Mapadri watatu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Same, wamefariki dunia ndani ya saa 72. Kanisa limesema vifo vya aina hiyo havijawahi kutokea.

Waliofariki wametajwa kuwa ni Padre Ubaldus Kidavuri, Padre Arbogast Mndeme na Michael Kiraghenja, wote wa jimbo hilo. Wawili kati ya hao walifariki ghafla usingizini.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kanisa hilo, padre mmoja ndiye aliyekuwa akiumwa na alifariki akiwa katika Hospitali ya KCMC.

Taarifa ya vifo vyao ilitolewa jana na Askofu wa Jimbo la Same, Mhashamu Rogath Kimario.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mapadri hao wanatarajiwa kuzikwa Aprili 17, katika Makaburi ya Mapadri Jimbo la Same.

Taarifa ilisema haijawahi kutokea vifo vitatu vilivyopishana kwa saa 24 katika jimbo moja. 

“Jana nilionana na Padri Kidavuri na alikuwa akijiandaa kwa safari ya kwenda kuzika wenzie na nikampa pole pale St. Joseph, alikuwa mzima wa afya. Wapumzike kwa amani, amina,” alisema Padre Kimario.

Akithibitisha vifo hivyo jana, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Raymond Saba, alisema kanisa limepokea kwa mshtuko mkubwa kufuatia vifo hivyo vya ghafla.

“Vifo vimetushtua sana maana vimekuwa vya ghafla mno, tulikuwa nao na walikuwa wazima kabisa,” alisema Padre Saba.

Alisema wanatarajia mazishi yatafanyika Jumanne ijayo, Same.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: