Articles by "WIZARA YA ELIMU"
Showing posts with label WIZARA YA ELIMU. Show all posts

 


Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Haruni  Mapesa amewataka viongozi wapya wa Serikali ya Wanafunzi (MASO) kutambua kuwa Uongozi ni utumishi wa kuwatumikia watu na si kutumikiwa, kwani kazi ya kiongozi ni kuwa tayari muda wote kutatua changamoto mbalimbali.

Mapesa ameyasema hayo wakati wa hafla fupi ya kuwapisha viongozi wapya wa Serikali ya Wanafunzi (MASO) kwa mwaka 2026/27 pamoja na mambo mengine amepongeza Uongozi wa Serikali  iliyomaliza muda wake iliyokuwa ikiongozwa na Magashi Magina  kuwa walizingatia Weledi wa hali ya Juu.

Mkuu huyo wa Taasisi ameitaka Serikali mpya kuzingatia misingi ya Uongozi, na kuwa na namna bora ya kutatua changamoto ikiwa ni pamoja na kushirikiana vyema na Serikali ya Wanafunzi ambayo imemaliza muda wake, huku akiwaahidi ushirikiano wa dhati kutoka kwa Uongozi wa Chuo.

Kwa upande wake, Rais aliyemaliza muda wake Magashi Magina ameishukuru Menejimenti ya chuo kwa ushirikiano alioupata katika kipindi chote cha uongozi wake, ameeleza kuwa mafanikio yote yaliyopatikana yalitokana na uwazi na utayari wa Menejimenti kusikiliza na kutatua Changamoto mbalimbali za Wanafunzi jambo lililorahisisha utendaji kazi wa serikali yake.

Nao, Viongozi wapya walioapishwa kuiongoza Serikali ya Wanafunzi , Rais ni Samir Naseer na Makamu wa Rais  Julieth Mandia  wametoa shukrani za dhati kwa Wanafunzi wote kwa kuonyesha imani kwao na kuwachagua kuongoza Serikali ya wanafunzi ambapo wameahidi kuongozi kwa Uadilifu, Amani, mshikamano kwa  kushirikiana na Menejimenti ya Chuo pamoja na Serikali ya Wanafunzi iliyomaliza muda wake.

 

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano na Masoko

CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE

28.05.2026

 


Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Haruni Mapesa amewataka Wafanyakazi wa MNMA kuendelea kufanya kazi kwa furaha, Uadilif na kuweka maslahi ya Taasisi mbele kwa kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa Wanafunzi na Watumishi kwa moyo na kufanya hivyo ni utumishi kama ilivyo utumishi wa Mungu, kwani kila kazi unayoifanya kwa ajili ya watu basi hiyo ni kazi ya Mungu.

Prof.Mapesa ameyasema hayo leo wakati wa kuwapongeza Watumishi hodari katika uwajibikaji wa utumishi wa umma kwa mwaka 2025/2026 kwa wale wote waliopata fursa ya kuwa Wafanyakazi bora, na kusisisitiza kuwa Watumishi waendelee kufanya kazi kwa kuzingatia Misingi ya utumishi wa umma na huo ndiyo uwe utamaduni wa kila siku.

Kwa upande wake Naibu Mkuu wa Chuo anaesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaaluma Prof. Richard Kangalawe amesema Ushindi ni heshima huku akiwataka watumishi wengine kuendeela kuwajibika katika nafasi zao kwa lengo la kutimiza malengo ya Taasisi.



Naye Naibu Mkuu wa Chuo anaesimamia Mipango, Fedha na Utawala Prof.Evaristo Haulle alisema mchakato wa kupata Mfanyakazi bora ulikuwa ni wa huru na haki ambapo vigezo mbalimbali vilizingatiwa ikiwemo Nidhamu ya mtumishi , Utendaji kazi wa mtumishi,(PEPMIS) na Mienendo mbalimbali, hivyo dosari zote zilizojitokeza zilishughulikiwa ipasavyo.

Nao viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Debora Donati wa THTU na kwa upande wa  RAAWU  Hashimu Mtongola  kwa pamoja wameipongeza Menejimenti kwa hafla hiyo fupi ambayo inatoa motisha na kuongeza morali ya kazi kwa Wafanyakazi na pia wameomba uongozi ufikirie kujumuisha Wafanyakazi wote kwa hafla ya namna hiyo wakati mwingine.



Wafanyakazi bora wa Taasisi kwa mwaka huu Filbert Nyakasi upande wa Wanataaluma  na Amedeus Mchau upande wa Waendeshaji wameshukuru uongozi kwa kutambua jitihada zao na mchango wao katika kutimiza majukumu ya kila siku na wameahidi kuendelea kufanya kazi kwa Uadilifu, Nidhamu kwa  kushirikiana na Wafanyakazi wengine.


Wafanyakazi wote hodari wamentunukiwa vyeti vya kutambuliwa na zawadi ya fedha, ambapo zoezi limejumuisha Wafanyakazi wote bora wa Kampasi ya Kivukoni, Karume na Pemba.


Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano na Masoko

ChUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE

25.05.2026

 


Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Prof. Haruni Mapesa amewataka wanataaluma kuacha tabia ya kuchapisha makala zao kwenye Majarida yasiyotambulika ili kuzuia upotezaji wa nguvu na rasilimali za uchapishaji wa Tafiti.

Prof. Mapesa ameyasema hayo wakati akifungua Semina ya Uwasilishaji wa Makala Mijadala za a Kitaaluma iliyoandaliwa na Idara ya Lugha na Fasihii Chuoni hapo hafla iliyofanyika katika Kampasi ya Kivukoni jijini Dar es salaam.

Mkuu huyo wa Chuo amesema kuwa sasa Tasisi ipo katika hatua za ukuaji ikiwemo kuidhinishwa kwa Kitivo cha Uchumi na Biashara, ambapo chuo kimetenga kiasi cha shilingi milioni 120 kwa ajili ya tafiti na kuna mpango wa kuongeza fedha hizo ili kuwekeza zaidi kwa wahadhiri watakaofanya tafiti mbalimbali.

Naibu Mkuu wa Chuo anayesimamia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaaluma Prof. Richard Kangalawe amekipongeza Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii kupitia Idara ya Lugha na Fasihi kwa kuandaa semina hiyo na kuwahimiza washiriki kutumia fursa hiyo kuimarisha mawazo ya kitafiti, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha tafiti zote zinasajiliwa rasmi na machapisho yawe yenye ubora wa hali. 

Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala Prof. Evaristo Haulle amewataka Wanataaluma kubadilika na kuanza kufikiria namna ya kuchangia asilimia 30 ya mapato ya ndani kupitia Tafiti na Miradi wanayoifanya badala ya kutegemea rasilimali na fedha za ndani za chuo pekee.

Akiwasilisha taarifa ya Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii, Mtiva wa Kitivo hicho Dkt. Luzabeth Kitali ameishukuru Menejimenti ya Chuo kwa Maelekezo na Ushauri na kuahidi kuwa idara yake imejipanga kikamilifu kusimamia ubora wa Tafiti, kuendeleza Uandishi ikiwa ni pamoja na kushiriki katika makongamano ya kitaaluma.


 

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano na Masoko

CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE

21.05.2026

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imegawa vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) vyenye thamani ya jumla ya Shilingi milioni 769 kwa shule za msingi na sekondari 19 zilizopo katika mikoa tisa nchini, ikiwemo Kusini Unguja (Zanzibar), Dodoma, Iringa, Ruvuma, Arusha, Geita, Kilimanjaro, Mbeya na Mtwara.


Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa vifaa hivyo iliyofanyika jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, alisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuendelea kuimarisha sekta ya elimu kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia za kisasa.


Alisema matumizi ya vifaa hivyo yataongeza uelewa kwa wanafunzi kwa kuwapa fursa ya kujifunza kwa vitendo na kuona, hasa katika masomo ya sayansi na teknolojia. Aidha, alieleza kuwa walimu watanufaika kwa kutumia mbinu bunifu za ufundishaji, kuandaa maudhui kwa ufanisi na kufuatilia maendeleo ya wanafunzi kwa urahisi kupitia mifumo ya kidijitali.


“Serikali inaendelea kutekeleza mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kama yalivyoainishwa katika Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023) pamoja na mitaala iliyoboreshwa, kwa lengo la kuboresha ubora wa elimu na kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye,” alisema Ameir.


Alitaja baadhi ya hatua zinazoendelea kuchukuliwa kuwa ni pamoja na utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka 10, kuanzishwa kwa mkondo wa elimu ya amali unaolenga kuwapatia wanafunzi stadi za ufundi na ujasiriamali, pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali katika ufundishaji, ujifunzaji na usimamizi wa elimu.


Aidha, aliongeza kuwa Serikali imeandaa na kuanza kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika Elimu, sambamba na miongozo mbalimbali ikiwemo mwongozo wa matumizi ya TEHAMA katika shule na vyuo vya ualimu pamoja na mwongozo wa matumizi ya Akili Unde (AI) katika elimu.


Kwa upande mwingine, alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imeanzisha madarasa janja matano na kufunga mbao janja 422 katika shule za sekondari, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya ujifunzaji nchini.


Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Caroline Nombo, alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuboresha elimu kwa kuzingatia mahitaji ya karne ya 21, hususan kwa kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali.


Alisema ugawaji wa vifaa hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya elimu pamoja na mkakati wa TEHAMA katika sekta hiyo, na ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha walimu na wanafunzi wanapata nyenzo bora za kufundishia na kujifunzia.


Profesa Nombo alisisitiza kuwa vifaa hivyo vitachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha ubora wa elimu, kuongeza ufanisi wa ufundishaji na ujifunzaji, pamoja na kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi wa kidijitali unaohitajika katika dunia ya sasa.








 


Hatua ya Mageuzi ya Elimu Tanzania imeendelea kuwa kuvutia nchi mbalimbali za Afrika kujifunza ikiwemo uboreshaji Sera na mabadiliko ya Mtaala  katika ngazi mbalimbali  za elimu.

Juali 18, Viongozi kutoka Wizara ya Elimu  Sudan Kusini wakiongozwa hiyo.Mhe. Kacuol Mabil Piok wamekutana na Menejimenti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Kibaha Mkoani Pwani chini ya Katibu Mkuu Prof Carolyne Nombo wakiwa katika ziara maalum ya kujifunza utekelezaji mageuzi ya kielimu.

Sudan Kusini imevutiwa na jinsi Tanzania inavyotekeleza  afua mbali za kielimu ikiwemo uwekezaji rasimali katika sekta kwa ujumla na miradi ya elimu ikiwemo utekelezaji mpango wa elimu nje ya mfumo rasmi ambapo Mhe Piok amesema wamevutiwa sana na maendeleo na Elimu Tanzania na hivyo kuamua kuja kujifunza na kuanzisha ushirikiano ili kuendelea kubadilishana uzoefu kama Nchi za Afrika Mashariki.

Akizungumza katika mkutano huo Katibu Mkuu Prof Nombo amewashukuru kwa kutambua Maendeleo ya Elimu Tanzania na kuamua kuja kujifunza, aidha ameongeza kuwa  Wizara ya Elimu inaendelea kupokea nchi mbalimbali kuja kujifunza mageuzi ya elimu ambayo yanalenga kuandaa wahitmu wenye maarifa na ujuzi.



 WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa Serikali itaendelea kuwapa kipaumbele walimu nchini kutokana na nafasi yao muhimu katika maendeleo ya taifa na jamii kwa ujumla.


Prof. Mkenda alitoa kauli hiyo jana usiku wakati wa hafla ya utoaji wa zawadi kwa washindi wa shindano la tatu la stadi za ufundishaji kwa elimu ya msingi na shindano la kwanza kwa walimu wa elimu ya sekondari.

Amesema kuwa Serikali inapanga kuingiza bajeti ya shindano hilo katika mwaka wa fedha 2025/2026, kwa kuwa linaongeza hamasa na motisha kwa walimu wanaofundisha wanafunzi katika ngazi mbalimbali.

"Walimu ndio nguzo ya msingi ya elimu. Serikali itaendelea kuweka mkazo katika kuwawezesha na kuwathamini, kwa sababu wao ndio wanaowatengeneza wataalamu wa kesho," alisema Prof. Mkenda.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, alisema kuwa shindano la mwaka huu limehusisha walimu wa sayansi kwa kidato cha kwanza kwa upande wa sekondari, huku likiwa ni mara ya tatu kufanyika kwa elimu ya msingi.

Ameeleza kuwa shindano hilo ni sehemu ya utekelezaji wa maboresho ya mtaala wa mwaka 2023, na linaongeza ujuzi wa walimu hasa katika matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), jambo ambalo ni muhimu kwa wanafunzi wa karne ya sasa.

Hata hivyo, Dkt. Komba alitaja changamoto ya baadhi ya walimu kurekodi maudhui yasiyofaa, akibainisha kuwa hilo ni eneo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi ili kuboresha mashindano yajayo.

Akizungumza katika hafla hiyo, mwakilishi mkazi wa Benki ya Dunia, Gema John, ambaye ni mmoja wa wadhamini wakuu wa mashindano hayo, alisema benki hiyo imekuwa ikiwekeza katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu ya awali na sekondari.

"Tumeamua kushirikiana na TET kuwekeza kwa walimu kwa sababu tunaamini walimu bora ndio msingi wa elimu bora. Na mwaka huu tumeongeza ushiriki kwa walimu wa sekondari," alisema Gema.
















 


Naibu Waziri Ofisi ya Rais - TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba amewataka walimu wote nchini kuhakikisha wanatumia taaluma na weledi wao katika kufundisha na kuleta mapinduzi ya kimaendeleo na fikra kwa jamii ya watanzania.

Mhe. Katimba ametoa maelekezo hayo leo Juni 05,2025 Jijini Arusha kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mhe. Mohamed Chengerwa wakati akizindua zoezi la ugawaji wa vifaa vya TEHAMA katika shule za Sekondari nchini kupitia Programu ya Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP).

“Niwaase walimu muendelee kufanya kazi kwa bidii, kuendana na mabadiliko ya Kisera yanayoendelea kufanyika katika siku za karibuni ikiwemo kutekeleza vema mtaala ulioboreshwa, ni muhimu kujituma na kuhakikisha tafsiri ya mitaala na sera ya elimu inafanyika kwa vitendo.” Amesema Katimba.

Katika kusisitiza hilo Mhe. Katimba amesema jamii ya kitanzania inamtazama mwalimu katika hatua zote za mabadiliko ya mwanafunzi hasa katika ulimwengu wa TEHAMA ambao kwa sasa unashika kasi ulimwenguni. 

Aidha, ameongeza kuwa Ofisi ya Rais - TAMISEMI itaendelea kushirikiana na Wizara za kisekta na Wizara Mtambuka ili haki na maslahi ya walimu yapatikane, kulindwa na kuhakikisha wanafanya kazi katika mazingira tulivu yaliyoboreshwa na kupata huduma kwa upendo.

Kwa upande wake Joseph Mkude, Mkuu wa wilaya ya Arusha akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha amesema matumizi ya TEHAMA kwa wanafunzi yatakwenda kuongeza uelewa na ufaulu kwa wanafunzi.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Dkt. Selemani Shindika amesema vifaa hivyo vinavyogawiwa vinagarimu kiasi cha shilingi bilioni 12 na vitagawiwa kwa shule 422 za Sekondari ili kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji kwa njia ya kisasa kwa kutumia TEHAMA ili kuendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia Duniani.