Thursday, 5 April 2018

CCM KARATU YATOA SIKU 14 KITUO CHA AFYA KISICHOKUA NA CHOO


Na Ferdinand Shayo,Arusha.

Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Karatu imetoa siku 14 kwa Wilaya na Uongozi wa kituo cha Afya cha Oldeani kuhakikisha kuwa wanajenga vyoo vya nje katika kituo hicho ambacho hakina vyoo vya nje kwa ajili ya wagonjwa wanaofika na kupatiwa matibabu kituoni hapo.

Kufuatia ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya Chama katika shule za serikali na vituo vya afya ,jumuia hiyo imebaini kuwa kituo hicho hakina choo jambo ambalo linaweza kuhatarisha afya za wananchi.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa kituo Henry Ernest hicho amesema kuwa licha ya changamoto ya ukosefu wa vyoo bado wanakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa mashuka,magodoro na uchakavu wa wodi za kinamama wajawazito hivyo wameiomba serikali iwasaidie ili kutatua changamoto hizo.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Karatu Luciani Akonay  ameagiza Serikali ya Wilaya kutatua changamoto hizo na kuhakikisha kuwa wanajenga vyoo hivyo ndani siku 14 ili kuhakikisha kuwa wananchi wanahudumiwa vizuri na amesema kuwa jumuiya hiyo itashiriki vyema kuhakikisha kuwa choo hicho kinajengwa.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Karatu Peter Mmasy na na katibu wa  jumuiya  hiyo  Deogratias Nakey  pamoja amesema kuwa jukumu la jumuiya hiyo ni kuhakikisha kuwa malezi ya watoto katika sekta ya elimu na sekta ya afya ili kuwa na taifa bora lenye maendeleo hivyo ni vyema Viongozi wa serikali wakawajibika kwa kutatua changamoto za afya na elimu.

Mkazi wa kata hiyo Gerald Guaha amesema kuwa licha ya hospitali hiyo kupewa hadhi ya kituo cha afya bado kituo hicho kina ubovu wa miundombinu jambo linalozorotesha huduma za afya Hivyo ameiomba serikali kuikumbuka hospitali hiyo.

Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Karatu pia wametoa msaada wa vifaa vya kufanyia usafi ,wamepanda  miti 3000 katika shule za msingi na sekondari ,Oldeani Sekondari,Shule ya Msingi Oldeani  na shule ya msingi Meali.

No comments:

Post a comment