Friday, 25 May 2018

ZAIDI YA BILIONI NNE KUTUMIKA KWENYE MIRADI YA UTAFITI


Serikali imetoa zaidi ya bilioni Nne kwa ajili ya Taasisi na Watafiti walioshinda maandiko ya miradi  8 ya utafiti ambayo itaanza kufadhiliwa mwaka huu wa fedha.

Akizungumza jijini Dar es Salaam kabla  ya kukabidhi hundi kwa Taasisi zilizoshinda fedha hizo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa. Joyce Ndalichako amesema miradi yote iliyopata fedha ni ile ambayo ina malengo madhubuti ya kuimarisha uchumi wa viwanda hadi ifikapo 2025.

Waziri Ndalichako amesema  kufadhiliwa kwa miradi hiyo nane kutaleta mchango mkubwa wa uzalishaji wa dawa nchini na kupunguza uagizwaji wa dawa kutoka nje, uboreshaji wa maabara za uhandishi jeni, kuongeza ushindani wa bidhaa, kuongeza uzalishaji wa mazao, uzalishaji wa mimea, pamoja na kuchangia katika uanzishwaji wa viwanda.

Wazizri Ndalichako amezitaka taasisi zilizopata fedha hizo kuzitumia kwa uadilifu na kwa malengo yaliyokusudiwa na siyo vinginevyo.
Miradi hiyo nane ni pamoja na ule wa umaliziaji wa kiwanda cha uzalishaji wa dawa na maabara ya utafiti ya mabibo, uimarishaji wa miundombinu ya utafiti na ugunduzi wa dawa katika chuo kikuu cha tiba (MUHAS), Muhimbili, ununuzi wa vifaa na uboreshaji wa maabara ya uhandisi jeni ya Taasisi ya Mifugo TALIRI kwa ajili ya kuongeza kasi ya uzasihaji wa mifugo, Uboreshaji wa maabara ya Chanjo ya Taasisi ya Taifa Kibaha.

Miradi mingine ni Uboreshaji wa maabara ya udongo, ili kuimarisha Afya ya Udongo kwa ajili ya kilimo endelevu kwa lengo la kuimarisha uchumi wa viwanda,Uboreshaji wa maabara ya kisasa ya utafiti wa mbogamboga na matunda kaskazini mwa Tanzania (HORTI Tengeru), Ukarabati wa mtambo  wa utafiti wa kutengeneza mvinyo  katika taasisi ya utafiti wa kilimo, Makutopora na uboreshaji wa usimamizi wa maabara za uchakataji wa mazao ya taasisi ya utafiti wa viwanda TIRDO.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi  Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia, COSTECH Dk. Amos Nungu amesema kuwa moja ya jukumu la tume hiyo ni kuratibu shughuli za sayansi na teknolojia kupitia ufadhili wa miradi ya utafiti.

Dk. Nungu amesema jumla ya Tungo, (Proposal) 155 kwa kutumia vigezo vilivyoainishwa tungo 86 tu ndizo zilizokidhi vigezo vya kupelekwa kwa wataalamu kwa mapitio na uchambuzi.

Amesema hata hivyo kati ya tungo zote hizo miradi 8 tu ndiyo iliyokidhi kupata fedha hizo kiasi cha zaidi ya bilioni 4 kwa kuzingatia michango itakayotokana na miradi hiyo katika dira ya nchi yenye lengo la kuendeleza viwanda, kuimarisha uchumi ili kuboresha maisha ya watanzania.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU,SAYANSI NA TEKNOLOJIA
25/05/2018

No comments:

Post a comment