Jeshi la Polisi mkoani Rukwa linawashikilia watu sita akiwemo mjukuu anayedaiwa kuchukua milioni moja na kukubali babu yake auawe kwa kupigwa rungu katika ugomvi wa Ardhi. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando, alisema Jana kuwa tukio la kuuawa kwa mzee huyo, Paul Kisiwa (72), mkazi wa Kijiji cha Ng’ongo lilitokea jioni Machi 3, mwaka huu kwenye Kijiji cha Kifinga Kata ya Mtowisa Wilaya ya Sumbawanga.

Imeelezwa kuwa Mzee Kisiwa pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya kata.

Taarifa kutoka eneo la tukio zilizothibitishwa na Diwani wa Kata ya Mtowisa, Edgar Malinyi, zilieleza baada ya kuuawa kwa mzee huyo alizikwa kinyemela shambani kwake.

Habari zinasema kuwa taarifa za kupotea kwa mzee huyo zilianza kuzagaa ndipo ndugu wa marehemu pamoja na majirani wakishirikiana na polisi walianza kuchunguza tukio hilo, na ilipofika Machi 8 mwaka huu, watu hao walimbana mjukuu wa mzee huyo, John Kisiwa (22), ambaye alikiri kushiriki kupanga njama za kumuua babu yake kwa ujira wa Sh. 1,000,000.

Diwani huyo, alisema kijana huyo anadaiwa kupanga njama ya mauaji hayo na wenzake ambao walikuwa katika mgogoro wa ardhi wa muda mrefu na babu yake ambaye awali aliwakodisha watu hao shamba la ekari zaidi 15 kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Alisema baadaye aliwanyang’anya shamba hilo na kuamua kulilima mwenyewe, kitendo kilichowaudhi watuhumiwa hao na wakiingia katika mgogoro wa kugombea eneo hilo.

Alidai kuwa kutokana na mgogoro huo, waliandaa mipango ya kumuua mzee huyo.Inadaiwa kuwa siku ya tukio la mauaji hayo, watu hao walimvamia mzee huyo akiwa katika shamba hilo kisha kumpiga na rungu kichwani ambapo alianguka na kufariki dunia papo hapo.

Diwani Malinyi alisema baada ya kumuua mzee huyo walichimba shimo shambani humo na kumfukia ili kupoteza ushahidi, lakini baada ya mjukuu wake kubanwa, alieleza ukweli, hivyo polisi walifukua eneo hilo na kukuta mwili wa mwenyekiti huyo.

Kamanda Kyando aliwataja watuhumiwa wengine waliokamatwa ni Kela Lubinza (15), Chani Lubinza (29), Simba Lubinza (16) wote wakiwa ni ndugu wa familia moja.

Wamo pia Deshi Mihambo (40) na Muli Sabini (21), ambao ni majirani wa wanafamilia hao.Alisema watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa, baada ya uchunguzi wa awali kukamilika.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: