Na. Edmund Salaho/Arusha
Waongoza watalii wa safari zaidi ya 750 leo tarehe 12, Decemba 2024 wamepigwa msasa katika semina maalum ikiwa na lengo la kujiandaa na msimu mwingine wa Utalii unaoanza Decemba 2024 hadi Februari 2025.
Semina hiyo ya siku mbili inahusisha vyama vya waongoza watalii vya TTGA, NTSGS, TGS, KTGA, IGS, na FGCI imeandaliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro inafanyika katika ukumbi wa Olasiti jijini, Arusha.
Akifungua semina hiyo ya awamu ya kwanza kwa waongoza watalii hao Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Utalii, Nkoba Mabula aliipongeza TANAPA na Ngorongoro kwa kuandaa semina hiyo na kuwaasa waongoza watalii kujivunia kuitangaza Tanzania duniani.
“Tanzania imepata tuzo nyingi duniani ikiwemo tuzo ya Kivutio bora cha Utalii wa Safari duniani ni lazima tujivunie, nisisitize kuendelea kujitolea kuwa bora kwa kuboresha ujuzi wetu, maarifa yetu kuhusu historia ya Taifa letu, Wanyamapori, maeneo ya kihistoria na utamaduni wetu.”
“Utalii unachangia kiasi kikubwa katika uchumi wetu, waongoza watalii ninyi ni mabalozi wa kiuchumi juhudi zenu zinasaidia kuunda ajira, kuimarisha biashara za ndani, na kuinua jamii jivunieni kuwa kiungo muhimu katika mnyororo huu wa maendeleo”
Aidha, Mabula alisisitiza waongoza watalii kuweka kipaumbele usalama wa wageni,kuboresha huduma na kuweka mazingira mazuri ya ukaribisho katika kila hatua ya safari.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA, Massana Mwishawa alibainisha kuwa kila mwaka mashirika ya TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro yamekuwa na utamaduni wa kukutana na wadau wake wa utalii kuweza kutambua na kujadili namna bora ya kutatua changamoto mbalimbali lakini pia kuendelea kupeana taarifa mbalimbali za maendeleo ya Utalii yanayofanyika katika maeneo yetu ya utalii.
“Kupitia semina hii waongoza watalii wataendelea kujenga uelewa wa pamoja juu ya taratibu mbalimbali tulizojiwekea katika hifadhi ili kuwa na utalii endelevu lakini pia kuhakikisha watalii wanaotembelea hifadhi zetu wanapatiwa huduma bora” alisema Kamishna Mwishawa.
Semina hiyo ya siku mbili inahusisha mada mbalimbali kama Huduma Bora kwa wateja, Uzalendo, Ukarimu na Protokali kwa wageni, Changamoto na fursa za Utalii, sambamba na kuzingatia sheria na taratibu mbalimbali zilizowekwa na Serikali katika maeneo ya utalii.
MWENYEKITI wa Bodi ya Wadhamini TANAPA, Jenerali (Mstaafu) George Waitara akiongozana na Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Kuji, leo tarehe 21, Novemba 2024 wameungana na watanzania kutoa pole kwa wahanga wa ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa - Kariakoo, jijini Dar es Salaam.
“TANAPA, kwa masikitiko makubwa inaungana na jumuiya za wafanyabiashara na watanzania wote kutoa pole kwa wafanyabiashara wa Kariakoo waliofikwa na ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa,ndugu zetu waliopoteza maisha katika ajali hii tunawaombea wapumzike kwa amani, na majeruhi wapone haraka ”. Alisema Jenerali Waitara.
Kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini, Menejimenti na Watumishi wote wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Jenerali Waitara amekabidhi hundi ya malipo ya kiasi cha shillingi Millioni 20 kwa Dkt. Jim James Yonazi Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) ikiwa ni pole kwa wahanga wa ajali hiyo ya kusikitisha ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa.
Katibu Mkuu Dkt.Yonazi, aliishukuru TANAPA kwa namna ambavyo imeguswa na kushirikiana na wananchi katika kutoa pole na kurejesha hali ya wananchi.
“Msaada huu ni mkubwa, chochote ambacho kinapatikana kinafaa kuhakikisha jambo hili linakwenda vizuri wapo wananchi ambao wanachangia elfu moja, na huo ndio utanzania. Tunaendelea kuwashukuru ambao hata hawako hapa kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika jambo hili”. Alisema Dkt. Yonazi.




WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana(Mb) ameipongeza Menejimenti na Watumishi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA),kwa kazi nzuri ya uhifadhi pamoja na ukusanyaji wa mapato yatokanayo na shughuli za utalii.
Ametoa pongezi hizo alipotembelea makao makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), leo tarehe 14,Novemba 2024 jijini, Arusha katika ziara yake ya kikazi.
“Mkakati wa kulinda maliasili ukiwa ndani ya eneo lako ndio haswa ninaoutaka na ninyi TANAPA mnatekeleza vizuri hili unapokuwa ndani ni rahisi kuwasoma majangili natoa maelekezo kwa taasisi zote chini ya wizara kuja kujifunza TANAPA na kwenda kulitekeleza hili”. alisema Balozi Chana.
Pia, Dkt.Chana alitoa rai kwa taasisi zote za wizara kuzingatia maelekezo ya mawaziri nane kuhusu utatuzi wa migogoro ya mipaka, 4R za Rais Samia na kusisitiza uadilifu kwa askari na watendaji wote na kubainisha kuwa ni jukumu kubwa la kuhifadhi ambalo walilopewa kwa niaba ya watanzania
Awali, akimkaribisha Mhe.Waziri, Kamishna wa Uhifadhi-TANAPA, Musa Nassoro Kuji alitoa ufafanuzi wa mafanikio mbalimbali ya shirika hilo ikiwemo juhudi zinazofanywa na TANAPA katika kuimarisha ulinzi na usalama wa rasilimali pamoja na wanyamapori, uboreshaji wa huduma za utalii, utekelezaji wa mfumo wa Jeshi la Uhifadhi pamoja na ukusanyaji wa mapato
“Kwa miaka minne hadi Septemba 2024, hakukuwa na tukio lolote la kuuawa kwa faru kutokana na ujangili, pia matukio ya ujangili wa tembo yamepungua kutoka 15 mwaka 2016/2017 kufikia matukio matatu (3) katika mwaka 2023/2024”.
Aidha, Kamishna Kuji aliipongeza Serikali awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kuruhusu upanuzi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti kujumuisha eneo la Ghuba ya Speke na kubainisha Wananchi/kaya 3,885 sawa na asilimia 91 wameshalipwa fidia zao na tayari wameshaanza zoezi la kuhama kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo hilo.
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana(Mb) ameipongeza Menejimenti na Watumishi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA),kwa kazi nzuri ya uhifadhi pamoja na ukusanyaji wa mapato yatokanayo na shughuli za utalii.
Ametoa pongezi hizo alipotembelea makao makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), leo tarehe 14,Novemba 2024 jijini, Arusha katika ziara yake ya kikazi.
“Mkakati wa kulinda maliasili ukiwa ndani ya eneo lako ndio haswa ninaoutaka na ninyi TANAPA mnatekeleza vizuri hili unapokuwa ndani ni rahisi kuwasoma majangili natoa maelekezo kwa taasisi zote chini ya wizara kuja kujifunza TANAPA na kwenda kulitekeleza hili”. alisema Balozi Chana.
Pia, Dkt.Chana alitoa rai kwa taasisi zote za wizara kuzingatia maelekezo ya mawaziri nane kuhusu utatuzi wa migogoro ya mipaka, 4R za Rais Samia na kusisitiza uadilifu kwa askari na watendaji wote na kubainisha kuwa ni jukumu kubwa la kuhifadhi ambalo walilopewa kwa niaba ya watanzania
Awali, akimkaribisha Mhe.Waziri, Kamishna wa Uhifadhi-TANAPA, Musa Nassoro Kuji alitoa ufafanuzi wa mafanikio mbalimbali ya shirika hilo ikiwemo juhudi zinazofanywa na TANAPA katika kuimarisha ulinzi na usalama wa rasilimali pamoja na wanyamapori, uboreshaji wa huduma za utalii, utekelezaji wa mfumo wa Jeshi la Uhifadhi pamoja na ukusanyaji wa mapato.
“Kwa miaka minne hadi Septemba 2024, hakukuwa na tukio lolote la kuuawa kwa faru kutokana na ujangili, pia matukio ya ujangili wa tembo yamepungua kutoka 15 mwaka 2016/2017 kufikia matukio matatu (3) katika mwaka 2023/2024”.
Aidha, Kamishna Kuji aliipongeza Serikali awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa kuruhusu upanuzi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti kujumuisha eneo la Ghuba ya Speke na kubainisha Wananchi/kaya 3,885 sawa na asilimia 91 wameshalipwa fidia zao na tayari wameshaanza zoezi la kuhama kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo hilo.
Na.Edmund Salaho - Kyerwa Kagera
Serikali imetoa kiasi cha Tsh. Billioni 3.9 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Ibanda - Kyerwa iliyoko mkoani, Kagera.
Akikagua miradi ya ujenzi wa miundombinu hiyo Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Juma Kuji alisema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetupa upendeleo wa kutupatia fedha za kujenga lango la kuingilia watalii (Complex gate), pamoja na Nyumba za kisasa za Watumishi eneo la Kifurusa hii yote kuhakikisha tunapata mazingira mazuri ya kufanyia kazi zetu.
“Hili ni deni ambalo Mhe.Rais wetu ametupa sisi TANAPA na hususani watumishi wa Hifadhi hii na tutamlipa kwa kuchapa kazi na kujituma zaidi katika kulinda na kutunza Rasilimali hizi kwa faida ya kizazi cha sasa na kile cha baadae” alisema Kamishna Kuji.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Fredrick Mofulu, ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ibanda - Kyerwa, alisema ujenzi wa lango hilo la Hifadhi unahusisha sehemu ya ukaguzi wa nyaraka na malipo, ofisi za wahasibu, ofisi za askari upande wa kuingia na kutokea, ofisi ya Afisa Utalii na msaidizi wake, ofisi ya Tehama, ujenzi wa barabara kilometa mbili, na mifumo ya umeme.
Pia, ujenzi wa vyoo upande wa kuingia, na kutokea vyenye mashimo 7 ya kawaida 1 walemavu kwa kila jengo, uchimbaji wa visima viwili, fensi ya umeme mita 400, Nyumba 2 za watumishi (Jengo 1 kwa familia 2), Nyumba 3 za watumishi (Jengo 1 kwa familia 4), vimbweta 08, sehemu ya kupaki magari makubwa na madogo upande wa kutoka na kuingia lenye ukubwa wa kilometa za mraba 5400, mfumo wa umeme jua, pamoja na eneo la kupumzikia wageni. Kazi ambayo inatekelezwa na Kampuni ya MJT Crew Co. Ltd na JV Sumry’s Enterprises Ltd za hapa nchini ambapo mpaka sasa ujenzi uko asilimia 55 na inatarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu.
Msimamizi wa Mradi kutoka kampuni ya MJT Crew Co. Mhandisi Issa Mfaume aliishukuru menejimenti ya Shirika kwa kuwapatia malipo ya mradi kwa wakati na kupelekea kazi kufanyika kwa ubora unaotakiwa na kuahidi kukamilisha kazi hiyo kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vilivyopo kwenye mkataba wa kazi.
Vilevile, Kamishna Kuji alizungumza na Maafisa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa Ibanda - Kyerwa na Hifadhi ya Rumanyika - Karagwe na kusitiza utendaji kazi imara ili kusukuma mbele gurudumu la Uhifadhi na Utalii ambalo tumekabidhiwa na Serikali.
“Wapiganaji ndio nguzo ya kupeleka mbele Shirika letu nitoe pongezi zangu za dhati kwa askari wetu ambao jua ni lao na mvua ni yao kuhakikisha Rasilimali hizi zinalindwa na kuwa urithi kwa vizazi vilivyopo na vijavyo” alisema Kamishna Kuji
Aidha, Kamishna Kuji alisisitiza kuwa kila mtumishi ana haki ya kujiendeleza kielimu, haki ya kulipwa posho kwa kila kazi aliyoifanya, haki ya matibabu, likizo, haki ya kupandishwa cheo pale unapotimiza vigezo vyote vya kiutumishi pamoja na haki ya kuthaminiwa kutokana na kazi unayofanya.
Wapiganaji kwa namna mbalimbali wamepongeza jitihada zinazofanywa taasisi katika kutatua changamoto zao na kupongeza namna viongozi wanawafikia katika maeneo yao, wanasikiliza na kutatua changamoto hizo.
“Nikupongeze Afande Kamishna Kuji licha ya majukumu uliyonayo unatoka na kuja kuzungumza na askari, tumekuona Serengeti, tumekuona uko Saanane, sasa Ibanda Kyerwa na Rumanyika Karagwe ukaribu huu kwetu kama askari na kiongozi wa juu wa taasisi unatia hamasa na morali zaidi ya kuchapa kazi“ alisema askari wa uhifadhi daraja la kwanza Henry Joseph Msabila.





WADAU wa Utalii katika Hifadhi ya Taifa Serengeti wameiomba Serikali kupatia suluhisho la kudumu la ujenzi wa barabara katika Hifadhi za Taifa hususani barabara ya Serengeti
Akizungumza leo na waandishi wa habari ambao wametembelea eneo hilo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Wolway Trekking Tanzania Limited, John Macha alipongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kupitia TANAPA katika kuboresha barabara hizo ambazo kwa kiasi kikubwa zinaathiriwa na wingi wa magari wastani wa magari 600 kwa siku.
Macha aliyasema hayo mbele ya Kamishna ya Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Nassoro Juma Kuji, ambaye alifanya ziara ya kukagua matengenezo yanayoendelea kufanyika katika barabara ya Naabi hadi Seronera.
Kutokana na hali hiyo wadau hao wamependekeza kujengwa kwa barabara yenye tabaka gumu katika hifadhi hiyo ikiwa ni mwarobaini wa tatizo la barabara.
“Niipongeze Serikali kwa matengenezo haya ya barabara kutoka Seronera mpaka Golini tunafahamu hii ni kazi kubwa mnaifanya na tunaomba muendelee nayo lakini kwa ufumbuzi wa kudumu kuwe na jawabu la kudumu kwa sababu magari ni mengi mtakuwa mnafanya zoezi hili ndani ya wiki mbili mpaka tatu mnarudia zoezi hili magari ni mengi sana na ndio chanzo kikuu cha ukorofi wa barabara hii”
“Kwa hiyo lile wazo Serikali kupitia Serengeti la kuwa na tabaka gumu la kudumu lingekuwa wazo zuri sana wakati huu tungesahau matengenezo haya ya mara kwa mara na hata kuongeza gharama ni bora tuingie gharama kutengeneza barabara itakayokaa muda mrefu hata kama ni gharama kubwa,” alisema Macha
Januari 26, 2024 Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Nassoro Juma Kuji alifanya ziara ya kukagua miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na kuiagiza menejimenti ya hifadhi hiyo, kushughulikia kwa haraka maeneo korofi ya barabara ndani ya hifadhi ili watalii wafikie azma yao ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Kutokana na hali hiyo aliilekeza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kurekebisha maeneo yote korofi na kuhakikisha kuwa hakuna maeneo ambayo hayatapitika ili kupunguza adha hiyo kwa wageni
“Shirika limeazimia kushughulikia kwa haraka maeneo yote korofi ikiwa ni hatua za haraka, lakini lengo kuu ni kuhakikisha barabara hizi zinakuwa na tabaka gumu, haya ni maagizo yangu kwa menejimenti kuhakikisha barabara zote zinapitika wakati wote,” alisema Kamishna Kuji.
Aidha, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya barabara katika hifadhi za Taifa zote nchini.
Pia, Kamishna Kuji amebainisha kuwa TANAPA inafanya jitihada za haraka kuhakikisha miundombinu yote katika Hifadhi zote za Taifa nchini inaboreshwa ili kukidhi matamanio ya wageni wanaotembelea hifadhi hizo zilizosheheni sifa lukuki za kuwa na utajiri mwingi wa bayoanuai.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayeshughulikia miundombinu Mhandisi Dkt. Richard Matolo alibainisha kuwa Shirika limekuwa likitumia teknolojia mbalimbali kutafuta mwarobaini wa changamoto za barabara na kubainisha kuwa mwaka huu hali imekuwa tofauti kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na idadi ya magari yanayotumia barabara hiyo.
“Shirika limefanya majaribio mbalimbali na kuja na teknolojia ambazo zitapelekea barabara hizi hususani hii ya Naabi iwe inapitika wakati wote tafiti nyingi zilionekana haziwezi kuleta matokeo chanya katika maeneo haya kutokana na asili ya udongo wa hifadhi zetu hivyo kutokana na stadi zote imethibitika kuwa tunaweza kutumia tabaka gumu kujenga barabara hizi,” alisema
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Stephen Msumi alisema kuwa menejimenti ya Serengeti imejipanga kuhakikisha maeneo korofi yanarekebishwa na kutoa rai kwa waongoza watalii kuzingatia sheria na taratibu mbalimbali katika hifadhi ikiwemo kudhibiti mwendokasi pamoja na kuzingatia alama mbalimbali za barababra ili kuepusha madhara yanayojitokeza kwa kutozingatia sheria hizo.
Hifadhi ya Taifa Serengeti inafanya ukarabati wa barabara zake ili kuondoa adha hiyo na kuzifanya barabara zote ndani Hifadhi ya Taifa Serengeti kupitika mwaka mzima.








Na. Edmund Salaho - Kimotorok Simanjiro
Mgogoro wa ardhi baina ya Hifadhi ya Taifa Tarangire na Kijiji cha Kimotorok wilayani Simanjiro Mkoani Manyara uliodumu kwa zaidi ya miaka 20 umefikia tamati baada ya kuwekwa mipaka mipya ya Hifadhi ya Taifa Tarangire ambapo wananchi wa Kijiji hicho wamepatiwa eneo la kilomita za mraba 17.77 sawa na ekari 4392
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Afisa Misitu Mkuu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Michael Gwandu, aliwataka wananchi wanaopakana na maeneo ya hifadhi kuheshimu mipaka iliyowekwa kwa mujibu wa sheria ili kupunguza migogoro ambayo serikali inalazimika kutumia gharama kubwa kuitatua.
Afisa Wanyamapori Mkuu ambae pia anashughulikia kitengo cha utatuzi wa migogoro ya maeneo yaliyohifadhiwa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Pellage Fransis Kauzeni, alisema zoezi hilo linatekelezwa kufuatia ushauri wa Kamati ya Mawaziri nane wa kisekta iliyoundwa na serikali ili kukusanya maoni kuhusu migogoro kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi.
Bw. Pellage aliongeza kuwa eneo hilo litasaidia wananchi hao ambao walishaanza kulitumia kwa ajili ya shughuli za kijamii ikiwemo kilimo, malisho na makazi.
Na kuongeza kuwa wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo linazingatia kutokuingilia mfumo wa ikolojia na kubainisha kuwa mojawapo ya maagizo ya Baraza la Mawaziri baada ya uamuzi wake ni kuwekwa alama za kudumu zinazoonekana ili iwe rahisi kila mmoja kuona mpaka wake.
Naye, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Tarangire Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi - Beatrice Kessy, amesema kamati hiyo ilishauri kilomita za mraba 17.77 ambazo ni sawa na hekari 4,392 zimegwe katika eneo la hifadhi na kurejeshwa kwa wananchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Aidha, Kamishna Kessy alisema eneo linalowekwa mpaka huo lina urefu wa kilomita 10 ambalo wanatarajia kuweka vigingi 30 na hadi sasa wameweka vigingi 22 na kuwa zoezi hilo lililoanza Juni 12,2023 litakamilika kabla ya Juni 30.
Pia, aliongeza mgogoro huo wa zaidi ya miaka 20 ulisababisha shughuli za uhifadhi, doria, uwekezaji na shughuli za wananchi kushindwa kutekelezwa, hivyo wanaamini baada ya kuisha kwa mgogoro mahusiano baina ya hifadhi na wanakijiji yataboreka zaidi ikiwa ni pamoja na shughuli za uhifadhi na utalii zitaendelea.
"Mgogoro huu umechelewesha maendeleo ya wananchi na shughuli za uhifadhi na utalii katika upande huu wa Kusini mwa Hifadhi ya Taifa Tarangire, kwa sasa shughuli za utalii zitafanyika kwa sababu hata ukimpa mwekezaji kuwekeza itanufaisha jamii na kusaidia kuendeleza uchumi wa kijiji na kuchangia kwenye pato la taifa,kuliko ilivyokuwa awali ambapo huwezi hata kuendeleza shughuli za utalii mfano kuanzia walking safari," alisema Kamishna Kessy.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho cha Kimotorok,Elias Pamelo, amesema wanatarajia baada ya mgogoro kuisha ujirani baina yao na hifadhi hiyo utaimarika na kuomba serikali kuangalia namna ya kusaidia maeneo machache ambayo bado yako nje ya kijiji hicho kurudishwa kwao.
"Mgogoro huu na sisi kama wananchi tunatamani uishe kwa sababu ni wa muda mrefu ila tunaomba serikali kwenye mapungufu ni kidogo hivyo tutakapopata nafasi tena licha ya kuwa tumepewa eneo kubwa ambalo awali lilikuwa la hifadhi ila kuna eneo ambalo limeonekana ni la hifadhi na tulikuwa tunatumia kwa ajili ya malisho,makazi na mashamba tungeomba hilo tuongezewe,"amesema
Naye, mzee wa mila la kabila la kimasai Laigwanan,Loserian Siria, alishukuru serikali kwa utatuzi wa mgogoro huo na kuomba kuangalia namna serikali inaweza kuongeza eneo kwa ajili ya kijiji hicho ambalo limeonekana kuwa ndani ya hifadhi huku kukiwa na maboma kadhaa ndani yake.
Wakati kila jitihada zikifanywa kwa ajili ya kunusuru uhifadhi katika Bonde la Usangu na Hifadhi ya Ruaha , shughuli za binadamu kama vile mifugo na uvuvi, zimeendelea kufanywa usiku, wananchi wakihisi kuwa majira hayo askari wanakuwa hawapo mbugani.
Kufuatia hatua hiyo TANAPA imebaini njama hiyo na tayari Ng'ombe zaidi ya 300 wamekamatwa kwenye Hifadhi ya Ruaha katika Bonde la Usangu /Ihefu Novemba 07, 2022 majira ya saa mbili usiku huku wafugaji wakiamini askari wa uhifadhi watakuwa wamelala.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye kituo cha Ikoga Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya Afisa Uhifadhi wa Tanapa Benedict Mwageni amesema kuwa wanafanya kila jitihada ya kuhakikisha shughuli za kibinadamu hazifanyiki katika bonde hilo.
Amesema wananchi wanaamini kuwa wakati wa usiku askari wanakuwa wamelala hali ambayo kwao kulala sio sehemu ya kazi zaidi ni kulinda hifadhi ya Ruaha.
"Iwe usiku iwe mchana Tanapa tutahakikisha kuwa tunakamata kila kitu kitakachoingia katika hifadhi" alisema Mwageni.
Mwageni amesema kuwa wananchi waache kuingiza mifugo kwenye hifadhi kwani kwa sasa nchi iko kwenye mgao wa umeme kutokana na mto Ruaha kukauka huku wanyama wakikosa maji na kufuata mabwawa ambayo kuna watu wanaendesha shughuli za uvuvi.
Amesema licha ya kuwa na wafugaji walioko karibu na hifadhi ,wamekuwa wakiingiza mifugo kuanzia saa mbili na kuitoa saa nane usiku kwa mategemeo ya askari watakuwa wamelala ambayo hiyo mbinu wameshagundua.
Hata hivyo amesema Ng'ombe hao waliokamatwa taratibu za kisheria zitafuatwa ikiwemo kuwapeleka mahakamani na maamuzi yatatolewa.
Kwa upande wa Mraghabishi na Mdau wa Mazingira Seleman Msindi ((Afande Sele) amesema kuwa suala la mifugo katika hifadhi ndio imesababisha mto Ruaha Mkuu kukauka na wanyama wanapata adha ya upatikanaji maji.
Msindi amesema kuwa kunatakiwa serikali kuangalia eneo la ufugaji na kujirudia wananchi kuingiza mifugo katika mto Ruaha ipo siku Ng'ombe watataifishwa na kugaiwa nyama makundi mbalimbali itakuwa fundisho kutokana na kuzoea faini au kuongeza faini.
Wakati ng’ombe hao wakikamatwa, vijana waliokuwa wakiwachunga hawakuweza kuonekana eneo hilo ila kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa ni kwamba wanasubiri ng’ombe zao zipelekwe kwenye kituo cha kuwakusanya ili waweze kuwatambua na kisha kulipa faini.
Kwa mujibu na sheria za uhifadhi, kila ng’ombe anatakiwa kulipiwa faini ya shilingi laki moja (Sh100,000) na mara nyingi huwa wanalipa faini na kuondoka na mifugo yao, jambo ambalo limekuwa halipunguzi tatizo bali linafanya jambo hilo kuwa la kujirudia
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) limetangaza ukomo wa utumishi wa maofisa wake wawili kwa sababu ambazo hazijawekwa bayana.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma, watumishi hao ni Kamishna Mwandamizi wa Uhifadhi, Pascal Shelutete na Ofisa Uhifadhi Mwandamizi, Justin Lema na kwamba utumishi wao umekoma kuanzia Septemba 15, 2022.
“Uongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania unaujulisha umma wa Watanzania na wadau wote wa uhifadhi na utalii kuwa waliokuwa watumishi waandamizi wa Tanapa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Pascal Shelutete na Ofisa Uhifadhi Mwandamizi, Justin Lema, utumishi wao umekoma kuanzia Septemba 15, 2022.
“Shirika halitahusika na jambo lolote watakalojihusisha nalo kwa niaba ya shirika,” inaeleza taarifa hiyo ambayo hata hivyo haijabainisha sababu za kukoma kwa utumishi wao.
Mwananchi lilimtafuta Ofisa Uhifadhi Mwandamizi wa Tanapa anayeshughulika na Mawasiliano, Catherine Mbena kujua sababu za kukoma kwa utumishi wa maofisa hao, hata hivyo hakuwa tayari kuzungumzia sababu hizo akidai kwamba shirika halijataka kuweka bayana.
“Tukiwa tunataka kufanya hivyo (kueleza sababu) tutawaambia, lakini for now (kwa sasa) tuna hilo tangazo tu,” amesema Mbena
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Fatma Mwassa ametoa rai kwa Jeshi la uhifadhi, Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kutumia rasilimali za Hifadhi kibiashara ili kuongeza idadi ya watalii na kuchagiza ongezeko la mapato kupitia sekta ya Utalii.
Mhe. Fatma Mwassa ametoa rai hiyo leo Agosti 14,2022 alipofanya ziara ya kikazi kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo hifadhini ikiwa ni mpango kuangalia utekelezaji wa maelekezo mbalimbali ya serikali kuhusu uimarishaji wa shughuli za uhifadhi na uboreshaji huduma za utalii.
Mkuu wa Mkoa alisema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha miundombinu ya utalii sambamba na kuimarisha shughuli za uhifadhi wa maliasili kwenye Hifadhi za Taifa.
‘’Kama ambavyo mnafahamu utalii ni kipaumbele kwa nchi, kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameamua kuwekeza zaidi kwenye utalii ili kuongeza mapato zaidi, tunatakiwa kuendelea kufanya biashara ya utalii wenye tija ili kuongeza pato la taifa’’ Alisema Mhe Fatma Mwassa.
Aidha, Mhe. Fatma Mwassa alisema kuwa Serikali ya mkoa inaunga mkono shughuli mbalimbali zinazofanywa na Hifadhi ikiwa pamoja na kupambana na kudhibiti ujangiri ambapo amewataka Hifadhi Taifa ya Mikumi na Kanda ya Mashariki kuendelea kupambana na kudhibiti ujangiri na uharibifu wa mazingira.
‘’Hatuwezi kuruhusu ujangiri katika mkoa huu. Tunatakiwa kuweka mikakati madhubutu kukabiliana na changamoto hii. Tusilegeze kamba hata kidogo kwa sababu na jangiri wanaoua wanyamapori ndio haohao wanaua hata watu. Hivyo, wasipewe mwanya. Serikali ipo pamoja nanyi kuukabili ujangiri na uharibifu wa mazingira ndani na nje ya hifadhi.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ameitaka menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Mikumi kuendelea kujitangaza zaidi na kwa kuweka bajeti maalumu ili kuongeza idadi ya watalii na mapato. Alishauri kujitangaza kupitia majarida na tovuti za mitandao ya kijamii ili jamii iweze kutambua vivutio vilivyo hifadhini na pia kujua maendeleo makubwa ya uboreshaji miundombinu ya Barabara, kiwanja cha ndege na maeneo ya malazi ya gharama nafuu iliyo ndani ya Hifadhi hiyo.
‘’Kwenye suala zima la biashara ni lazima tujitangaze. Maendeleo yaliopo sasa katika Hifadhi ni makubwa sana lazima wananchi wayatambue, wakati tunayafanya haya kwenye hii idara yenu ya mahusiano vitu vyote vinanyofanywa hapa hakikisheni vimeandaliwa kwa namna bora ya kuwavutia watalii kwa kufanya maandalizi bora ili kukuza soko la utalii wa kibiashara’’ Alisema Mhe. Fatma Mwassa
Kwa upande wake Mkuu wa Kanda ya Mashariki Kamishna Msaidizi Mwandamizi Massana Mwishawa akaeleza kuhusu mikakati ya kudhibiti ujangiri ndani na nje ya hifadhi, kuendeleza mahusiano kati ya hifadhi na jamii pamoja na kuendelea kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kwenye soko la ndani na nje ya nchi kwa kutangaza vivutio vya asili, malikale na tamaduni za watanzania kwa kule ya zaidi vivutio vilivyo kwenye mkoa wa Morogoro.
“TANAPA tumejipanga vizuri kupambana na kudhibiti ujangiri. Tunatekeleza hilo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na pia kuendelea kushirikiana na ofisi yako. Vile vile, tutaendelea kuboresha mahusiano na jamii sambamba na kuendelea kutangaza vivutio vilivyo kwenye Hifadhi ya Mikumi.
Serikali ya awamu ya sita imejidhatiti kuboresha sekta ya utalii nchini kwa kuboresha miundombinu ili kuzifanya Hifadhi za Taifa nchini ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kuweza kufikika na kuzifanya Hifadhi ziweze kuongeza mapato.
Na. Catherine Mbena /TANAPA.
Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), William Mwakilema amewataka makamishna wapya kufanya kazi kwa weledi, ushirikiano na kufuata utaratibu katika kutekeleza majukumu yao mapya.
Kamishna Mwakilema ameyasema hayo leo katika Makao Makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania jijini Arusha wakati wa zoezi la kuwavisha vyeo na kuwaapisha makamishna wateule wa Uhifadhi walioteuliwa na Bodi ya Wadhamini ya shirika hilo kushika nafasi mbalimbali za uongozi.
“Mmeaminiwa na Bodi ya Wadhamini kutekeleza majukumu haya, pale mtakapohitaji usaidizi wetu msisite, tupo tayari wakati wote. Uongozi wa pamoja iwe ndiyo nguzo yenu katika utendaji kazi.” Alisema Mwakilema.
Aidha, Kamishna Mwakilema amewaasa kuwa na umoja, mshikamano, nidhamu na uadilifu pamoja na kufanya kazi kwa bidii hasa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya maendeleo ya TANAPA, na miradi ya ufadhili pia kuhakikisha inakamilika kwa wakati kwa kuzingatia thamani ya fedha za miradi hiyo.
Akishuhudia tukio, hilo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma Mkomi aliwaasa watumishi wa TANAPA kuwa na umoja katika utendaji kazi ili kuleta tija iliyokusudiwa pamoja na kuongeza juhudi za kuhifadhi maeneo yote ili juhudi zote zilizofanyika za kutangaza utalii ziweze kufanikiwa.
Hivi karibuni Bodi ya Wadhamini ya TANAPA ilifanya uteuzi katika nafasi mbalimbali za uongozi pamoja na upandishwaji vyeo wa viongozi waandamizi wa shirika kwa lengo la kuboresha utendaji kazi ambapo ilimpandisha cheo Afisa Uhifadhi Mkuu, Richard Shilunga kuwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Nyerere,
Afisa Uhifadhi Mkuu, Dkt. Emillian Kiwhele alipandishwa cheo kuwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Idara ya Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara Kanda ya Kaskazini
Afisa Uhifadhi Mkuu, Sonia Lyimo alipandishwa cheo kuwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Idara ya Huduma za Shirika Kanda ya Magharibi.
Pia Afisa Uhifadhi Mwandamizi, Salim Mjema alipandishwa cheo kuwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Idara ya Huduma za Shirika Kanda ya Kaskazini.
.jpeg)









.jpg)




















.jpeg)

.jpeg)







.jpeg)