Friday, 18 May 2018

Kilauea: Volkano yarusha mawe makubwa angani Hawaii, Marekani

Mlipuko mkubwa ulitokea katika volkano ya Kilauea katika jimbo la Hawaii nchini Marekani na kuzua wasiwasi zaidi eneo hilo.

Mlipuko huo ulirusha majivu futi 30,000 (9,100m) juu angani. Aidha, ulirusha juu mawe makubwa wa kilo kadha, na baadhi inakadiriwa kuwa yanaweza kuwa na uzani wa tani kadha.

Mlipuko huo ulitokea mwendo wa saa kumi na robo alfajiri saa za huko, Wanasayansi wanasema bado kuna uwezekano mlipuko mwingine unaweza kutokea.

Watu waliokuwa wakifanya kazi katika kituo cha kufuatilia volkano hiyo waliokuwa kwenye mbuga ya taifa ambapo kunapatikana volkano hiyo wamehamishwa.

Shirika la Jiolojia la Marekani linasema mawe ya ukubwa wa hadi 60cm (2ft) yalionekana hatua kadha kutoka kwenye shimo la mlipuko wa volkano hiyo.

Lakini walitahadharisha kwamba huenda mambo yakawa mabaya zaidi, "Wakati wa milipuko ambayo imesababishwa na mvuke, mawe ya ukubwa wa hadi 2m yanaweza kurushwa pande zote umbali wa 1km au zaidi," shirika hilo lilisema.

"Mawe hayo yanaweza kuwa na uzito wa kilo kadha hadi tani kadha. mawe madogo yanaweza kurushwa mbali, kilomita kadha."


Tangu milipuko ya volkano ilipoanza kutokea eneoi jipya Kilauea, matope yenye moto yamekuwa yakimwagika na kuharibu mamia ya nyumba eneo hilo na kulazimu maelfu ya watu kuhamishwa.

Tahadhari ya kiwango cha juu zaidi imetolewa, na marubani wa ndege wameonywa kuhusu hatari inayoweza kutokana na 'wingu' la majivu ya volkano hiyo.

Shirika la Jiolojia la Marekani lilikuwa limeonyesha kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kutokea mlipuko mkubwa eneo hilo.

Hii ni baada ya kina cha 'ziwa la matope moto' kwenye vilkano hiyo kuonekana kupungua na kuongeza uwezekano wa maji yanayopatiukana chini ya ardhi kukutana na matope hayo moto chini ya ardhi, maji yakijaribu kujaza mianya inaoachwa wazi na kupungua kwa matope hayo.

Shirika la huduma za dharura Hawaii liliwatahadharisha watu walio maeneo yaliyoathiriwa na majivu hayo kusalia ndani ya nyumba zao.

Kilauea ni moja ya volkano tano ambazo bado hulipuka katika kisiwa cha Hawaii, Ni moja ya milima inayolipuka sana duniani na imekuwa ikilipuka mara kwa mara ingawa hakujakuwa na mlipuko mkubwa kwa miaka zaidi ya 30.


Mlipuko wa mwisho mkubwa eneo hilo ulitokea 1924, Hata kabla ya mlipuko huo wa Alhamisi, majivu kutoka kwa volkano hiyo yalikuwa yanaweza kuonekana kutoka kituo cha kimataifa cha anga za juu (ISS).

No comments:

Post a comment