Articles by "BASHUNGWA"
‏إظهار الرسائل ذات التسميات BASHUNGWA. إظهار كافة الرسائل

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amevihimiza Vyama vya Siasa pamoja na Wagombea wa Urais, Ubunge na Udiwani kunadi sera zao kwa Wananchi bila kutumia lugha ya matusi au kuanzisha vurugu zinazoweza kuhatarisha amani, pia amewasisitiza Wananchi kushiriki katika shughuli za kisiasa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu na kushiriki kupiga kura Oktoba 29, 2025.

Bashungwa ametoa wito huo leo, tarehe 22 Agosti 2025, mara baada ya kuzindua jengo la Kituo cha Polisi Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, ambapo amesisitiza kuwa jukumu la ulinzi wa Taifa ni la Watanzania wote, siyo Serikali, Jeshi la Polisi au vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

“Wananchi wote muwe huru kushiriki katika shughuli za siasa hususan wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, zitakazoanza wiki ijayo pamoja nasiku ya kupiga kura Oktoba 29, 2025. Ni matumaini yangu kwamba vyama vya siasa na wagombea wao wa Uraisi, Ubunge, Udiwani watajielekeza kunadi sera zao, na sio matusi ama kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani.” amesema Bashungwa.

Waziri Bashungwa amewahakikishia Wananchi kuwa hali ya usalama nchini ni shwari, hivyo akawahimiza kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii bila kuwa na hofu yoyote.

Aidha, Bashungwa ametoa wito kwa wananchi kupuuza taarifa ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya taasisi, watu binafsi pamoja na vikundi vya watu ambao wamekuwa wakitoa taarifa zinazolenga kuleta taharuki na hofu ya kiusalama nchini, hususan katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Ameliagiza Jeshi la Polisi, kwa kushirikiana na Vyombo vya Usalama, kuendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria kwa wale watakaokaidi na kutaka kuvuruga amani na utulivu wa nchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Halima Okash, amesema kukamilika kwa Kituo cha Polisi cha Wilaya kutasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao, pamoja na kuwezesha Maafisa na Askari wa Jeshi hilo kutimiza majukumu yao katika mazingira mazuri.

Awali, Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi (DCP), Narsis Misama amesema ujenzi wa Kituo cha Polisi Chemba cha Daraja B ni muendelezo wa utekelezaji wa miradi ambayo Serikali imeliwezesha Jeshi la Polisi kuitekeleza ili kuendelea kuboresha mazingira ya Jeshi hilo kutekeleza majukumu yake.








 


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, ametoa wito kwa Waandishi wa habari kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwaelimisha na kuwakumbusha Watanzania juu ya umuhimu wa tunu ya amani na usalama, ambayo ni urithi kutoka kwa waasisi wa taifa letu, Tanzania.

Ametoa wito huo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua Mkutano wa Wakuu wa Majeshi ya Polisi kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), unaofanyika katika ukumbi wa JNICC – Dar es Salaam, leo tarehe 5 Juni, 2025.

“Niendelee kuwaomba, muendelee kushirikiana na Serikali kwa kuwakumbusha Watanzania kuwa amani ni tunu ambayo waasisi wa taifa letu wametuachia, na ulinzi wa taifa letu ni jukumu la kila Mtanzania,” amesema Bashungwa.

Bashungwa amesisitiza nafasi ya vyombo vya habari katika kufanya uandishi wa uchunguzi (investigative journalism), ili kuwaonesha Watanzania hali halisi ya mataifa yanavyopata shida kutokana na kukumbwa na migogoro iliyopelekea amani kutoweka.

Aidha, Bashungwa ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kulinda nchi kwa uzalendo mkubwa, mshikamano na utulivu, na kuifanya Tanzania kuendelea kuwa kisiwa cha amani.

Ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuviwezesha vyombo vya usalama, ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi, kwa kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaendelea kuimarishwa.

Kadhalika, Bashungwa amesema Tanzania inaendelea kuimarisha ushirikiano na nchi za SADC katika kupambana na uhalifu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Camillus Wambura, amesema mkutano huo wa Wakuu wa Majeshi ya Polisi wa nchi za SADC utajadili na kujipanga kwa pamoja kupambana na uhalifu mkubwa wa kupanga na unaovuka mipaka, ili kwa pamoja kuzuia matukio ya kihalifu katika nchi hizo.













Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa (Mb), ameshiriki Mkutano wa Tisa wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Masuala ya Amani na Usalama wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, uliofanyika leo, tarehe 23 Mei 2025, jijini Entebbe, nchini Uganda.

Mkutano huo muhimu, uliolenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika masuala ya amani na usalama kwa kujadili changamoto za kiusalama zinazozikabili nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana nazo, ulitanguliwa na mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu na Wataalamu ulioanza tarehe 19 hadi 22 Mei 2025.

Mawaziri wamejadili na kukubaliana kwa pamoja kuhusu utekelezaji wa masuala mbalimbali muhimu, ikiwemo kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka, kuboresha usimamizi wa mipaka, kuboresha matumizi ya vitambulisho vya taifa, na kukamilisha mchakato wa kuandaa utaratibu wa pamoja wa usimamizi wa masuala ya wakimbizi.

Katika mkutano huo, ujumbe wa wataalamu kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Dkt. Maduhu Kazi, ambapo aliambatana na maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Uhamiaji, na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

 


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, amelipongeza Jeshi la Polisi kwa juhudi zake katika kufuatilia na kuchukua hatua dhidi ya matukio mbalimbali ya kihalifu, ikiwemo tukio la kukamatwa na kuhojiwa kwa mtu anayetuhumiwa kutoa ujumbe wa vitisho kabla ya shambulio dhidi ya Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dkt. Charles Kitima.

Bashungwa alitoa pongezi hizo leo, Mei 5, 2025, mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Jumanne Muliro, kuhusu hatua zinazochukuliwa na Jeshi hilo kufuatia matukio mbalimbali ya kihalifu.

“Nimepata taarifa za kukamatwa na kuhojiwa kwa aliyetoa vitisho kabla ya tukio la kushambiliwa la Padri Kitima. Nalipongeza Jeshi la Polisi kwa jitihada  mbalimbali zinazoendelea za ufutiliaji wa matukio mbalimbali yaliyotokea” amesema Waziri Bashungwa.

Aidha, Waziri Bashungwa amelielekeza Jeshi la Polisi kuendelea na msako dhidi ya washukiwa wa matukio yote ya kihalifu na kuhakikisha wanachukuliwa hatua kali za kisheria kwa haraka.

 


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amelaani vikali tukio la kushambuliwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Dkt. Charles Kitima na kuliagiza Jeshi la Polisi kumtafuta na kumhoji mtu aliyeandika kwenye mitandao ya kijamii kuwa "siku za Kitima zinahesabika",pamoja na watu wote waliohusika na uhalifu huo ili hatua kali za kisheria zichukuliwe.

“Naliagiza Jeshi la Polisi kumtafuta kwa haraka, yule mtu aliye-tweet kwenye mitandao ya kijamii kwamba, ‘siku za Kitima zinahesabika’. Mtu huyu atafutwe haraka, ahojiwe ametumwa na nani, na hatua kali za kisheria zichukuliwe haraka iwezekanavyo, kwa watu wote watakaobainika kuhusika katika tukio hili.” amesema Bashungwa.

Bashungwa amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa viongozi wa dini nchini katika kudumisha amani, mshikamano wa kijamii, na maadili ya Taifa.

“Tunalaani vikali shambulio hilo la kinyama dhidi ya kiongozi wa Dini na tunamuombea Padre, Dkt. Charles Kitima uponaji wa haraka na urejeaji salama katika majukumu yake muhimu kwa taifa” amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa ameagiza Jeshi la Polisi kuwatafuta waliotengeneza na kusambaza waraka feki uliodaiwa kutolewa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), waraka ambao ulilenga kuchochea mgongano kati ya Kanisa na Serikali.

“Kumekuwepo na ‘Waraka feki’ uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ukidaiwa ni waraka wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Baraza la Maaskofu Tanzania kupitia taarifa yake kwa umma imekanusha kuwa waraka huo haukutolewa na TEC, na kuwataka wananchi, waumini na watu wote wenye mapenzi mema kupuuza kabisa waraka huo” amesema Bashungwa

Ameeleza hayo, Mei 02, 2025  jijini Dodoma wakati wa hafla ya kuwaaga Watumishi wa umma waliostaafu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, ambapo alikumbusha kuwa Wizara hiyo ndiyo yenye dhamana ya kuhakikisha usalama wa raia na mali zao kupitia Vyombo vyake vya Usalama.

Bashungwa amewaelekeza Watendaji wote wa Wizara na vyombo vya usalama kutekeleza wajibu wao kwa weledi, kwa kuzingatia sheria, ili kulinda amani na usalama wa nchi.

“Naliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika na kuchukua hatua zinazositahili dhidi ya wahalifu wanaotaka kuvuruga amani ya nchi yetu” amesisitiza Bashungwa.

Vilevile, Bashungwa amekemea vikali vitendo vyote vinavyochafua taswira ya taifa, vikiwemo vya kudhuru watu au kusambaza taarifa zenye kuchochea uhasama wa madhehebu ya  kidini.

“Ni wakati muafaka sasa, Jeshi la Polisi kuongeza kasi ya kusimamia sheria zinazohusu mitandao ya kijamii ili kuhakikisha watu wote wanatii sheria bila shuruti na hivyo kuendelea kuwa na jamii yenye ustaarabu na kuheshimu utu wa kila mtanzania na hata mgeni” amesisitiza.

Amewahakikishia Watanzania kuwa nchi iko salama na kuwasihi kuendelea kutii sheria bila kushurutishwa, ili kudumisha hali ya amani, utulivu na usalama nchini.


 


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amesema kuwa Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania litaendelea kuwawezesha Wafungwa na Mahabusu kusikiliza mashauri yao wakiwa magerezani kupitia Mahakama Mtandao, hasa kunapokuwepo na viashiria vya matishio ya kiusalama, ili kudumisha amani na kulinda usalama wa raia na mali zao.

Ameeleza kuwa mojawapo ya sababu ya kuendelea kutumia Mahakama Mtandao ni masuala ya kiusalama, ambapo hivi karibuni baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wametoa matamko yanayoashiria uvunjifu wa amani na usalama, hali iliyosababisha baadhi ya Wafungwa na Mahabusu kusikiliza mashauri yao kwa njia ya mtandao.

Bashungwa ameyasema hayo leo, tarehe 30 Aprili 2025 jijini Dodoma, alipoambata na Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), kukagua Makasha ya kisasa ya Mahakama Mtandao yanayowezesha usikilizaji wa mashauri kwa njia ya kiteknolojia katima Gereza la Isanga -Dodoma

“Jeshi la Polisi linapokuwa na taarifa za kiinterejensia za wazi na zisizo wazi, kwa mfano maandamano ya CHADEMA na Watanzania ni mashahidi, Viongozi wa CHADEMA walisema waziwazi kwamba waandamana wakakinukishe. Jeshi linapokuwa na taarifa za kiusalama likashirikiana na Mahakama kutoa haki ile ile lakini kwa kutumia teknologia ya Mahakama Mtandao ili kuzuia fujo mtaani, naomba Watanzania watuelewe” amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amewahakikishia wananchi kuwa Vyombo vya Usalama vitaendelea kuhakikisha kuna utulivu kwa kudhibiti maandamano, matishio ya kiusalama, na vitendo vyote vinavyoweza kuhatarisha amani na usalama wa nchi

“Niendelee kuliagiza Jeshi la Polisi  kusimamia sheria na kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa na amani, hata yule ambaye hataki amani, sisi tutamlazimisha kuhakikisha nchi yetu inakuwa amani na salama” amesisitiza Bashungwa

Pia, Bashungwa ameliagiza Jeshi la Magereza kusimamia kwa ukamilifu sheria na taratibu kwa wale wanaotaka kuwaona Wafungwa na Mahabusu, akieleza kuwa taratibu hizo lazima ziheshimiwe bila upendeleo.

““Niliona moja ya viongozi akisema anataka ‘Special treatment’ anapoenda kumuona Maabusu, hiyo nayo sio sawa. Zipo taratibu zinazosimamiwa ndugu, jamaa na rafiki anapotaka kwenda kumuona Maabusu au Mfungwa, kwahiyo mkitaka tuwe na ‘VIP treatment’ na yenyewe sio sawa” amesema Bashungwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), Vita Kawawa, amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kuendelea kuwawezesha Wafungwa na Mahabusu kupata haki zao kwa kusikiliza mashauri kupitia Mahakama Mtandao, hatua inayotekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.







 


Jumla ya Milioni Tatu zinashindaniwa katika Mashindano ya mpira wa miguu yaliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Nkenge wilaya Missenyi mkoani Kagera ambayo yatashirikisha timu 20 kutoka katika wilaya hiyo.

Mashindano hayo yenye jina la Dk.Samia Na Kyombo yanalenga kuwakunsanya vijana wa wilaya ya Missenyi ili kuibua vipaji vya vijana wanaoishi vijiji vya pembezoni mwa Tanzania na kiviendeleza katika ngazi nyingine za mpira wa miguu chini pamoja na kuendeleza mshikamano kutoka kwa vijana wa kata moja Hadi nyingine

Mashindano hayo yamefunguliwa Rasmi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa katika Uwanja wa Mashujaa, Bunazi, wilayani Missenyi, mkoani Kagera, na Yanatarajia kutamatika Juni mwaka huu baada ya kupata timu ambazo zitaingia Fainali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri Bashungwa alisema kuwa mashindano hayo yatasaidia kuibua vipaji vya michezo kwa vijana, kuimarisha afya, kuendeleza mshikamano na kudumisha upendo miongoni mwa vijana na wakazi wa Wilaya ya Missenyi huku watakaonyesha vipaji vyao watapata nafasi ya kutafuta Fursa nyingine Za kimichezo ndani na nje ya nchi

“Mbunge kwa kushirikiana na Madiwani wameonyesha dhamira ya dhati katika maendeleo ya michezo ndani ya Wilaya ya Missenyi Ligi hii siyo tu burudani bali pia ni fursa kwa vipaji chipukizi,wilaya hii Iko pembezoni lakini naelewa kuwa vijana wengi wanavipaji hivyo wasisite kuonyesha vipaji vyao ,naomba vijana kutoka kata zote 20 mshiriki kwa moyo wa upendo na mshikamano,” alisema Bashungwa.

Aidha, Waziri Bashungwa ametoa wito kwa waamuzi na wasimamizi wa mashindano hayo kuhakikisha wanatenda haki wakati wa michezo yote, katika Mashindano hayo ili kiyafanya yamalizike kwa amani na kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

Mbunge wa Jimbo la Missenyi, Florent Kyombo, alisesema kuwa mashindano hayo yanalenga kuimarisha mahusiano na mshikamano kati ya vijana na wananchi wa kata zote 20 za wilaya hiyo na hiyo ilikuwa moja ya haadi zake katika kuhakikisha anatekeleza ilani ya chama Cha mapinduzi ni lazima vijana wapate Fursa ya kushiriki michezo na kuonyesha vipaji vyao.

Alisema kuwa viwanja vya Mugana B na uwanja wa Mashujaa Bunazi ndivyo vitakavyotumika katika Mashindano hayo kwa kukutanisha makundi yaliyopangwa na kamati.

Hafla ya uzinduzi ilizikutanisha timu za kata za Kyaka na Mtukula, timu zote shiriki zilipatiwa vifaa mbalimbali vya michezo, ikiwemo jezi, mipira, vifaa vya mazoezi, pamoja na fedha kwa ajili ya maandalizi ya mechi.









 


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa (Mb), leo tarehe 20 Aprili 2025, ameungana na waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Kiruruma, Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, kushiriki Ibada ya Sikukuu ya Pasaka.

Akizungumza mara baada ya Ibada hiyo, Bashungwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira bora ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, hususan kupitia kilimo cha mazao ya kimkakati kama kahawa.

"Rais Samia alipoingia madarakani alikuja na sera mpya na utaratibu wa minada ya kahawa kufanyika kupitia vyama vya msingi. Msimu uliopita tulishuhudia bei ya kihistoria ya kahawa. Na sasa, kwa mujibu wa mwongozo mpya wa Bodi ya Kahawa, msimu huu bei ya kuanzia kwenye mnada ni shilingi 5,000 kwa kilo, na ushindani wa bei unatarajiwa kuifanya ipande zaidi," amesema Bashungwa.

Ameongeza kuwa kupanda kwa bei ya kahawa kumesababisha ongezeko la vitendo vya wizi wa kahawa mashambani, hivyo amemuelekeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera kuhakikisha Jeshi la Polisi linachukua hatua kali dhidi ya wahalifu hao.

“Nimeshamuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera kuhakikisha Jeshi la Polisi linasimama imara kukabiliana na wezi wa kahawa ili wakulima waweze kunufaika ipasavyo na bei nzuri za zao hilo,” amesisitiza Bashungwa.

Katika Ibada hiyo iliyoongozwa na Paroko wa Parokia ya Kiruruma, Padre Cyril Ndamutahi, Mhe. Bashungwa ameanzisha harambee ya kuchangia ujenzi wa Makao ya Padre kwa kuchangia kiasi cha Shilingi milioni 10.

Awali, Padre Ndamutahi aliwahimiza waumini kuendelea kuwa karibu na Mungu kwa kushiriki ibada na shughuli mbalimbali za kanisa, akiwataka kuepuka mienendo inayowatenga na imani, ikiwemo uzembe wa kushiriki ibada na kutokujitoa katika kazi za kanisa.

 


Bashungwa aagiza Jeshi la Polisi kushughulikia wizi wa kahawa

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kusimamia sera nzuri na mifumo madhubuti ya usimamizi na uuzaji wa kahawa, kwa lengo la kuhakikisha wakulima wa zao hilo wanaendelea kunufaika kwa kupata bei nzuri na yenye tija.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Mbunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa, tarehe 17 Aprili 2025, wakati akifunga kambi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) katika Wilaya ya Karagwe, mkoani Kagera.

Bashungwa alieleza kuhusu changamoto zilizokuwepo katika vyama vya ushirika, ambako baadhi ya viongozi wachache walihusika katika kuwaumiza na kuwanyonya wakulima wa kahawa wilayani humo.

"Kipindi kile haikuwa kazi rahisi. Mnajua vita iliyokuwepo kwenye masuala ya ushirika. Niliwaambia viongozi wangu wa chama kuwa niko tayari kuwa mbunge wa kipindi kimoja, lakini siwezi kuwa sehemu ya unyonyaji wa wakulima wa kahawa," alisema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amemuagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Karagwe (OCD) kuhakikisha anashughulikia aina yoyote ya uhalifu unaowalenga wakulima wa kahawa, ikiwemo usalama wa mashamba, ili mkulima aweze kunufaika na jitihada zake.

"OCD, tunavyoingia kwenye msimu wa kahawa, kutokana na bei kuwa nzuri, kutakuwepo na ongezeko la vitendo vya uhalifu mashambani. Wewe na askari wako hakikisheni mnadhibiti hali hiyo na kumlinda mkulima hadi kahawa yake iuzwe katika vyama vya msingi," alisisitiza.

Pia, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali imehakikisha vyama vya ushirika vinaendeshwa kwa kuzingatia taratibu sahihi ili kuleta ushindani wa bei na kuhakikisha wakulima wanapata faida stahiki.