Wednesday, 16 May 2018

Hakimu atoa sababu za kukataa kujitoa katika kesi ya Nondo


Hakimu John Mpitanjia anayesikiliza kesi ya kujiteka na kusambaza taarifa za uongo katika mitandao ya kijamii, inayomkabili Abdul Nondo, amegoma kujitoa katika kesi hiyo kwa sababu za kumkataa ni za kufikirika na hazina mashiko.

Juzi, mshatakiwa huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi (TSNP), aliandika barua ya kumkataa hakimu huyo kujitoa kutokana na kutokuwa na imani naye ambapo alitoa sababu tano akidai ukaribu wake na Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Iringa na shahidi wa tatu katika kesi hiyo, Paul Kisapo unatia shaka.

Akitoa uamuzi huo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa,  Hakimu Mpitanjia amesema sababu alizotoa mshtakiwa hazina msingi wowote na ataendelea kusikiliza shauri hilo kwani akijitoa haki itachelewa.

“Sababu walizotoa upande wa utetezi ni za kufikirika ambazo hazina ushahidi wowote na kwa kuwa mahakama ni chombo cha mwisho katika kutenda haki na kuwahisha haki, nitaendelea kusikiliza shauri hili ili niwahishe haki ya mshtakiwa kwa mujibu wa sheria,” amesema Hakimu Mpitanjia.

Akizungumzia uamuzi huo wa mahakama, Wakili wa Nondo, Jebra Kambole, amesema upande wa utetezi wamepokea uamuzi wa mahakama na hawawezi kuupinga ila kama kutakuwa kuna ulazima wa kufanya jambo lolote la kisheria watatumia njia nyingine za kupata haki yao.

“Kwa sasa tunaona shauri liendelee tu ili mshtakiwa aendelee na mambo mengine, kama anafungwa afungwe na kama anaachiwa aachiwe akaendelee na shule,” Jebra Kambole

No comments:

Post a comment