Serikali imesema wanafunzi wa vyuo vikuu wanaongoza  kutukana na kutumia lugha zisizo na maadili kwenye mitandao ya kijamii.

Angalizo hilo limetolewa na naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha  Jumamosi Machi 24, 2018 katika hafla fupi ya uzinduzi wa Unilife Compus iliyopo Mkoa wa Kilimanjaro uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Mwenge na kuvikutanisha vyuo vikuu vyote vya mkoa huo.

Alisema  yapo mambo matatu ambayo yanachangia wanafunzi kutofanya vizuri, yakiwamo matumizi mabaya ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), anasa na starehe zilizopitiliza na kujiingiza kwenye siasa ambazo zinawanyima fursa ya kusoma vizuri.

“Serikali imebaini mambo yanayochangia kufifisha na kudidimiza jitihada za elimu tunayoitoa kuonekana bure. Kuna vitu ambavyo siyo vizuri  vinaendelea katika vyuo vyetu, ndizo changamoto tunatakiwa kukabiliana nazo. Chuoni unaweza kutengeneza au kuharibu maisha yako,” alisema.

Naye mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira alisema  wanafunzi wengi hawataki kujifunza  kwa kutumia muda vizuri kwa kusoma vitabu.

"Tunabaki kuwa waigaji wa dhana za wenzetu wa magharibi, hatutaki kujifunza vitu vipya bali vilevile vya wenzetu vinatumika hadi leo. Wasomi wa Tanzania tunajishusha kwa sababu ya kushindwa kuleta mawazo mapya kwenye sekta ya elimu na afya," alisema  Mghwira.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: