Saturday, 14 April 2018

TLS Yakerwa na Kanuni za Uchaguzi.......yapendekeza kuonana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali


Kamati ya Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, (TLS) iliyoundwa kujadili uamuzi wa Mwanasheria wa Mkuu wa Serikali (AG)wa kuzifanyia mabadiliko kanuni za uchaguzi wa chama hicho imesema, AG hakuwa na mamlaka ya kufanya mabadiliko yoyote.

Hayo yameibuka leo Aprili 14 wakati wa uchaguzi wa kumpata Rais mpya wa chama hicho, mjini Arusha.

Katika tukio hilo,  Makamu wa Rais wa sasa wa TLS, Godwin Ngwilimi, ametoa hoja hiyo na kumtaka mjumbe wa Baraza la uongozi, Jeremiah Mtobesya kusoma mapendekezo hayo ambayo yalisema Mwanasheria Mkuu wa serikali hakuwa na Mamlaka ya kufanya mabadiliko bali kuyachapisha kwenye gazeti la serikali.

Pia walipendekeza kufuata njia za kiutawala kuonana na Mwanasheria Mkuu au kwenda mahakamani kutafuta tafsiri ya mamlaka yake kwa TLS.

Mgombea Urais wa TLS, Fatma Karume amesema maboresho yaliyofanywa hayana msingi wa kisheria kwa kuwa kanuni za uchaguzi wa TLS zinaanza kufanya kazi mara tu baada ya kupitishwa na mkutano mkuu.

Hata hivyo wajumbe hao walikubaliana na baraza la uongozi kutengeneza kanuni ambazo zitatamka kuwa si lazima zitangazwe kwenye gazeti la serikali ili ziwe halali.

No comments:

Post a comment