MSTAHIKI Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita leo amekutana na kufanya mazungumzo na Meya wa Jiji la Blantyre  Nchini Malawi Wild Ndipo ambapo pamoja na mambo mengine wamejadiliana namna watakavyoweza kubadilisha uzoefu katika kuendesha majiji.

Aidha ugeni huo wa  Meya wa Jiji la  Blantyre ulihusisha madiwani watatu, Balozi mdogo wa Maalawi Sai Kaphale ambapo wote walipata  fursa ya kutembelea mradi wa mabasi yaendayo haraka(UDART).

Akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kufanya mazungumzo hayo, Meya Mwita amesema lengo la ugeni huo ni kuendeleza urafiki ambao utawezesha kubadilishana ujuzi kwenye  uendeshaji wa majiji hususani kwenye miundombinu  ya Elimu, barabara ,Utalii na huduma nyingine za kijamii.

Amesema kuwa wakiwa jijini hapa watajifunza namna ya kuendesha miundombinu hiyo hususani ya Barabara na Elimu ambapo kwa Jiji la Dar es Salaam limepata mafanikio makubwa kwenye utoaji wa huduma hizo.

Ameongeza kuwa mbali na miundombinu  hiyo,  lakini  watapa fursa ya kujifunza namna ya ukusanyaji kodi na kuongeza mapato kwenye jiji ambapo kesho watashiriki kwenye baraza la Bajeti  litakalokaa siku mbili.

Kwaupande wake Meya wa Jiji la Blantyre Wild Ndipo amefurahia mapokezi waliyopata kutoka kwa Meya Mwita na kuahidi kushirikiana na jiji la Dar es Salaam katika masuala mbalimbali ya maendeleo.

Mwisho.

Imetolewa leo Februali 22 na Christina Mwagala

Afisa Habari ofisi ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: