Rufani ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) imeahirishwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, baada ya Kaimu Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Sekela Mosha, kutokuwapo mahakamani hapo.

Katika kesi ya msingi, Lema alimkataa Hakimu Desderi Kamugisha, akisema hawezi kutenda haki katika kesi yake ya madai ya kumtukana Rais John Magufuli.

Alidai hakimu huyo aliwahi kumnyima dhamana hali ambayo ilimfanya asote mahabusu miezi zaidi ya  minne.

Akiahirisha rufani hiyo jana, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Angelo Rumisha, alisema itasikilizwa Juni 15, mwaka huu, saa 3:00 asubuhi mbele ya Jaji Mosha.

Katika rufani hiyo, Lema aliwasilisha hoja zake zikiwamo za kumkataa Hakimu Kamugisha kuendelea na kesi yake ya uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli kwa madai ya kuwa na upendeleo.

Hoja nyingine ni kuwa taarifa ya kukata rufani haianzishi kukata rufani kutokana na hakimu huyo kukataa kujitoa katika kesi yake, baada ya kumkataa.Katika rufani hiyo, Lema anatetewa na Wakili John Mallya.

Awali katika kesi hiyo, Oktoba 9, mwaka jana, Wakili Sheck Mfinanga, alijitoa kuendelea kumtetea Lema kwa kile alichodai kuomba mwenendo wa kesi zaidi ya mara tatu mahakamani hapo na kushindwa kupewa, ili aweze kukata rufani Mahakama Kuu, lakini Hakimu Kamugisha aligoma kutoa.

Wakili Mfinanga alimtaka Hakimu Kamugisha kujitoa kusikiliza kesi ya uchochezi inayomkabili Lema, licha ya mbunge huyo kumtaka afanye hivyo kwa kile alichodai aliwahi kufanya uamuzi wa hila na kusababisha kusota mahabusu zaidi ya miezi minne.

Hata hivyo, hakimu huyo aliamua kuendelea na shauri hilo, hata pale mawakili wa Lema walipowasilisha kwa mdomo kusudio la kukata rufani Mahakama Kuu kwa lengo la kupinga uamuzi huo wa kuendelea kusikiliza kesi hiyo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: