Serikali imesema inakemea vitendo vya udhalilishaji na ubakaji wa aina yeyote ambao wanafanyiwa watoto na wanawake huku wakiwataka wahanga wa matukio hayo kutokaa kimya bali wakatoe taarifa kwenye vyombo dola ili sheria zipate kuchukuliwa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mh. Dkt. Faustine Ndugulile Bungeni Jijini Dodoma kwenye kikao cha 28 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalum, Mwantumu Haji ambaye alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kupambana na wanaume wanaowadhalilisha watoto.

"Ni kweli lipo ongezeko la matukio ya ubakaji na udhalilishaji wa wanawake na watoto. Serikali inaendelea kuhamasisha utekelezaji wa sheria ya kanuni za adhabu sura Na. 16 na sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009 na kuhimiza wazazi walezi, jamii na wahanga wa vitendo vya ukatili kutokaa kimya pindi wanapoona mtoto au mwanamke anafanyiwa vitendo hivyo ili kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa wale wote wanaotenda vitendo hivyo", amesema Dkt. Faustine.

Pamoja na hayo, Naibu Waziri Dkt. Faustine ameendelea kwa kusema "katika kipindi cha Januari hadi Disemba mwaka 2017, Jeshi la Polisi limeripotiwa kuwapo na jumla ya matukio 41,416 ya ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake lakini kati ya hayo matukio 13,457 ni ya ukatili wa kijinsia kwa watoto na serikali inaendelea kukemea udhalilishaji na ubakaji wa aina yoyote kwa wanawake na watoto".

Kwa upande mwingine, Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mh. Dkt. Faustine Ndugulile ametoa rai kwa wananchi wote nchini Tanzania amewataka kuacha tabia ya kumaliza mashauri ya kesi yaliyopo kwenye vyombo dola katika ngazi za kifamilia.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: