Saturday, 7 April 2018

Rais Magufuli Awapiga Marufuku Polisi Kufyeka Mashamba ya Bangi

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka maofisa wa Jeshi la Polisi na Makamishna wake kutoyafyeka na kuyachoma moto mashamba ya bhangi na badala yake watumie njia za kiintelijensia kuwababini watuhumiwa, kuwakamata na kuwashughulikia ikiwa ni pamoja na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Rais ameyasema hayo leo wakati akiwahutubia wananchi wa Arusha katika Uwanja wa Amri Abeid baada ya kuzindua kituo cha polisi na nyumba za polisi mkoani humo.

“Hakuna kitu kinachonikera kama Askari Polisi kwenda kufyeka mashamba ya bhangi, makamanda wako na askari wako, wasikate mashamba ya bangi, hawakuajiriwa kufyeka bhangi. Niwashauri tu kwamba, tumieni njia za kintelijensia, mtawashika tu, kama shamba lipo karibu na kijiji, kamata kijiji kizima, wazee, vijana, wanawake hata na watoto, ndio wakafyeke hilo shamba la bhangi.

“Nasema askari wasiende kufyeka bhangi, hawakuajiriwa kufyeka bhangi, usiwatume askari wako kufyeka bhangi, wataumwa nyoka bure, wamevaa uniform nzuri, msidhalilishe jeshi kwa kufyeka bhangi, mimi nisingefyeka bhangi na wa kufyeka wapo.

“Nilimuona Waziri naye yumo anafyeka na kuchoma moto shamba la bhangi, juzi nikaona tena RPC wa Dodoma naye anafyeka shamba la bhangi na askari wake, mpaka akachoka anasema hili shamba lililobaki tutalimalizia kesho. Inashangaza sana, tusijidhalilishe hivyo,” alisema Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amelitaka Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya Usalama kuendelea kuimarisha hali ya amani nchini na kuwatumikia Watanzania kwa maendeleo ya Taifa.

No comments:

Post a comment