Monday, 2 April 2018

Idadi ya Vifo vya wajawazito vyaongezeka


IDADI ya vifo vya wajawazito imeongezeka kutoka 454 hadi 556 kwa kila vizazi 1,000, ukiwa ni wastani wa wanawake 30 ambao hufariki dunia hapa nchini.

Idadi hiyo ilibainika katikati ya wiki iliyopita wakati Shirika la Kimataifa linalojishughurisha na idadi ya watu duniani (UNFPA), lilipotoa semina  kwa waandishi wa habari kuhusu masuala ya uuguzi na ukunga.

Semina hiyo ilikuwa maandalizi ya kuelekea kongamano la kisayansi la wakunga na wauguzi litakalofayika mwezi huu mkoani Dodoma.

Semina hiyo iliwaasa waandishi kufanya tafiti kabla ya kurusha taarifa mbaya za wauguzi, hali ambayo imekuwa ikisababisha wavunjike moyo wa kufanya kazi zao za kila siku.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wakunga, Sebalda Leshabari alisema moja ya sababu ya kuongezeka kwa vifo hivyo ni idadi kubwa ya wanawake kujifungulia nyumbani na kusaidiwa na wakunga wasio na sifa.

Alitaja sababu nyingine kuwa ni kushindwa kuhudhuria kliniki kwa sababu mbalimbali na kuwa utafiti unaonyesha idadi ya wajawazito wanaohudhuria kliniki kwa mara ya kwanza ni asilimia 98 lakini idadi hiyo hushuka kadri siku zinavyokwenda.

Akizungumza katika warsha hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma ya Uuguzi na Ukunga, Gustuv Moyo alitaka waandishi wa habari kuandika habari za wakunga na wauguzi kwa weledi ili kuondoa dhana mbaya iliyojengeka katika jamii.

Alisema wauguzi wanafanya kazi katika mazingira magumu kutokana na upungufu wa vifaa na vitendea kazi kwa ujumla, ingawa siyo sababu ya kufanya kazi bila kufuata maadili.

Moyo alisema kuna upungufu mkubwa wa watumishi wakunga ingawa serikali iko mbioni kuajiri baada ya kuwepo kwa idadi kubwa ya wahitimu wa fani hiyo.

Pia alisema serikali imesema itaongeza bajeti ya dawa mara 10 ya ile ya kwanza, na pia imetoa pesa za ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vituo vya afya nchini kote.

"Uuguzi ni kazi ngumu, wauguzi wanakesha usiku mchana pamoja na uchache wao pamoja na upungufu wa vitendea kazi na madawa... wanajitahidi kuhakikisha wanatoa huduma stahiki za afya," alisema.

Msajili wa Baraza la Wakunga, Lena Mfalila alisema wako katika harakati za kuhakikisha vifaa maalumu vya kusaidia wauguzi ili waepukane na tatizo hilo vinaletwa hapa nchini.

Mfalila aliwataka wanawake kujifungulia hosptali kwani ndiko mahali salama kwa kujifungulia na kuwa hali hiyo itapunguza vifo vya wanawake wanaofariki wakati wa kujifungua.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: