Monday, 21 May 2018

OKWI AMWAGA MACHOZI TAIFA SABABU YA KASEJA


Straika wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi aliangua kilio mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli baada ya kukosa penalti iliyopanguliwa na kipa wa Kagera Sugar, Juma Kaseja.

Simba ilijikuta ikilala bao 1-0 Kagera Sugar kwenye mchezo huo uliopigwa jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kuzima ndoto yao ya kumaliza Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza mechi baada ya kufungwa kwa mara ya kwanza msimu huu.

Simba ilipata penalti baada ya Okwi kuchezewa rafu na George Kavila wa Kagera Sugar ambayo aliipiga lakini ilipanguliwa na Kaseja, ambaye ni kipa wa zamani wa timu hiyo.

Hatua hiyo ilikuwa pigo kwa Okwi kwani aliipotezea nafasi timu yake ya kusawazisha baada ya Kagera Sugar kuongoza kwa bao lililopachikwa na Edward Christopher katika dakika ya 85.

Mganda huyo alitoka uwanjani huku akilia na wenzake wakimbembeleza kutokana na kupoteza penalti hiyo.

Okwi pia alikuwa na hisia kali za kumbukumbu kiungo wa zamani wa Simba, Patrick Mafisango, ambaye alizikwa siku kama ya leo Mei 20, 2012 nchini Congo baada ya kufariki kwa ajali ya gari jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a comment