BARAZA la Madiwani wa  Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, limepitisha sheria ndogo itakayomlazimu binti anayetaka kuolewa kuonyesha cheti cha kuzaliwa kwanza kitakachomwezesha mwenyekiti wa kijiji kutoa kibali au la.

Uamuzi wa kupitisha sheria hiyo ulitolewa juzi na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ngassa Mboje, kwenye mkutano wa Shirika la

Agape la kutetea haki za watoto mkoani Shinyanga, uliohusisha madiwani wa Manispaa ya Shinyanga, vijiji, maofisa maendeleo ya jamii na wakuu wa shule, uliokuwa na lengo la kujadili namna ya kumkomboa mtoto wa kike kielimu.

Alisema baada ya kuona tatizo la ndoa na mimba za utotoni linaendelea kushamiri kwenye wilaya hiyo, wakaona ni vyema kutunga na kupitisha sheria ndogo ambayo itawabana wazazi kushindwa kuozesha mabinti zao walio chini ya umri wa miaka 18 kwa tamaa ya mifugo na mali.

“Sheria ya Ndoa ya mwaka (1971) siyo rafiki kabisa kumlinda mtoto wa kike, ina ruhusu kuolewa akiwa chini ya umri wa miaka 18 kwa ridhaa ya wazazi wake au mahakama, na hivyo kusababisha kuendelea kuwepo kwa ndoa nyingi za utotoni, na kukatisha ndoto za wanafunzi wa kike,” alisema Mboje.

“Baada ya kuona sheria hiyo ni tatizo, sisi baraza letu ikabidi tutunge sheria na kuipitisha na inafanya kazi sasa, kuwa hakuna mzazi kuozesha binti yake bila ya kutoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya kijiji, pamoja na kuonyesha cheti chake cha kuzaliwa ili kujiridhisha kama hayupo chini ya umri miaka 18 na hasomi,” aliongeza.

Ofisa Mradi wa kutokomeza mimba na ndoa za utotoni kutoka Shirika la Agape mkoani hapa, Mustapha Isabuda, alisema wameamua kukutana na madiwani hao kuonyesha ukubwa wa tatizo ulivyo, ili wapate kuguswa na kutunga sheria ndogo za kubana wazazi kuozesha watoto.

Aidha, aliwataka madiwani wanapokuwa wanapitisha bajeti zao la kila mwaka wa fedha, wahakikishe suala la elimu wanalipatia kipaumbele kwa kulitengea bajeti kubwa, ili kuondoa upungufu wa ujenzi wa matundu ya vyoo na vyumba vya kujisitiri hedhi na vitaulo vya kujihifadhi wanafunzi wa kike.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Geofrey Mwangulumbi, alilipongeza Shirika hilo kwa kumpigania mtoto wa kike apate kusoma, na kuahidi watatunga sheria hizo ndogo kupitia Mwanasheria wao. 
Share To:

msumbanews

Post A Comment: