Mratibu wa Sehemu ya Elimu Maalum Ofisi ya Rais TAMISEMI, Julius Migea amesema Serikali imeanzisha Mpango wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wenye mahitaji maalum ili kuwabaini na kuwawezesha kumudu stadi hizo muhimu kwa maendeleo yao na Taifa.

Migea aliyasema mjini Dodoma wakati wa kuanza rasmi kwa zoezi hilo lenye lengo la kuwabaini watoto wenye mahitaji maalum kama uoni hafifu, viungo vya mwili, kutosikia, kushindwa kuongea na matatizo mengine.

“Mpango huu wa kukuza stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) ulianzishwa kwa lengo la kukabiliana na kiwango duni cha kumudu stadi hizo za msingi kilichobainika miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi nchini, na watoto waliolengwa ni wenye umri kati ya miaka mine hadi sita”

Migea alisema kuwa uendeshaji wa uchunguzi wa nchi nzima kwa watoto wenye umri wa miaka 4 hadi 6 ni kwa ajili ya kuwabaini watoto wenye mahitaji maalum ili waweze kupatiwa afua stahiki ikiwa ni pamoja na kuwaandikisha shule stahiki. Kwa hivi sasa, tayari timu za maafisa waliopewa mafunzo maalum zimekwisha kwenda katika mikoa na halmashauri zote nchini na wameanza kuwabaini watoto hao wenye mahitaji maalum wanaoishi katika kata, vijiji, vitongoji na mitaa.

Mmoja wa Waratibu wa kazi ya kubaini watoto wenye mahitaji maalum Stephen Mwendi amesema zoezi la kubaini watoto wenye mahitaji maalum mkoani Dodoma linaendelea vizuri katika wilaya ya Kondoa Mji na Halmashauri ya Kondoa, baada ya kumaliza Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma na baada ya hapo watakwenda katika halmashauri nyingine za mkoa wa Dodoma.

“sisi tunaendelea vizuri na zoezi la kuwabaini watoto wenye mahitaji maalum katika Halmashauri ya Mji Kondoa na Halmashauri ya wilaya ya Kondoa na tunatarajia zoezi litakamilika kwa wakati kwani vituo karibu vyote vinafikika”

Mwendi pia amezitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili katika zoezi hilo kuwa ni za kawaida lakini wanatarajia taarifa ya mwisho itawasilishwa Serikalini ili kuifanyia kazi kwa wakati katika sekta hiyo muhimu.

“muda wanaofika walengwa wakati mwingine wanafika tukiwa tumeondoka na kutulazimu kuwarudia tena, pia mahitaji yaliyoanishwa katika ubanishaji ni miaka 4 hadi 6 lakini tunakutana na watoto wengi wa umri zaidi ya miaka 10, 18 ijapokuwa kwa kuwaangalia wanakuwa na maumbo madogo kama watoto na vile vile wengi wa wazazi wanafikiria kuwa zoezi hilo ni kwa ajili ya kuwapatia misaada jambo ambalo si kweli na hivyo tunaendelea kuwaelimisha”

Mmoja wa wazazi walioleta watoto katika Halmashauri ya Kondoa Mji, mama wa Abubakari Hussein amesema mwanaye alipata ulemavu wa viungo alipokuwa na miaka 4 hadi sasa ambapo ana miaka 16 anapatanaye shida sana na anaoimba Serikali imsaidie kumsomesha mtoto huyo na kumpatia mahitaji madogo madogo kwani anaishi katika nyumba ya kupanga, lakini pia Serikali iwajengee shule maalum kwa ajili ya watoto wa aina hiyo ambao wamevuka umri wa kuandikishwa wa miaka 4 hadi 6.

Katika Halmashauri ya wilaya ya Kondoa kata ya Mnenia, mmoja wa wazazi, Mussa Dudu amesema mjukuu wake Haji Twalib ambaye anatatizo la kichwa kikubwa, kutokuongea vizuri na tumbo kuwa kubwa amepata ushauri wa kitaalam ikiwa ni pamoja na kujaza fomu ya kumwona daktari na fomu ya kujiunga na shule na ametoa maoni kwa Serikali kufanya utafiti zaidi kwani kuna baadhi ya wazazi wanaficha watoto wao wenye ulemavu (mahitaji maalum) majumbani.

“nashukuru juhudi za Serikali kwa zoezi hili zuri kwani kijana wangu (mjukuu) hakuwahi kupata uchunguzi wowote, nimepata fomu ya ubainishaji ili niende hospitali na kupeleka shuleni, Serikali pia itupe msaada ili kuweza kuwahudumia watoto hawa na pia Serikali ifanye uchunguzi kamili kwani kuna watoto wanafichwa tu na wazazi hawahamasiki wanasema huyu ni mlemavu tampeleka wapi. Pia natoa wito kwa Serikali kuwatumia Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji ili kuweza kuwafichua wototo kama hao”  

Ubainishaji wa kundi la watoto wa aina hii kawaida unatakiwa kufanyika kabla ya zoezi la uandikishaji ili wapatiwe afuastahiki, kwani awali zoezi hili lilikuwa halifanyiki kabla ya kuanza masomo na kupelekea watoto wenye changamoto za kujifunza kutokuwa na maendeleo mazuri ya kitaaluma, kuacha masomo, kutopenda masomo na kukosa haki yao ya msingi kutokana na kuwa katika mazingira yasiyo rafiki ya kusomea.

Serikali imekuwa ikitekeleza Mipango mbalimbali katika sekta ya elimu, ambapo kwa hivi sasa kupitia Mpango wa Kukuza stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (Literacy and Numeracy Education Support – LANES) inatekeleza mikakati ya kuhakikisha wanafunzi wote walioandikishwa shule za Msingi wanapata stadi za KKK ambazo ni msingi muhimu wa maendeleo ya kitaaluma katika ngazi zingine za Elimu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: