Articles by "INEC"
‏إظهار الرسائل ذات التسميات INEC. إظهار كافة الرسائل


Na Mwandishi wetu, Magu

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele leo Aprili 23,2025 ameongoza kikao cha pamoja kati ya Tume na Wadau wa Uchaguzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mkoani Mwanza kwa lengo la kujiridhisha iwapo taarifa zilizopo kwenye maombi yaliyowasilishwa ya kuligawa jimbo la Magu ni sahihi kuhusu jimbo husika.

 

”Tulipokea maombi ya mapendekezo ya kugawa jimbo la uchaguzi la Magu kupitia barua yenye Kumb. Na. CFA.89/231/01C/20 ya tarehe 11 Machi, 2025 kutoka kwa Katibu tawala Mkoa wa Mwanza, hivyo kikao hiki ni kifupi, lengo lake ni kujiridhisha na takwimu na jina la jimbo kama mlivyowasilisha ikiwa ni sehemu ya jukumu la Tume la kuwashirikisha wadau wake wa uchaguzi,”alisema Jaji Mwambegele.

 

Alisema, Tume imechagua kutembelea baadhi ya majimbo yaliyoomba kugawanywa kwa lengo la kujiridhisha iwapo taarifa zilizopo kwenye maombi yaliyowasilishwa ni sahihi kuhusu jimbo husika.

 

Jaji Mwambegele alisema kwa mujibu wa ibara ya 75(4) na 74(6)(c) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 ikisomwa pamoja na kifungu cha 10(1)(d) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 1 ya mwaka 2024, Tume ina jukumu la kuchunguza na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika majimbo ya uchaguzi. Aidha, Tume inaweza kutekeleza jukumu hilo mara kwa mara au angalau kila baada ya miaka kumi.

 

”Aida, ibara ya 75(3) na (4) imeainisha vigezo vya ugawaji wa majimbo ambavyo ni idadi ya watu, upatikanaji wa mawasiliano, na hali ya kijiografia. Vigezo vingine vinavyozingatiwa na Tume katika kugawa majimbo vimeainishwa katika Jedwali la Tatu la Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za Mwaka 2024,”alisema Jaji Mwambegele.

 

Jaji Mwambegele alivitaja vigezo vingine vinavyohusika katika ugawaji wa majimbo kuwa ni pamoja na hali ya kiuchumi, ukubwa wa eneo la jimbo husika, mipaka ya kiutawala, jimbo moja kutokuwa ndani ya Wilaya au Halmashauri mbili, mpangilio wa maeneo ya makazi ya watu yaliyopo, mazingira ya muungano, uwezo wa ukumbi wa Bunge; na  idadi ya viti maalum vya wanawake.

 

Miongoni mwa waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na viongozi wa Mkoa wa Mwanza, Viongozi wa Wilaya ya Magu, Viongozi wa Vyama vya Siasa Magu, Wawakilishi wa makundi mbalimbali ya wanawake, vijana, wenye ulemavu na wazee wa Kimila.

 

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilitangaza kuanza kwa mchakato wa kuchunguza na kugawa au kubadili majina ya majimbo ya uchaguzi ambapo ilipokea  mapendekezo kuanzia tarehe 27 Februari, 2025 hadi tarehe 26 Machi, 2025.

 Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kuanza kwa mzunguko wa 12 wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambao utafanyika mkoani Morogoro na sehemu ya mkoa wa Tanga kwa siku saba kuanzia tarehe 01 had 07 Machi, 2025.

 

Akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi mkoani Morogoro leo tarehe 17 Februari, 2025, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa, Jacobs Mwambegele amesema uboreshaji huo utafanyika kwenye mkoa huo na mkoani Tanga kwenye halmashauri za Wilaya ya Bumbuli, Handeni, Pangani na Mkinga.

 

“Kwa mujibu wa ratiba, kwa sasa Tume imeanza maandalizi ya mzunguko wa 12 kati ya mizunguko 13 ya uboreshaji wa Daftari. Mzunguko huu wa 12 unahusisha Mkoa huu wa Morogoro na Mkoa wa Tanga katika Halmashauri za Wilaya ya Bumbuli, Handeni, Pangani na Mkinga,” amesema Jaji Mwambegele.

 

Amesema mikoa 27 tayari imekamilisha zoezi hilo ambayo ni pamoja na Kigoma, Tabora, Katavi, Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Manyara, Dodoma na Singida.

 

Ameitaja mikoa mingine kuwa ni Mjini Magharibi, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, Kusini Pemba, Kaskazini Pemba, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Rukwa, Songwe, Njombe, Ruvuma, Lindi na Mtwara.

 

“Mikoa miwili ya Pwani na sehemu ya mkoa wa Tanga kwenye Halmashauri ya Jiji la Tanga, Halmashauri za Miji ya Handeni na Korogwe na Halmashauri za Wilaya ya Kilindi, Lushoto na Muheza inatarajia kukamilisha zoezi hilo tarehe 19 Februari, 2025,” amesema.

 

Wakati huohuo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ndugu. Kailima Ramadhani amesema Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 302,752 mkoani Morogoro sawa na ongezeko la asilimia 18.7 ya wapiga kura 1,612,952 waliokuwepo kwenye daftari la wapiga kura mwaka 2020.

 

“Tume inatarajia baada ya uandikishaji Mkoa wa Morogoro utakuwa na wapiga kura 1,915,704. Idadi hii inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo watanzania ambao walikuwa na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa uboreshaji wa Daftari mwaka 2019/20, lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza kujiandikisha,” amesema.

 

Ameongeza kuwa Mkoa wa Morogoro una vituo   2,816 vitakavyotumika kwenye uboreshaji wa daftari ikiwa ni ongezeko la vituo     112    katika vituo       2,704 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele akizungumza wakati akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoa wa Morogoro unaotaraji kuanza kufanyika Machi 01 hadi 07, 2025. Vituo vikifunguliwa kuanzia Saa 2:00 asubuhi hadi 12:00 jioni kwa siku saba. (Picha na INEC).

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele (kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Ndg. Kailima Ramadhani wakati wa mkutano wa wadau wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoa wa Morogoro unaotaraji kuanza kufanyika Machi 01 hadi 07, 2025. Vituo vikifunguliwa kuanzia Saa 2:00 asubuhi hadi 12:00 jioni kwa siku saba. (Picha na INEC).



Sehemu ya washiriki wa mkutano wa wadau wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoa wa Morogoro wakiwa katika mkutano huo wakisikiliza mada mbalimbali. Uboreshaji wa Daftari Mkoa wa Morogoro unataraji kuanza kufanyika Machi 01 hadi 07, 2025. Vituo vikifunguliwa kuanzia Saa 2:00 asubuhi hadi 12:00 jioni kwa siku saba.