Articles by "UMMYMWALIMU"
Showing posts with label UMMYMWALIMU. Show all posts

 Na: Dk. Reubeni Lumbagala, Tanga


Usalama wa maisha ya binadamu ni jambo la msingi sana, na ndiyo maana unapaswa kulindwa kwa gharama zote. Katika suala la usalama barabani ambalo ni muhimu katika kuhakikisha raia wanakuwa salama dhidi ya ajali na majanga mengine yanayoweza kutokea barabarani, suala la madereva wenye sifa stahiki kwa maana ya kuhudhuria mafunzo ya udereva katika vyuo mbalimbali linasisitizwa sana.

Kimsingi, ni kosa kisheria kwa dereva wa pikipiki au gari kuendesha chombo cha moto barabarani bila kuwa na leseni ya udereva. Hii inasisitiza watu kuhudhuria kwanza mafunzo ya udereva, kuhitimu na kupata leseni, ndipo waingie barabarani kuendesha vyombo vya moto. Lakini sheria hii inakiukwa na baadhi ya madereva kukosa leseni zinazotambulika. Wanachofanya baadhi yao ni kujifunza kuendesha vyombo vya moto mitaani na kuingia barabarani, jambo linaloongeza ajali na kusababisha ulemavu na vifo kwa watumiaji wa barabara.

Madereva waliopo chini ya mwamvuli wa Umoja wa Wamiliki na Waendesha Pikipiki na Bajaji Tanga (UWAPIBATA) wanakabiliwa na tatizo la kuendesha vyombo vya moto kama pikipiki maarufu bodaboda na bajaji wakiwa hawana leseni za udereva, jambo linalowaathiri sana kwa kuhatarisha maisha yao na kupigwa faini na askari wa barabarani (trafiki). Kutokana na hali hiyo, wakaamua kuanzisha mfuko wa kukopeshana fedha ili waweze kurasimisha kazi yao kwa kuhudhuria mafunzo kikamilifu ili wapate leseni za udereva.

Kutokana na mahitaji makubwa ya fedha waliyonayo kumudu kulipia mafunzo ili wapate leseni wakawasilisha ombi la fedha kwa Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini (CCM), Ummy Mwalimu, ili aweze kuwasaidia fedha za kutunisha mfuko wao huo ili kuwezesha madereva wengi zaidi kupata mafunzo na hivyo kupata leseni na hatimaye kuwa salama barabarani na kuongeza vipato vyao kupitia kazi yao ya udereva wa pikipiki na bajaji.

Januari 04, 2025, katika viwanja vya Lamore jijini Tanga, Mbunge Ummy Mwalimu alikabidhi fedha kiasi cha Shilingi 10,000,000 (Milioni Kumi) kwa viongozi wa UWAPIBATA ili ziweze kuwasaidia katika kupata mafunzo vyuoni ili kuongeza kasi ya madereva wenye leseni Tanga Mjini . Katika hafla ya kukabidhi fedha hizo, Ummy Mwalimu alisema " Bodaboda ni kazi kama kazi nyingine, mimi kama Mbunge wa Tanga Mjini nitaendelea kuwathamini na kushirikiana nao ili kuboresha mazingira ya kazi zao".

Kitendo cha kuwaunga mkono madereva bodaboda na bajaji ni miongoni mwa mkakati wa Ummy Mwalimu kuwawezesha wananchi kiuchumi hasa vijana kwa kuzingatia kuwa kundi hili ni kubwa, na mafanikio yao kiuchumi yanawezesha pia ustawi wa familia, jamii na Taifa kwa ujumla.

Ni jambo la faraja kuona, fedha hizo zimeleta athari chanya kwani baadhi ya madereva wa bodaboda na bajaji wamepata mafunzo ya udereva na kupata leseni zao, hivyo kufanya shughuli zao za udereva kwa uhuru lakini pia kuongeza vipato vyao na kuongeza usalama wa maisha yao kwani sasa ni madereva mahiri wanaojua sheria, miongozo na kanuni za usalama barabani. 

Kwa hakika, madereva bodaboda na bajaji Tanga Mjini wamepata tabasamu kupitia Shilingi Milioni Kumi zilizotolewa na Mbunge wao Ummy Mwalimu, na hivyo kupata leseni za udereva, jambo ambalo lilikuwa kilio chao cha muda mrefu, lakini sasa limepatiwa ufumbuzi.

Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga.

Maoni: 0620 800 462.








* Ni baada ya kuboresha taarifa zake katika Kituo cha Suji, Mtaa wa Suji Kata ya Mzingani. Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Mhe Ummy Mwalimu leo tarehe 14/2/2025 amefika katika kituo cha kujiandikisha na kuboresha taarifa zake katika Daftari la Kudumu la Mpiga kura ili kuboresha taarifa zake na ametumia muda huo kuhamasisha wananchi wa Jimbo la Tanga Mjini kujitokeza kwa wingi katika vituo hivyo ili kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ili waweze kushiriki kuchagua Rais, Mbunge na Diwani. Akizungumza baada ya kuboresha taarifa zake Mhe Ummy amesema “Nahimiza wananchi wa Tanga Mjini kujitokeza kwa wingi kujiandisha na kuboresha taarifa zao na pia kwa wale ambao watafikisha miaka 18 mwezi wa 10 wanapaswa kujiandikisha ili wapate vitambulisho vya kupiga kura ambavyo pia vinatumika katika masuala mengine muhimu ikiwemo kufungulia account bank na kuombea mikopo.






Na Denis Chambi, Tanga.

MDAU wa maendeleo Mkoani Tanga John Mapima ameiomba Serikali kuunda tume maalum itakayohusika na kuchunguza mienendo ya watumishi katika sekta mbalimbali hapa nchini ikiwemo sekta ya afya ambao wamekuwa wakikiuka miiko yao ya kazi ikiwemo kuwatolea lugha chafu wananchi pale wanapohitaji huduma.

Mapima ametoa ombi  wakati akizungumza na vyombo vya habari  ikiwa ni siku kadhaa zimepita tangu lilipotokea tukio la kujibizana baina yake na mtumishi mmoja wa hospitali ya wilaya Ngamiani iliyopo  jijini hapa ( jina limehifadhiwa) baada ya kuhitaji msaada kiti mwendo wa kwaajili ya kumbebea mgonjwa aliyempeleka kupatiwa huduma siku hiyo.

Kwa mujibu wa Mapima amesema "Nilifika hospitali na mgonjwa nikapewa kiti mwendo ambacho ni kipya kwajili ya kumbebea mgonjwa wangu niliyempeleka  lakini baadaye alitokea nurse mmoja ambaye hakunijibu vizuri alinijibu kwa kejeli na kudai kuwa kiti kile kina mwenyewe baada ya kumhoji majibu yake hayakunipendezesha na alienda ndani kuleta kiti kingine ambacho ni chakavu ili mgonjwa wangu aweze kuwekwa kwenye kiti hicho, tulilazimika kumbebea hivyo hivyo japo hali yake haikuruhusu kulingana na mazingira ya kile kiti ki ukweli Ile iliniumiza sana"

Kufwatia changamoto hiyo aliyokutana nayo ilimlazimu Mapima kwenda kununua kiti mwendo kingine na kukipeleka hositalini hapo ili kuweza kusaidia wahitaji wengine huku akiiomba Serikali pamoja na kuboresha mazingira pamoja na huduma nyingine kutazama hali hiyo ambayo bado uhitaji wake ni mkubwa.

"Nilijiuliza ni wagonjwa wangapi wanaofanyiwa kama mimi ki ukweli sikupendezwa hata kidogo baada ya huduma nikamrudisha mgonjwa wangu nyumbni  kesho yake nilienda dukani kuulizia gharama ya kitimwendo kipya nikakinunua kwa shilingi 250,000  nikawapelekea  nikakutana naganga mfawidhi wa kituo alinipokea vizuri tu" alisema.

"Katika hospitali za umma tunapitia changamoto nyingi sana watumishi waliofanya kazi kwa muda mrefu sehemu moja wanakuwa na mazoea kuna watu wanajibu wagonjwa vile wanavyojisikia wao ningeshauri iundwe tume ambayo itakuwa inapitia wale wafanyakazi waweze kutambua majukumu yao"alisema Mapima. 

Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ikiwemo kuboresha huduma hususani kwenye sekta ya  afya Mapima amewaomba wadau wa Maendeleo kujitokeza kuchangia kwa hali na mali  mahitaji mbalimbali.

" Napenda kuishauri jamii husasan wenzetu wenye uwezo wa kifedha kujitolea  msaada wa vitu mbalimbali ambavyo vina umuhimu na uhitaji mkubwa kulingana na mazingira ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwahudumia wananchi" alisisitiza



Bodaboda nao wachangia milioni  1 kwa ajili ya fomu ya Rais Dkt Samia

Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini Ummy Mwalimu amefanya kikao na viongozi na madereva wa Bodaboda zaidi ya mia tano (500) kupitia Umoja wa Madereva wa Pikipiki na Bajaji  Wilaya ya Tanga (UWAPIBATA) kuzungumzia masuala ya maendeleo ya Bodaboda Tanga Mjini ambapo pamoja na mengineyo Bodaboda kupitia Mwenyekiti wao Mohamedi Chande walimuomba Mh Ummy kuwaunga mkono ili kutunisha Mfuko wao wa  kukopeshana pesa za Leseni kwa Bodaboda. 

Mhe Ummy alikubali ombi hilo na kuwachangia kiasi cha shilingi milioni 10 sambamba na kuwataka bodaboda wengi zaidi kujiunga katika Umoja huo ili kuweza kunufaika na fursa mbalimbali ili kufanya shughuli zao katika mazingira mazuri zaidi.

Wakati huo huo, Bodaboda wa Wilaya ya Tanga kupitia UWAPIBATA wamechangia shilingi miloni moja kwa ajili ya Fomu ya Urais wa Dkt Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi nzuri za maendeleo kwa watu wa Tanga ikiwemo maboresho ya Bandari ya Tanga ambao yameongeza fursa za wateja kwa Bodaboda.

Mhe Ummy alimeshukuru Bodaboda kwa kuchangia Fomu ya Rais Dkt Samia Suluhu na amesema kuwa Mh Rais anastahili kutiwa moyo na kuungwa mkono. 

Aidha ameahidi atashirikiana nao bega kwa bega kutafuta kura za Rais Samia na pia kutafuta wadau mbalimbali ili kuboresha shughuli za bodobda. Sambamba na hilo Mhe Ummy alitoa ofa ya mafuta lita mbili kwa bodaboda wote waliohudhuria.

Shughuli hiyo ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tanga Ndg.Meja mst.Hamisi Mkoba, katibu wa UVCCM Wilaya ya Tanga ndugu Salim Dede, viongozi wa bodaboda wakiongozwa na mwenyekiti wake ndg. Mohamed Chande.

Imetolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini.













 



MBUNGE wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu amesema kazi ya Rais Dkt Samia Suluhu anayoifanya ya Maendeleo katika Mkoa wa Tanga sio ya kutafuta kwa Tochi.

Ummy aliyasema hayo leo wakati akitoa salamu katika Kongamano la Samia Challenge 2024 ambalo limeandaliwa na African Anti-Violence Journalist lililofanyika Jijini Tanga kwenye ukumbi wa Samia Business Centre Kange.

Ambapo alisema kuna miradi mingi ya maendeleo ikiwemo ya Afya,Umeme,Elimu,Maji na Vitega Uchumi karibia kila kona ambayo imechangia kuinua uchumi wa mkoa wa Tanga.


Alisema kwa sababu katika kila eneo la maendeleo utamkuta Rais Samia na kubwa zaidi ambalo wanajivunia nalo ni maboresho makubwa ya Bandari ya Tanga ambapo uwekezaji uliofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu ni wa Bilioni 429.1

“Kutokana na hili sasa tunatembelea kifuata mbele kutokana na uwekezaji huo ambao umeufanya mkoa huo kuanza kupokea meli kubwa zinazoleta shehena za magari na hilo linaonyesha matunda ya uwekezaji katika Bandari kwa kuchimbwa kina na meli kutia nanga gatini “Alisema

 


Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini (CCM) Mhe Ummy Mwalimu leo Octoba 18 mwaka 2024 ametembelea vijiwe mbalimbali katika mitaa ya Mwambani, Mchukuuni, Mwahako, Mwakidila na Mwang'ombe katika kata za Tangasisi na Masiwani kuhamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la mkazi na pia kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakao fanyika tarehe 27/11/2024.

Akizungumza mara baada ya kuvitembelea vijiwe hivyo amesema kuwa mitaa ndio chimbuko la Amani na Maendeleo kwa Wananchi hivyo ni muhimu kila wananchi wa Tanga Mjini kushiriki.



Mbunge wa Tanga Mjini Ummy Mwalimu ameshiriki Ibada ya Misa ya kumuaga aliekuwa Diwani wa kata ya Masiwani Mhe Longson Njau iliyofanyika nyumbani kwake Mtaa wa Njombe Mpirani, Kata  ya Masiwani.

Akitoa salamu za pole kwa familia, ndugu, Waheshimiwa Madiwani wa Jiji la Tanga, Viongozi na wakazi wa Kata ya Masiwani kwa msiba huu mkubwa, Mhe Ummy alisema kuwa  alimtambua Mhe Njau kama diwani mpambanaji alietanguliza mbele maslahi ya wananchi wake wakati wote ikiwemo kuacha alama ya kudumu ya Ujenzi wa Shule ya Msingi Mbugani.

Hata hivyo amewahakikishia wananchi wa Masiwani kuwa katika nafasi yake ya Ubunge ataendelea kuwa karibu nao ili kuhakikisha mwendelezo wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata hiyo hususani maboresho ya barabara.

Aidha Mhe Ummy ameiombea familia  ya marehemu kuwa  na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Ibada ya Misa ya leo ya kumuombea Mhe Njau ilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tanga, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Waheshimiwa Madiwani, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji pamoja na  wananchi wa Kata ya Masiwani na wana Tanga kwa ujumla.







 


Mbunge wa Tanga Mjini Mhe Ummy Mwalimu amezindua Tawi la Coastal Union City Center lililopo barabara ya 8, Jijini Tanga. Akiongea katika Uzinduzi huo Mhe Ummy alieleza kuwa Coastal Union ni timu ya Tanga na hivyo kutoa rai kwa kila mwanaTanga na mwenye mapenzi na Tanga kuiunga mkono timu hiyo ikiwa ni sehemu ya kuijenga Tanga.

Katika uzinduzi huo, Mhe Ummy alikabidhi form za kujiunga na uanachama wa Coastal Union kwa wanachama wapya.

Mlezi wa Matawi ya Wanachama wa Coastal Union Alhajj Salim Bawazir alieleza kuwa wamemualika Mhe Ummy kuwa Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo kutokana na kuthamini mchango wake wa hali na mali alioutoa kwa Coastal Union kupanda daraja na kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara. 

Katika ufunguzi huo, Mhe Ummy amechangia shilingi laki tano katika tawi hilo lililofunguliwa ikiwa ni sehemu ya kuwaunga mkono.


Imetolewa na ;

Ofisi ya Mbunge Jimbo la Tanga Mjini.

18/8/2024



Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amewataka Viongozi wa Kata na Wahudumu wa afya ngazi ya jamii kushirikiana kuwatambua wagonjwa waliofichwa ndani na watu wenye ulemavu ili waweze kupata haki yao ya msingi ya kupata huduma ya afya hatimaye kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Mhe. Nderiananga alitoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo viongozi wa Kata na wahudumu wa afya ngazi ya jamii 170 yaliyoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Apotheker Health Access Initiative kwa kushirikiana na Taasisi ya Dkt. Godwin Mollel Mbunge wa Jimbo la siha na Naibu Waziri wa Afya ambapo alisema kila mwananchi ana haki ya kupata matibabu sahihi kwa mujibu wa sheria bila kujali hali yake ikiwa ni mwenye ulemavu au hana ulemavu huku akiwasisitiza kuwa sehemu ya faraja kwa wagonnjwa badala ya kuwanyanyapaa.

Aliwahimiza kufanya kazi kwa ushirikiano hatua itakayosaidia kuwafichuwa baadhi ya wagonjwa waliofichwa ndani na kukosa matibabu pamoja na kuisaidia jamii kwa kutoa elimu ya masuala ya afya kwa lengo la kuepukana na magonjwa mbalimbali hatimaye kuwa na jamii yenye afya bora.

“Viongozi wa Kata na wahudumu wa afya ngazi ya jamii nyinyi mna jukumu kubwa sana la kuhakikisha mnavumbua wagonjwa waliofichwa, aidha wagonjwa au wenye ulemavu kwani na wao wana haki ya kupata huduma, tusiwaweke ndani watoeni ili wapate msaada kwa sababu kumfungia ndani kunahatarisha afya yake na utakuwa umemfanyia ukatili,” Alisema Mhe. Nderiananga.

Naye Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel alieleza kwamba ni muhimu kwa viongozi wa Kata na wahudumu wa afya ngazi ya jamii kushirikiana katika kuhakikisha usalama wa afya za wananchi katika maeneo yao zinaimarika kwani wao ni watu wa karibu zaidi na jamii husika.

“Nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani amekuwa akitoa fedha nyingi za kutekeleza miradi mikubwa ya huduma muhimu ya afya kama ujenzi wa Vituo vya Afya, hospitali za Wilaya, Mkoa na Rufaa pamoja na kutoa fedha za kununua vifaa tiba kuhakikisha wananchi wanatibiwa vizuri na kupunguza gharama ya kuwasafirisha kwenda nje ya Nchi,” Alipongeza Mhe. Dkt. Mollel.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Operesheni na Programu kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Apotheker Dkt. Angel Dillip amesema kuwa ni muda wa kuwaunganisha wahudumu wa afya ngazi ya jamii na viongozi wa kata kwani wote wanafanya kazi eneo moja hivyo kurahisisha shughuli ya kuimarisha hali ya huduma za afya kwa wananchi endapo watakua pamoja.

Aidha Mkurugenzi wa Mipango, Maendeleo ya Biashara na Sera kutoka Apotheker Dkt. Suleiman Kimatta amewaasa viongozi wa Kata na wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kukabiliana na udumavu.

“Vijana balehe ni kuanzia miaka 10-19 kundi ambalo linatakiwa kuangaliwa sana hususani katika kupunguza kasi ya maambukizi ya UKIMWI, Kupunguza mimba za utotoni, ukatili wa kijinsia, afya ya akili na lishe kwa watoto. Viongozi mna wajibu wa kutumia mikutano yenu kuzungumzia masuala ya afya kuijengea jamii uelewa ili kuepukana na magonjwa mbalimbali,” Alieleza Dkt. Kimatta.

 

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ametoa shukrani kwa nchi ya Switzerland kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kusaidia Sekta ya Afya hasa kwenye uboreshaji wa Utoaji wa huduma za Afya ya Msingi nchini. 

Waziri Ummy amesema hayo leo Julai 29, 2024 wakati akiagana na Balozi wa 'Switzerland' nchini Tanzania Mhe. Didier Chassot katika ofisi ndozo za Wizara ya Afya Jijini Dar Es Salaam aliyedumu kwa muda wa Miaka Minne nchini. 

"Tanzania na Uswisi zina ushirikiano wa muda mrefu wa maendeleo kupitia Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswisi (SDC), maeneo ya sasa ya ushirikiano kati ya Tanzania na Uswisi ni pamoja na kuendelea kuchangia katika Mfuko wa Afya wa pamoja ambapo kupitia awamu ya ufadhili wa moja kwa moja wa Kituo cha Afya (DHFF) Mwaka 2021-2025." Amesema Waziri Ummy 

Waziri Ummy amesema nyanja nyingine wanayoshirikiana na Uswisi ni katika kuchangia kutokomeza Malaria ifikapo mwaka 2030, mpango wa kulinda Afya za vijana (SYP) pamoja na kutoa msaada kwa nafasi ya usimamizi wa ubia na uhamasishaji wa rasilimali ili kusaidia Wizara ya Afya. 

Waziri Ummy ameiomba Serikali ya Uswisi kuiunga mkono na kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa kuendelea kuchangia Mfuko wa Afya wa pamoja na kusaidia utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ili Watanzania wapate huduma za Afya bila kikwazo cha fedha. 

Kwa upande wake Balozi wa Switzarland Mhe. Didier Chassot ameihakikishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kushikiana hasa katika upande wa Sekta ya Afya ikiwemo kuchangia katika Mfuko wa Afya wa pamoja. "Nitaenda kumweleza mwenzangu anaekuja baada yangu jinsi tulivyokuwa tunashirikiana na Serikalinya Tanzania hasa katika kuchangia Mfuko wa Afya wa pamoja lakini pia na ombi hilo la kusaidia kufanikisha Bima ya Afya kwa Wote." Amesema Balozi Chassot

Balozi Chassot ameishukuru Tanzania kwa kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake ambapo pia ameelezea jinsi Watanzania walivyo wakarimu.

 SUALA La Bima ya Afya kwa wote limetakiwa kupewa kipaumbele zaidi katika maandalizi ya Dira ya Taifa 2050 ili kuboresha zaidi huduma za afya ili kila mtanzania awe na afya bora na kuweza kulitumikia Taifa.


Akizungumza  jijini Dar es Salaam katika kongamano la kitaifa la wadau wa sekta ya ya Afya kuhusiana na maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema, Katika kuijenga Tanzania tuitakayo lazima wananchi waone umuhimu wa kuwekeza katika afya na kuingizwa kwa suala la Bima ya Afya kwa wote katika maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kutasaidia kuboresha huduma za afya nchini.

Akieleza mafanikio ya sekta hiyo Waziri Ummy ameeleza kuwa ni pamoja na kufanikiwa kwa kiwango cha juu kwa wanawake kujifungulia katika Vituo vya Afya, kwa kuongezeka kutoka asilimia 41 mwaka 2000 hadi kufikia asilimia 81 kwa sasa na mpango ni kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2025.

Waziri Ummy amesema changamoto kubwa katika sekta ya afya ni ugharamiaji wa huduma za afya, huku akitaja changamoto kubwa kuwepo katika magonjwa
yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo, kisukari na afya ya akili.

"Tukiwa na Bima ya afya kwa wote tutafanikiwa kwa kuwa huduma za afya ni kila kitu, Nchi nyingi katika uchaguzi angalieni Marekani, Uingereza na kwingineko kampeni kubwa ni kuhusu bima ya afya na hifadhi ya jamii, kuna umuhimu mkubwa wa kuwekeza katika gharama za matibabu.” Amesema Ummy.

Aidha kuhusiana na changamoto ya ugharamiaji huduma za matibabu kwa wasiojiweza Waziri Ummy ameeleza kuwa, baada ya muswada kuwa sheria na kuona namna gani watanzania wasio na uwezo watachangia Rais Samia Suluhu Hassan alielewa suala hilo.

“Na tayari chanzo cha ugharamiaji kimepatikana sasa hivi kitagharamia wazee wasio jiweza, watoto wenye umri chini ya miaka mitano na wajawazito na tutaanzia kwa watoto wa umri sifuri mpaka miaka miwili," ameeleza Waziri Ummy.

Akizungumza katika Kongamano hilo Waziri wa Nchi; Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema tafiti imeonesha kuwa asilimia 81 ya Watanzania wanahitaji mabadiliko katika huduma za kijamii ikiwemo uboreshaji wa huduma za afya.

Maoni hayo yaliyokusanywa na Tume ya Mipango kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kutoka kwa watanzania zaidi ya milioni moja, asilimia 81 ya waliohojiwa walipendekeza uboreshaji wa huduma za afya huku asilimia 19 wakitaka upatikanaji wa huduma za afya.

Ameeleza kuwa maoni ya wadau hao ni muhimu na yatapewa kipaumbele katika kuhakikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaleta tija kwa jamii.

Wadau wa sekta ya afya nchini, wametoa maoni yao na kushauri kupewa kipaumbele kwa Bima ya Afya kwa wote ili kuboresha huduma zinazotolewa pamoja na kuwekwa kwa mfumo rasmi katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kupambana na changamoto ya ajira kwa wahitimu wa kada ya Afya wakiwemo madaktari na wauguzi kwa kuwa kada hiyo ni muhimu na wanahitajika zaidi katika jamii hivyo kukosekana kwa wataalam hao huchagiza changamoto ya ubora wa huduma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma (BMH,) Prof. Abel Makubi akitoa maoni katika kongamano hilo amesema kuwa ni muhimu kuwa na mikakati ili fedha inayowekezwa katika kusomesha na mafunzo kwa wataalamu hao ilete tija kwa jamii.

Pia Katibu Mtendaji; Tume wa Mipango Lawrence Mafuru amesema mwongozo na usimamizi wa matayarisho ya Dira hiyo ulipitishwa na Baraza la Mawaziri na utakuwa sheria pindi utakapokamilika rasmi na kuongeza kuwa michango mingi katika simu na midahalo watanzania wanahitaji huduma bora za afya na kueleza kuwa maoni yatakusanywa hadi Agosti mwaka huu na baadaye kupangwa kwa ajili ya utekelezaji.

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imejikita katika maeneo sita ikiwemo maboresho ya Utawala bora, Haki na Amani,Uchumi na Jamii,Utunzaji wa mazingira sayansi ya mabadiliko ya kidijitali na mabadiliko ya tabia Nchi.

Wadau walioshiriki kongamano hilo ni pamoja na Taasisi za Utafiti, wamiliki wa vituo binafsi vya Afya, Taasisi za Elimu, watoa huduma za Afya, Waganga wakuu wa mikoa na wataalam wa Afya.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akizungumza katika kongamano la kitaifa la Wadau wa Sekta ya Afya kuhusiana na maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kueleza kuwa kipaumbele kwa Bima ya Afya kwa wote ni muhimu ili kuboresha huduma za afya. Leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi; Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo akizungumza katika kongamano la kitaifa la Wadau wa Sekta ya Afya kuhusiana na maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kueleza kuwa utafiti unaonesha asilimia 81 ya watanzania wanahitaji mabadiliko katika huduma za kijamii ikiwemo uboreshaji wa huduma za Afya. Leo jijini Dar es Salaam.


Matukio mbalimbali wakati wa kongamano hilo.