo vya kughushi.

Kampuni ya Millicom (Tanzania) NV inadai ndiyo yenye hisa nyingi katika Mic Tanzania Limited.

Akisoma uamuzi huo kwa niaba ya jopo la majaji hao, Msajili wa Mahakama ya Rufaa, John Kahyoza alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahakama imejiridhisha kuwa malalamiko ya Millicom (Tanzania) NV kuhusu mauzo hayo yana mashiko.

Kahyoza alisema Mahakama imejiridhisha kuwa mchakato wa utekelezaji wa amri ya hukumu ya Mahakama Kuu iliyompa ushindi raia huyo wa Uingereza katika shauri la msingi la mwaka 2002 ulikuwa na kasoro zilizosababisha mauzo ya hisa hizo kuwa batili.

Alisema Mahakama inatengua mauzo ya hisa hizo na kuamuru mnunuzi arejeshewe fedha alizonunulia hisa na yeyote ambaye anazishikilia.

“Pia, tunaamuru hisa 34,479 halali zilizouzwa zirejeshwe kwa muombaji, Millicom (Tanzania) NV mara moja,” alisema Kahyoza akinukuu uamuzi wa majaji.

Mapitio yalifunguliwa na Jaji Mkuu kutokana na barua ya malalamiko ya Millicom (Tanzania) NV ambayo katika maombi ya mwenendo wa mapitio hayo ilitajwa kama mwombaji.

Wajibu maombi katika mapitio hayo walikuwa ni Bell, Golden Globe, Quality Group Limited, Mic UFA Limited, Millicom International Cellular S.A na Mic Tanzania Limited (Tigo).

Wakati wa usikilizwaji wa mapito hayo, Millicom Tanzania NV iliwakilishwa na mawakili Eric Ng’mario, Fayaz Bhojan na Gaudiosus Ishengoma wakati Mpaya Kamara na Joseph Ndazi waliiwakilisha Golden Globe International Services Limited.

Kampuni ya Quality Group iliwakilishwa na wakili Seni Malimi na Alex Mgongolwa; Millicom International iliwakilishwa na wakili Dk Wilbard Kapinga na Gasper Nyika huku Mic Tanzania Limited ikiwakilishwa na wakili Rosan Mbwambo.

Millicom (Tanzania) NV katika barua kwa Jaji Mkuu ilidai kulikuwa na vitendo vya kughushi katika mauzo ya hisa hizo na uhamishaji wake kutoka Tigo.

Mgogoro wa mauzo ya hisa hizo chanzo chake ni shauri la madai namba 306 la mwaka 2002, lililofunguliwa na Bell dhidi ya Mic UFA Ltd, Millicom International Cellular SA na Mic Tanzania Limited.

Katika hukumu iliyotolewa mwaka 2005, Bell alishinda madai dhidi ya Mic UFA Limited na Millicom International Cellular SA.

Kutokana na hukumu hiyo, Bell alifanya mchakato wa utekelezaji wa hukumu hiyo dhidi ya hisa katika Kampuni ya Tigo.

Hata hivyo, alishindwa baada ya Mahakama Kuu kupitia kwa Jaji Laurian Kalegeya, Novemba 7, 2009 kuamua kuwa hisa hizo hazikuwa zikimilikiwa na Millicom International Cellular SA, bali Kampuni ya Millicom Tanzania NV ambayo ni kampuni tofauti kisheria na haikuwa mdaiwa kwenye shauri hilo.

Februari 8, 2014 Bell alifungua maombi mengine ya utekelezaji wa hukumu hiyo dhidi ya hisa hizo ambazo alidai kuwa zilikuwa zinamilikiwa na Millicom International Cellular ndani ya kampuni ya Tigo. Juni 17, 2014 Mahakama Kuu iliteua kampuni ya udalali ya kushughulikia utekelezaji wa hukumu hiyo na ikatoa amri ya zuio la kukamata hisa zilizodaiwa kumilikiwa na Millicom International Cellular ndani ya Tigo.

Hisa hizo zilikusudiwa kuuzwa kwa mnada Novemba 5, 2014 kwa kampuni ya nje ya Golden Globe International Services na Novemba 10, 2014 na Mahakama ilitoa hati ya mauzo ya hisa hizo.

Kwa mujibu wa barua ya Millicom (Tanzania) NV, baada ya kubaini kuwa kampuni hiyo imenunua hisa zisizokuwapo, mnunuzi wa hisa hizo na dalali waliiomba Mahakama kutoa hati nyingine ya mauzo ya hisa ambayo jina la Millicom (Tanzania) NV liliingizwa.

Millicom (Tanzania) NV ilidai katika barua ya malalamiko kwa Jaji Mkuu kuwa mazingira yaliyozunguka uhariri wa amri iliyotolewa na Mahakama hiyo yanaashiria kuwapo kwa vitendo vya kughushi.

Ilidai jina Millicom (Tanzania) NV liliongezwa katika mwenendo wa shauri hilo kwa kalamu bila yenyewe kuwa mdaiwa kwenye kesi, bila kusikilizwa, wala bila kuitwa mahakamani.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: