Siku ya Ijumaa usiku wa tarehe 27 Julai, 2018, tukio la kupatwa kwa mwezi linatarajiwa kutokea ambapo nuru ya mwezi mkamilifu (full moon) itazuiwa na Dunia hivyo mwezi kuonekana kuwa na rangi nyekundu katika kipindi cha saa kadhaa kuanzia saa 4:30 usiku hadi saa 6:14 usiku.
Tukio la kupatwa kwa mwezi linatarajiwa kuonekana vizuri katika maeneo mengi ya Bara la Afrika, Asia na Ulaya. Hapa nchini Tanzania tukio hilo linatarajiwa kuonekana katika maeneo mengi na linatarajiwa kudumu kwa takribani saa mbili.
Kupatwa kwa Mwezi hutokea wakati Dunia, Mwezi na Jua vinapokuwa kwenye mstari mmoja. Hali hiyo inapotokea mwanga wa jua unaofika katika uso wa mwezi huzuiwa na duara la Dunia.
Katika mpangilio huo nuru ya Mwezi huonekana kuwa na giza (Total Lunar Eclipse). Hiyo ndio hali inayotarajiwa kujitokeza katika maeneo ya Bara la Afrika, Asia na Ulaya usiku wa tarehe 27 Julai 2018.
Kupatwa kwa Mwezi husababisha mabadiliko katika nuru ya mwezi na hivyo kufanya nuru ya mwezi kuwa hafifu(Partial Lunar Eclipse) au kuwa giza (Total Lunar Eclipse).
Kwa kuwa kupatwa kwa mwezi kutatokea kipindi Mwezi ukiwa mbali zaidi na Dunia, inatarajiwa kuwa tukio hili litaonekana kwa muda mrefu zaidi ukilinganisha na matukio mengine katika karne ya 21.
Mabadiliko katika hali ya hewa;
Kwa vile katika tukio hili mabadiliko katika nguvu za uvutano kati ya Dunia na Mwezi yatakuwa ni madogo kutokana na umbali mkubwa kati ya Mwezi na Dunia hali ya Bahari Kujaa (High tide) na Bahari Kupwa (Low Tide) haitarajiwi kuwa na mabadiliko makubwa, na pia hakuna mabadiliko makubwa yanayotarajiwa katika mifumo ya hali ya hewa.
Imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
Share To:

msumbanews

Post A Comment: