Thursday, 10 May 2018

Naibu Spika aagiza wateja wa benki iliyofungwa walipwe


NAIBU Spika, Dk. Tulia Ackson, ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kutatua changamoto ya kutolipwa kwa wateja wa benki ya FBME ambayo imefungwa na Benki Kuu (BoT).

Kiongozi huyo alitoa agizo hilo bungeni jijjini Dodoma jana alipokuwa anajibu mwongozo ulioombwa kwake na Mbunge wa Muyuni, Jaku Hashim Ayoub (CCM).

Mbunge huyo alitaka mwongozo wa Kiti cha Spika, ili serikali ieleze ni lini hasa wateja wa benki hiyo kwa upande wa Zanzibar watalipwa fedha zao.

“Kwa sababu amelizungumza hapa na ni wananchi wanaopata tabu, Wizara ya Fedha imesikia, impatie Mheshimiwa Jaku ufafanuzi kuhusu jambo hili ili na yeye aweze kuwafafanua wapigakura wake," alisema.

Kabla ya kuombwa mwongozo wa Kiti cha Spika kuhusu jambo hilo, Jaku kuwa kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, wateja wa benki hiyo kwa upande wa Zanzibar hawajalipwa chochote, “Nataka kujua wateja hawa watalipwa lini na je, fedha zao ziko salama kweli?" Jaku alihoji.

Novemba mwaka jana, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alisema serikali imetenga Sh. bilioni 728 kwa ajili ya kuwafidia wateja 695 wa benki hiyo.

Akizungumza bungeni kipindi hicho, Dk. Kijaji alisema malipo kwa wateja hao yanafanyika kwa mujibu wa Kifungu cha 39 cha Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.

“Serikali haina mpango wa kumwonea mteja yeyote. Madeni yote yatakusanywa na fedha italipwa kwa wateja kulingana na kiwango walichoweka na kwa kuzingatia matakwa ya sheria. Serikali inalifanyia kazi suala hili kwa uangalifu mkubwa," alisema.

Dk. Kijaji alitoa maelezo hayo bungeni alipokuwa anajibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Rukia Kassim Ahmed (CUF), ambaye alitaka kujua malipo kwa wateja wa benki hiyo yatafanyika lini baada ya leseni yake kufutwa na serikali mwaka jana.

Mei 8, mwaka jana, Benki Kuu (BoT) ilitangaza kuzuia shughuli za FBME na kuiweka chini ya uangalizi maalum baada ya serikali ya Marekani kuituhumu benki hiyo kujihusisha na utakatishaji mkubwa wa fedha.

BoT iliingilia utendaji wa benki hiyo Julai 2014 kufuatia ripoti ya Mtandao wa Udhibiti wa Fedha Haramu wa Marekani (U.S. Treasury’s Financial Crimes Enforcement Network -FinCEN) kuitaja benki hiyo kuwa sehemu ya taasisi kubwa za utakatishaji fedha.

Benki hiyo ilifungua mashtaka kupinga tuhuma hizo, lakini mahakama ya Marekani ilitoa uamuzi uliokuwa upande wa FinCEN Aprili, ikiruhusu kufungwa kwa mfumo wa benki hiyo Marekani

No comments:

Post a comment