Friday, 11 May 2018

Kenya kutimiza ndoto ya kurusha satelaiti yake leo

Kenya inajiandaa kutimiza ndoto kubwa ya kisayansi leo Ijumaa (Mei 10 2018) ya kurusha Chombo cha Satelaiti kilichoundwa nchini humo.
Wanasayansi wa anga za juu kutoka Kenya waliokiunda chombo hicho tayari wako katika makao ya Uchunguzi wa Sayansi ya Anga za juu nchini Japan, (JAXA) ambapo chombo hicho kitarushwa kutoka huko.
Nchini Kenya kwenyewe raia wataweza kufuatilia shughuli hiyo moja kwa moja kwenye mtandao wa You Tube, na sherehe maalumu ya kushuhudia imeandaliwa katika chuo kikuu cha Nairobi.
Satelaiti hiyo ndogo ni ya thamani ya dola milioni moja – gharama inayoonekana kuwa ndogo kifedha kwa kiwango cha sayansi ya anga za juu.
Wahadhiri wa vyuo vikuu wanasema satelaiti hiyo inaweza kutoa huduma tofuati ikiwemo kukusanya taarifa zitakazosaidia katika kilimo na usalama, kutabiri hali ya hewa na hata kukabiliana na majanga.
Kenya kwa sasa inakabiliwa na janga la mafuriko ambalo limesababisha maafa makubwa.
Takriban watu mia mbili wamepoteza maisha yao, huku wengine zaidi ya laki mbili wamepoteza makaazi yao.
Huenda ufanisi katika uzinduzi wa satelaiti hii utaisaidia serikali pakubwa katika kujitayarisha kupambana na majanga ya aina hiyo.

No comments:

Post a comment