Baba mzazi wa ‘Akwilina’ amlilia polisi aliyemuua mwanaye ‘nitapambana naye hata kumuua kwa meno’


Mzee Akwilini Shirima (Picha na Mwananchi)
Kwa mara ya kwanza Baba mzazi wa mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini ambaye ameuawa na askari polisi kwa kupigwa risasi siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita, Mzee Akwilini Shirima ameongea na kueleza hisia zake kwa askari aliyetekeleza mauaji ya mwanaye akidai kuwa endapo akikutana naye atapambana naye hadi kifo.
Mzee Shirima amesema endapo muuaji atakuwa ni kijana mwenye nguvu kumzidi yeye, atapambana naye hata kwa kumuuma kwa meno ili mradi tu afanikiwe kumtoa uhai.
Najua ni ngumu kukutana na aliyempiga mwanangu risasi, lakini laiti ningekutana naye kama ni kijana mwenye nguvu kunizidi nitapambana naye hata kumuuma kwa meno.. Kama ni mzee mwenzangu nitapambana naye hadi kifo ila kwa bahati mbaya siwezi kumpata, hivyo sina namna,“amesema Mzee Shirima kwenye mahojiano yake na Gazeti la Mwananchi.
Kwa upande mwingine Mzee Shirima amesema kuwa kifo cha mwanaye kimezima ndoto ya familia yake kuondokana na umasikini huku akiiomba serikali kuliangalia suala hilo kwa kina na kuona namna ya kumsaidia kwa kuwa tegemeo lake limeondoka .
Jamani hii ni taa yangu imezimika na kuniacha gizani kwani toka nimepata taarifa za kifo chake sijaweza kula chochote. Nimekuwa kama nguruwe aliyetelekezwa porini bila msaada,“ameliambia gazeti hilo huku qkieleza jinsi alivyopokea taarifa hizo mbaya zaidi kwenye familia yake.
Nilipopata taarifa za kifo cha mwanangu nilishtuka sana na kuhoji ni mwizi au nini kimetokea, lakini baadaye nikaambiwa ni Serikali imefanya mambo hayo. Imenitia uchungu sana na siwezi hata kula,“amesema Mzee Shirima.
Akwilina alifariki dunia Februari 16, 2018 baada ya kupigwa risasi kichwani akiwa kwenye daladala wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji ambao ni wafuasi wa Chadema.
Soma ripoti ya uchunguzi iliyotolewa na Madaktari kuhusu kifo cha mwanafunzi huyo HAPA
Previous Post
Next Post

post written by:

0 komentar: