WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe (pichani) amepeleka rasmi katika Kamati ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii, maombi ya kutaka Bunge kuruhusu wabunge wanaume kuvaa mashati ya vitenge, batiki na nyinginezo za asili ndani ya Bunge.

Hatua hiyo itaondoa sheria ya wabunge wanaume kuvaa suti, jambo linalowafanya kupata shida pale vipoza upepo vinaposhindwa kufanya kazi. 

Mwakyembe alisema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya sanaa na utamaduni iliyoadhimishwa ndani ya uwanja wa Maonesho ya 42 ya Biashara ya Kimataifa (DITF) yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam na kubainisha kuwa suala hilo likipitishwa na Bunge, litachochea kuongeza utengenezaji wa mavazi hayo pamoja na wajasiriamali kuwa wabunifu zaidi.

Alisema hatua hiyo itakwenda sambamba na uvaaji wa mavazi yenye rangi za taifa, hivyo maombi yakipelekwa na kukubalika yatachochea sanaa nchini. 

Dk Mwakyembe alisema kazi za sanaa na utamaduni katika maonesho ni fursa ya wanasanaa kuonesha ubunifu na vipaji walivyonavyo huku akibainisha siku kama hiyo mwakani wataitangaza zaidi ili kupata washiriki kutoka nchi nzima.

Alisema tamasha kubwa la sanaa katika nchi za Afrika Mashariki linalotarajiwa kufanyika Septemba au Oktoba mwakani, litafanyika katika viwanja hivyo, wataanza kujipanga ili kuangalia namna watakavyofanya kutokana na ukubwa wa uwanja huo.

Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya alisema maonesho ya mwaka huu yamefana katika sanaa kwani zamani watu walikuwa wanakusanya vya nje ya nchi na kuuza lakini sasa nyingi zimetengenezwa na watanzania wenyewe. 

Awali Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Edwin Rutageruka alisema wameamua kuwa na siku hiyo kwa ajili ya kutangaza sanaa za Tanzania huku akitaka wanautamaduni na wadau wa sanaa kutumia uwanja huo kwa shughuli mbalimbali.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: