Tuesday, 29 May 2018

Dk. Tulia asema Wabunge hawakuwa na taarifa za Bilago

Naibu spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Tulia Ackson amesema kuwa msiba wa aliyekuwa mbunge wa Kakonko  Samson Bilago umepokelewa kwa mshtuko kutokana na wabunge wengi kutokuwa na taarifa za ugonjwa wake.

Dk. Tulia amesema hayo wakati wa ibada ya kuaga mwili wa marehemu Bilago katika viwanja vya bunge Jijini Dodoma, marehemu aliugua na taarifa ziliufikia uongozi wa Bunge na taratibu zilianza za kushughulikia matibabu lakini ni wabunge wachache ambao walikuwa na taarifa hizo.

“Marehemu Bilago aliugua akapelekwa hospitali hapa Jijini Dodoma ,lakini baadae hali yake ilibadilika na kupelekwa hospitali ya taifa muhimbili ambako hakuchukua muda mrefu akafikwa na mauti, jambo ambalo wabunge wengi wamelipokea kwa mshtuko taarifa hizi kutokana na kutokuwa na taarifa”, amesema Dk. Tulia.

Marehemu Bilago alifariki Mei 26 mwaka huu katika hospitali ya taifa ya muhimbili ambako alikuwa akipatiwa matibabu ya mishipa, mwili wake umeagwa bungeni leo na kuanza safari ya kuelekea Mkoani Kigoma kwaajili ya shughuli ya maziko.

No comments:

Post a comment