UBALOZI wa Marekani jijini Dar es salaam umetaka kufanyika kwa uchunguzi ulio wazi wa tuhuma za kutekwa na kisha kuuawa kwa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Daniel John mwishoni mwa wiki iliyopita.

Taarifa iliyotolewa na ubalozi huo kwa vyombo vya habari jana ilisema Marekani inaungana na Watanzania kutaka kuwapo kwa uchunguzi ulio wazi ili kuwawajibisha wote waliohusika kwa mujibu wa sheria za nchi.

Mbali na kuuawa kwa John, watu wanaodaiwa kufanya uhalifu huo walimjeruhi Reginald Mallya.

“Pia tunaungana na Watanzania kutaka kufanyika kwa uchunguzi wa uwazi ili kuhakikisha wahusika wote wa tukio hilo wanatiwa nguvuni na kushtakiwa kwa mujibu wa Sheria za Tanzania,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilisema Marekani imesikitishwa mno na kuhuzunishwa na matukio ya utekaji na vurugu vilivyosababisha mauaji ya John na kujeruhiwa kwa Mallya.

“Tunatuma salamu za pole nyingi kwa familia zao na marafiki,” taarifa hiyo ilisema zaidi.

“Kuongezeka kwa vurugu na mapigano vyenye uhusiano na siasa kunatupa wasiwasi, na tunaviomba vyama vyote kulinda amani na utulivu kwa manufaa ya mchakato wa kidemokrasia, nchi, na watu wa Tanzania.”

Mwili wa John uliokotwa maeneo ya ufukwe wa Coco wa Bahari ya Hindi wilayani Kinondoni Jumapili iliyopita ukiwa na majeraha kichwani na shingoni, baada ya kudaiwa kutekwa na watu wasiojulikana.

Jumanne Mbowe aliviambia vyombo vya habari kuwa John aliyekuwa Katibu wa Chadema wa kata ya Hananasif, Kinondoni mkoani Dar es Salaam alitekwa na watu wasiojulikana akiwa na mwenzake Jumapili.

Aidha, juzi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Jumanne Muliro, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa wanaendelea kuchunguza sababu ya mauaji hayo na pia watachunguza kauli ya Mbowe.

“Moja ya kazi ya Jeshi la Polisi ni kuchunguza jambo," alisema Kamanda Murilo na kwamba “pamoja na hilo (la mauaji) tutachunguza kauli ya Mbowe kulituhumu Jeshi la Polisi.

“Tutachunguza anasema hivyo kwa kuzingatia misingi ipi na amesukumwa na nini mpaka kusema hayo anayoyasema.

“Hatuwezi tukaacha mtu akajisemea vitu kwa kusukumwa na hisia zake. Ndiyo maana sisi jambo linapotokea moja ya kazi yetu ni kuchunguza na hatusukumwi na hisia za mtu kwa sababu yeye hajasomea kazi ya Jeshi la Polisi."

Aidha, Kamanda Murilo alisema wanachukua maelezo na taarifa ya Mbowe kama ya mwananchi wa kawaida na kuifanyia kazi na endapo italazimu kuhojiwa ataitwa.

"Sisi hatuwezi kusukumwa na kauli yake tukatoka kwenye misingi ya upelelezi kwa kuburuzwa na hisia zake halafu baadaye tukosee ili haki isitendeke," alisema Kamanda Murilo.

Alisema polisi watafanyakazi zao kwa kufuata weledi na wahalifu wakibainika huwa wanafikishwa kwenye vyombo vya dola na si kwenye vyombo vya habari.

Lakini sasa Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam umetaka kufanyika kwa uchunguzi ulio wazi.

Kuhusu tarifa za tukio hilo, Kamanda Muliro alisema Jumatatu walipata taarifa kutoka kwa msamaria mwema ya kuwapo kwa maiti na walipofika ufukwe wa Coco walikuta mwili wa kijana anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 30-35 ukiwa na majeraha maeneo ya kichwani, usoni, mkononi na miguuni.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: