Friday, 23 February 2018

Ulinzi na Usalama waimarishwa Kijiji atakachozikwa Akwilina


Vyombo vya ulinzi na usalama vimeimarisha usalama katika eneo atakalozikwa mwanafunzi wa chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline katika kijiji cha Olele wilayani Rombo.

Uchunguzi uliofanywa na MCL Digital saa 2:00 hadi saa 4:30 asubuhi leo Ijumaa Februari 23, 2018 umebaini uwapo wa askari wengi wakiwamo wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na askari kanzu.

Mbali na askari kanzu, wameonekana maofisa usalama wa Taifa na polisi waliovalia kiraia, wakiwa wameegesha magari kimkakati, mita kati ya 100 hadi 150 kutoka nyumbani kwa wazazi wa marehemu.

Ofisa mnadhimu wa polisi namba moja wa Mkoa Kilimanjaro, Koka Moita, ambaye amezoeleka kuwa katika sare, leo ameonekana akitembea kwa miguu mitaani akiwa amevalia kiraia.

Moita alipoulizwa kuhusu usalama, alikiri kuna ulinzi wa kutosha japo amesema anayeweza kuzungumzia hilo ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah.

Mbali na polisi, lakini wapo mgambo ambao wameshika doria maeneo ya maegesho ya magari ya wageni mbalimbali na eneo la kanisa itakapofanyika ibada.

Askari wa usalama barabarani, nao wameonekana barabara kuu ya Olele-Useri, wakisimamia usalama wa watembea kwa miguu na watumiaji wengine wa barabara, jirani na shughuli za mazishi zitakapofanyika.

No comments:

Post a comment