Articles by "OSHA"
‏إظهار الرسائل ذات التسميات OSHA. إظهار كافة الرسائل

 


Wajasiriamali wadogo wapatao 500 wanaojihusisha na uchimbaji na uchakataji kokoto Jijini Dar es Salaam wamewezeshwa vifaa kinga na kupatiwa mafunzo ya usalama na afya ili kujiepusha na ajali, magonjwa na vifo vinavyoweza kusababishwa na vihatarishi vilivyopo katika mazingira ya kazi.


Uwezeshaji huo umefanywa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ikiwa ni utekelezaji wa jukumu lake la msingi la kujenga uelewa wa masuala ya usalama na afya miongoni mwa waajiri, wafanyakazi na wananchi kwa ujumla.

Makundi yaliyonufaika na uwezeshaji huo kwa hatua ya awali ni wale ambao wanafanya shughuli zao katika maeneo ya Boko Magereza, Kata ya Bunju katika Wilaya ya Kinondoni na maeneo ya Mjimwema katika Wilaya ya Kigamboni.

Akifungua program hiyo ya uwezeshaji wa wachimbaji wadogo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, amesema pamoja na changamoto zinazowakumba wachimbaji na wachakataji wadogo wa kokoto ikiwemo matumizi ya teknolojia duni na ukosefu wa mitaji, mchango wa wachimbaji hao katika uzalishaji wa malighafi za ujenzi ni mkubwa.

“Ninapenda kuwatia moyo kwamba changamoto zilizopo katika sekta hii hazitakuwa za kudumu. Hivyo, niwaombe tushirikiane kuchukua hatua za kuleta mabadiliko chanya katika sekta hii ikiwemo kuhakikisha kwamba shughuli zote zinafanyika katika mazingira salama na tija inaongezeka kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa,” ameeleza Waziri Kikwete na kuongeza:

“Kwa upande wetu kama serikali tumeshaanza kuchukua hatua kwa kuanzia na kuwapa elimu kama inavyofanyika leo lakini tutaendelea na hatua nyingine ikiwemo kutengeneza mazingira wezeshi yatakayopelekea tija kuongezeka ikiwemo kuhakikisha mnapata mitaji kwa ajili ya kununua zana za kisasa ikiwa ni pamoja na kuanzisha shughuli mbadala.”

Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya Masuala ya Kazi, Bi. Mary Ngelela Maganga, aliyehudhuria baadhi ya madarasa ya semina iliyokuwa ikiendeshwa na wataalam wa OSHA, amesema kwa kuzingatia mchango wa wajasiriamali wadogo katika maendeleo ya nchi, Taasisi yake ya OSHA imeona ni muhimu kuwapa elimu ya usalama na afya wachimbaji hao ili waweze kuchukua tahadhari dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema mafunzo yanayotolewa na wataalam wake kwa wachimbaji wadogo yamejikita katika kuwawezesha kutambua vihatarishi vinavyoambatana na shughuli zao ikiwemo vumbi, joto kali na mtindo wa ufanyaji kazi usiozingatia taratibu za igonomia.

Aidha, Kiongozi huyo Mkuu wa Taasisi ya OSHA ameeleza kuwa mafunzo hayo yanaambatana na utoaji wa vifaa kinga muhimu vilivyogharamiwa na serikali ili kuwahamasisha wachimbaji hao kuzingatia matumizi sahihi ya vifaa kinga katika kazi zao.

Vifaa kinga vilivyotolewa kwa wajasiriamali hao ni pamoja na barakoa, vikinga mikono (gloves), vizibao vinavyoakisi mwanga (reflective vests) kutambulisha uwepo wa mfanyakazi mahali pa kazi pamoja na masunduku ya huduma ya kwanza.

Wajasiriamali walionufaika na uwezeshaji huo akiwemo Bi.Berena Bilal, wameishukuru serikali kupitia OSHA kwa uwezeshaji waliopata.

“Kwa niaba wajasiriamali wenzangu naishukuru OSHA kwa kutuelimisha na kutuletea vifaa kwani awali tulikuwa hatufahamu hatari zinazotuzunguka lakini leo wataalam wametufahamisha na kutupatia mbinu za kudhibiti hatari hizo,” amesema Bi Berena Bilal.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, akizungumza na wachimbaji na wapondaji wa kokoto waliowezeshwa na OSHA kwa kupatiwa mafunzo ya usalama na afya pamoja na vifaa vya kujikanga katika machimbo ya Masasi, Mjimwema, Kigamboni Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Bi. Mary Ngelela Maganga, akimkabidhi kiongozi wa wachimbaji na wapondaji wa kokoto wa eneo la Boko Magereza, sanduku la huduma ya kwanza mara baada ya kuwapa mafunzo ya usalama na afya kazini.


Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya usalama na afya kwa wachimbaji na wapondaji wa kokoto Kigamboni Jijini Dar es Salaam.

Mkufunzi wa Huduma ya Kwanza wa OSHA, Bi. Moteswa Meda akiwaongoza washiriki wa mafunzo ambao ni wapondaji wa kokoto wa eneo la Boko Magereza kufanya mazoezi ya kutoa huduma ya kwanza kwa vitendo.


 Wakala wa Usalama Mahala Pa kazi (OSHA) imefuta tozo za ada 10 zenye thamani ya Sh.Bilioni 35 ambazo fedha hizo ilikuwa ikipata kila mwaka ikiwa ni kupunguza mzigo kwa wawekezaji kuhusiana na kulipia tozo.

Hayo ameyasema Mtendaji Mkuu wa OSHA  Khadija Mwenda wakati akizungumza katika kikao cha Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Waandishi wa Habari kwa uratibu wa Ofisi ya Masjili wa Hazina kilichofanyika jijini Dar es Salaam.


Mwenda amesema kuwa  katika mafanikio ya Miaka mitatu ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan baada kutoa tozo hizo  OSHA haijaweza kuteteleka lengo ni kuhakikisha nchi inapata wawekezaji wengi ambao watachochea uchumi na ajira kwa watazania.

"Baada kupunguza na kuondoa baadhi ya ada za huduma ambazo haujaadhiri usimamizi na utoaji wa huduma za usalama wa afya mahali pa kazi nchini," amesema  Mwenda.
Amesema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amefungua mipaka ya uwekezaji nchini hivyo OSHA kazi yake ni kuendana na Rais katika kuhakikisha adhima ya Rais Wetu inatimia inayoendana na vitendo vya watendaji wake.

Aidha amesema OSHA inaangalia usalama mahala pa kazi kwa kipindi cha miaka mitatu wameweza kufanya ukaguzi katika maeneo ya kazi  yote na kuwapa cheti.

Amesema mafanikio  ya Wakala katika kipindi cha miaka  mitatu kuanzia mwaka 2021 hadi  2023 kuhimarika kwa shuhuli za usimamizi mahala pa kazi nchini  ambapo wakala amefanikiwa kuongea idadi ya maeneo ya kazi yaliyo sajiliwa kutoka 4336 hadi 30306 ongezeko hilo sawa na asilimia 599.

Mwenda amesema  OSHA kwa kushirikiana na wadau  wanaanda mpango  wa kutambua matumizi ya simu kwenye  vituo vya mafuta si salama  wanahitaji kutoa elimu zaidi namna ya kuboresha utoaji huduma juu ya malipo ya simu kwenye vituo hivyo.

"Kushirikiana na wadau kutengeneza  mpango wa kutambua  matumizi  ya simu kwenye vituo vya mafuta si salama kwa kutengeneza vibonzo kwa ajili elimu zaidi  watu waelewe sii salama  kazi  yetu kubwa  osha ni kuzuia na kutoa elimu, "amesema Mwenda.

Amesema   Dkt.Samia Suluhu Hassan amekuwa  akifanya juhudi kuhakikisha kuwa wawekezaji  wanakuja kuweza nchini  ikiwemo kuhimiza  uboreshaji  wa mazingira ya biashara  kuwa wezeshi na hili ni pamoja  na maelekezo  mbalimbali katika hotuba zake. 

Amesema  kuwa wao kama OSHA  wamefanya mapitio ya mlolongo wa shughuli  zao wa kuweza kubaini  maeneo yanayohitaji maboresho  katika utoaji wa  huduma  katika kulinda afya na usalama mahala pa kazi 

"Baada yakufanya na kujiridhisha kwa  mapitio hayo  tukakuta kuna maeneo  yanahitaji  maboresho  ambapo miongoni mwa maeneo yaliyoonekana kuwa na uhitaji wa maboresho tunafanya utatuzi katika  kufanya sehemu za kazi zinakuwa salama ili kuwa na uzalishaji wa nguvu kazi unakuwa unatija kwa Taifa".Amesema Mwenda 

Amesema ada zilizofutwa  ama kupunguzwa na OSHA zimeleta unafuu ambao unachochea ukuaji wa biashara na uwekezaji nchini ikiwemo Kuongeza ajira kwa watanzania.

Ameeleza kuwa kiasi cha ada zilizopunguzwa zinakadiriwa kuwa zaidi ya bilioni 35 ambapo imependeza Rais Dk.Samia  fedha  hizo zitatumika katika kuhimarisha mifumo  ya kulinda wafanyakazi waweze kuzalisha kwa tija.
Hata hivyo amesema idadi ya ukaguzi zilizofanyika zimeongezeka kutoka kaguzi 104,203 hadi kufikia kaguzi 776,968 sawa na asilimia 646 kaguzi hizo zilizohusisha ukaguzi wa jumla.

Amesema Taasisi ya OSHA amefanikiwa  kusimika mfumo wa TEHAMA  wa usimamizi wa taarifa  za kaguzi nchini  ambapo kupitia  mfumo huo huduma ya utoaji wa taarifa  za ukaguzi ajali na mfumo unafanyika kwa njia ya kieletroniki.

Mwenda  akizungumza kuhusu  changamoto zinazowakabili amesema baadhi ya waajiri kutotekeleza ipasavyo sheria namba 5 ya usalama na afya mahala pa kazi  wanaosimamia ikiwemo kuto wasilisha taarifa za ajali zinazotokea maeneo ya kazi. 

Amesema,  katiba ya nchi inasema kila binadamu  ana haki ya kuishi inatambua  hilo na wana  program kila maeneo  wanafikia kutoa elimu kulinda vijana. 

Amesema OSHA imekuwa kimbilio kwa nchi nyingine kujifunza  na hiyo kutokana kuwa mifumo thabiti ya utoaji huduma kuwa umetukuka pamoja na kupata kutambulika kimataifa pamoja na Shirika la Kazi Duniani (ILO).Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama Mahala Pa Kazi (OSHA) Khadija Mwenda akizungumza na Jukuu la Wahariri (TEF) na Waandishi wa Habari kuhusiana na mafanikio ya OSHA kwa miaka mitatu ya awamu ya sita ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan Jijini Dar es Salaam.Kaimu Mwenyekiti Jane Mihanji akitoa maelezo kuhusiana na ushiriki wa wahariri katika kikao kati ya OSHA na TEF jijini Dar es Salaam.Afisa Habari Mwandamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina Sabato Kosuri akizungumza kuhusiana na uratibu wa Ofisi hiyo kwa Taasisi zilizo chini ya Msajili kueleza juu ya ufanisi wa kazi zao ,jijini Dar es Salaam

Baadhi ya wahariri na waandishi wa habari katika mkutano kati ya TEF na OSHA jijini Dar es Salaam.