Friday, 8 June 2018

Wamiliki Viwanda Mikocheni wapewa mwezi mmoja


WAMILIKI wa viwanda eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam wamepewa mwezi mmoja kutatua kero ya uchafuzi wa mazingira kwa kudhibiti utiririshaji wa majitaka unaohatarisha afya za wakazi wanaoishi kabla ya kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria.

Agizo hili lilitolewa jana na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola, baada ya kutembelea viwanda vya Iron and Steel Ltd na MMI Integrated Mills Ltd vilivyopo maeneo ya Mikocheni ‘B’ kujionea uchafuzi wa mazingira.

Akizungumza mara baada ya ziara yake ya ghafla, Lugola alisema hakuridhishwa na namna viwanda hivyo vinavyolinda mazingira na afya ya wananchi, hivyo kutoa mwezi mmoja kurekebisha hali hiyo.

“Nawaagiza wamiliki wa viwanda hivi wakutane na watendaji wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) mara moja kujadili namna ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira, utirirshaji wa maji machafu, moshi na kuutatua kero hii ya muda mrefu kwa wananchi,” alisema Lugola.

Alisisitiza wamiliki hao wanapaswa kuhakikisha wanatengeneza mpango mkakati wa kuyatibu maji machafu na kuhakikisha moshi wa viwandani hauleti madhara kwa wananchi na kuwataka kumpelekea taarifa ya utekelezaji huo ndani ya mwezi mmoja.

Aliwakumbusha wamiliki wa viwanda kwamba kabla ya kuwekeza shughuli za viwanda nchini, wanapaswa kujua namna ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira na hawaruhusiwi kudhuru afya za wananchi bali wafuate sheria za mazingira na kuzitekeleza kikamilifu na kuongeza kuwa serikali ya Rais John Magufuli sio ya kuchezewa, inamaanisha kuwatumikia wananchi.

Naibu Waziri alimweleza meneja uzalishaji wa kiwanda cha Iron & Steel Ltd, Johari Badri kufuata sheria, kanuni na taratibu

za uendeshaji wa viwanda na kwamba agizo hilo ni la mwisho kulitoa na hatakuwa na msamaha tena kwani mara nyingi mmiliki huyo ameendelea kukaidi maagizo ya serikali licha ya kupigwa faini za mara kwa mara.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa serikali za mitaa Mikocheni ‘B’ Manispaa ya Wilaya ya Kinondoni, Sixbert Qamdiye, alisema wananchi wa maeneo yake kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia kero ya uchafuzi wa mazingira na maji machafu yanayotokana na viwanda hivyo licha ya ofisi yake kuchukua hatua mbalimbali kutatua kero hizo.

Amemshukuru Lugola  kwa kufanya ziara katika baadhi ya maeneo hayo ya viwanda na kutoa maagizo kwa NEMC na wamiliki wa viwanda hivyo kukutana na kujadili suala hilo ambalo anaamini mapendekezo yatakayotolewa yatatatua kero hizo.

Naye Mratibu wa NEMC wa Mazingira Kanda ya Mashariki, Jafar Chimgege, alisema eneo la Mikocheni ‘B’ lina viwanda vingi na kusisitiza wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali kushughulikia usafi wa mazingira katika maeneo hayo na kuhakikisha wamiliki wa viwanda husika wanatekeleza sheria ya mazingira ili kulinda afya za wananchi wanaoishi karibu na viwanda.

No comments:

Post a Comment