Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Kuhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) inamshikilia ofisa wa jeshi la polisi kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya zaidi ya Sh. 250,000.

Akizungumza na waandishi wa habari, Ofisa Uhusiano wa ZAECA, Mwanaidi Suleiman Ally, alisema ofisa huyo Rajabu Juma Simba, mkazi wa Meli Nne-uzi, kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya zaidi ya Sh. 250,000 kutoka kwa vijana wawili ambao majina yao yamehifadhiwa.

Alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 4.30 asubuhi nje ya kituo cha polisi cha Mwanakwerekwe, baada ya kuwakamata na chombo walichokuwa nacho aina ya Pasola, kwa kuwatuhumu wanaenda kununua dawa za kulevya aina ya bangi.

Alidai baada ya kuwapekua hakuwakuta nazo na kuwaamuru kwenda nao kituo cha polisi Mwanakwerekwe kwa mahojiano zaidi.

Alisema mara baada ya mahojiano, ofisa huyo aliwaamuru vijana hao wampatie Sh. laki mbili ili awaachie na chombo chao, vijana hao walimpatia shilingi laki moja na baadae kuwachiwa wao na kuendelea kukushikilia chombo chao.

Kwa mujibu wa sheria namba moja ya mwaka 2012 ya kuzuiya rushwa na uhujumu uchumi afande huyo atakuwa amefanya kosa la kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu hicho cha sheria.

Alisema uchunguzi wa jalada hilo utakapokamilika litapelekwa kwa Mkurugenzi wa mashtaka kwa hatua za kisheria.

Kamanda wa Polisi Zanzibar, Muhammed Haji Hassan, alisema jeshi hilo halitamvumilia askari wake yeyote atakaebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Alisema jeshi la polisi linafanya kazi kwa mujibu wa kanuni na sheria zao hivyo wanapotokea wachache wenye dhamira ya kutaka kulichafua jeshi hilo ikiwamo kuomba rushwa hawatavumiliwa.

Aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa jeshi hilo au mamlaka husika iwapo watagundua askari yeyote anajihusisha na rushwa kwa lengo la kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alisema tabia ya baadhi ya wananchi kukubali kutoa rushwa ni miongoni mwa vishawishi ambavo wakati mwingine huchangia kutendeka kitendo alichokiita adui wa haki.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: