Sunday, 8 July 2018

Askofu Mkuu mwandamizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Yuda Thadeus Ruwa’ichi Kupokelewa Septemba 7

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema jimbo hilo linatarajia kumpokea Askofu Mkuu mwandamizi, Yuda Thadeus Ruwa’ichi, Septemba 7.

Kardinali Pengo alisema hayo jana wakati akiwapangia vituo vya kazi mapadri wapya na kuwabadilisha wale wa zamani baada ya sherehe za upadirisho, zilizofanyika katika viwanja vya Msimbazi Centre, jijini Dar es Salaam.

Juni mwaka huu, Papa Francis wa 16 alimtangaza Ruwa’ichi kuwa askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Kardinali Pengo alisema mapokezi hayo yatategemea ujio wa hati yake kutoka kwa Papa Mtakatifu Francis wa 16, pamoja na yeye mwenyewe kuweka tayari vitu vyake.

“Kwa hiyo tarehe hiyo inaweza kubadilishwa kwa sababu hizo mbili,” alisema.

Kadhalika aliwataka vijana wa kanisa hilo kukimbilia upadri kwa sababu huko kuna uhakika wa ajira.

“Vijana kimbilieni huku kuna uhakika wa ajira, huku siyo kama huko kwingine kwa hiyo ni wakati wenu. Ninyi mapadri wapya nawapa likizo ya siku 28 ili muende huko mkamshukuru Mungu,” alisema Kardinali Pengo.

Aliwataka mapadri wapya kuwa tayari kufanya kazi mahali popote watakapotumwa ili waendelee kutenda kazi ya Mungu.

No comments:

Post a Comment