

Kwa kauli moja leo tarehe 13 Mei 2025 Bunge la Tanzania limepitisha kwa kishindo bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Taasisi zake kwa mwaka 2025/2026 yenye jumla ya shilingi Trilioni 2.439.
Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameainisha vipaumbele vya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, ambako imelenga kuimarisha mchango wa Sekta ya Madini katika kukuza uchumi wa taifa, kuongeza ajira, na kuinua ustawi wa jamii kupitia matumizi bora ya rasilimali za madini hapa nchini.
Ameyabainisha hayo leo Mei 02, 2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha Hotuba ya Mpango wa Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha wa Serikali wa 2025/2026 ambapo kupitia mpango huo, Wizara ya Madini imepanga kukusanya maduhuli ya shilingi 1,405,537,268,755.00 (Trilioni 1.4).
Ili kufikia lengo hilo la makusanyo ya maduhuli, Waziri Mavunde amebainisha kuwa, Wizara imeweka mkazo kwenye kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa kuhakikisha mifumo ya ukusanyaji mapato inaendelea kuwa ya kisasa, shirikishi sambamba na yenye uwazi.
Waziri Mavunde amesema kuwa, hatua hiyo, inakwenda sambamba na lengo kuu la kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa (GDP) hususan kupitia ongezeko la shughuli za uongezaji thamani na mauzo ya madini ndani na nje ya nchi. Itakumbukwa kuwa mchango wa Sekta kwenye GDP umefikia asilimia 10.1 mwaka 2024 ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya muda ulioainishwa katika Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2021/2022 hadi 2025/2026.
Aidha, Waziri Mavunde ameeleza kuwa, Vipaumbele hivyo pia vinaangazia kuendeleza mnyororo wa thamani kwenye madini muhimu na mkakati kama vile madini ya kielektroniki, ambayo yanatajwa kuwa nguzo ya maendeleo ya teknolojia duniani ambako kwa kufanya hivyo, Tanzania inalenga kujenga uchumi shindani unaotegemea maarifa na ubunifu.
Ameongeza kuwa, Wizara imedhamiria kuhamasisha uwekezaji katika Sekta ya Madini, huku kipaumbele kikiwa ni uongezaji thamani ndani ya nchi kabla ya kusafirishwa na kuuzwa nje ya nchi. Aidha, kuimarisha uendeshaji wa minada na maonesho ya madini ya vito ni hatua inayolenga kuongeza uwazi, ushindani, na thamani halisi ya madini yanayouzwa.
Sambamba na hilo, katika jitihada za kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika kwa tija, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa Serikali imepanga kuongeza uwekezaji kwenye tafiti za kina za madini, kwa kushirikiana na taasisi za kitaaluma na sekta binafsi, hatua itakayowezesha kugundua maeneo mapya ya uchimbaji, kuandaa ramani sahihi za kijiolojia pamoja na kuimarisha kanzidata ya jioliojia ya nchi.
Kwa kutambua mchango wa wachimbaji wadogo, Waziri Mavunde ameeleza kuwa, mpango huo umeweka kipaumbele cha kuwarasimisha na kuwaendeleza wachimbaji hao, kwa kuwapatia elimu, teknolojia, kuwaunganisha na taasisi za kifedha ili kupata mikopo yenye masharti nafuu kukuza mitaji yao na kuendelea kuwa masoko ya uhakika ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi, usalama na tija.
Pia, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa, Serikali kupitia Wizara itaendelea kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini kama Tume ya Madini, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) pamoja na Taasisi ya Uhamasishaji na Uwazi katika rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) ili kusaidia kuboresha usimamizi, utafiti na uwekezaji katika sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Bajeti ya Wizara ya Madini kwa Mwaka 2025/2026 inalenga kujenga Sekta ya Madini imara, endelevu na shindani kimataifa kwa kuwa ni moja kati ya sekta inayozalisha ajira, kuongeza mapato ya serikali, na kuchochea maendeleo na miundombinu nchini, maendeleo ya kijamii na uchumi kwa ujumla.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha mradi wa njia kuu ya kusafirisha umeme kutoka Tabora hadi Katavi (132kV) pamoja na ujenzi wa kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme vinakamilika kwa wakati ili Mkoa wa Katavi uingizwe kwenye gridi ya Taifa ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.
Mhe. Dkt.Samia ameyasema hayo leo 13 Julai, 2024 wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 wa Tabora-Katavi na kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Inyonga ambapo ameridhika na maendeleo ya miradi hiyo.
‘’Natamani Katavi iachane kabisa na matumizi ya Majenereta ambayo ni gharama kubwa na pia kukamilika kwa miradi hii kutawawezesha wananchi wa Katavi kuutumia umeme kwa maslahi ya kiuchumi na kukuza uwekezaji, Serikali imetumia gharama kubwa kutekeleza miradi hii nawaasa wananchi mchangamkie fursa zinazotokana na kuwepo kwa umeme wa kutosha na wa uhakika." Amesema Dkt.Samia
Aidha, amepongeza kazi nzuri inayofanywa na TANESCO katika kutekeleza miradi ya umeme na kuwataka kuongeza kasi kwenye uunganishaji wa wateja pindi miradi inapokamilika.
Amesisitiza kuwa, umeme ni tegemeo kubwa kwa watu binafsi pamoja na uchumi wa viwanda na hiyo yote ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo inaelekeza uwepo wa umeme wa kutosha nchini.
Aliwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa Mhe. Rais, Mkurugenzi Mtandaji wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO Mha. Gissima Nyamo-Hanga amesema, mradi huo pindi utakapokamilika utaokoa kiasi cha takribani Bilioni 2.2 kwa mwezi kwa ajili ya mafuta yanayotumika kuendesha Mitambo ya Umeme inayotumiwa mkoani Katavi pindi tu itakapoingizwa kwenye umeme wa Gridi ya Taifa
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuagiza Mkandarasi Avic anayejenga barabara ya mzunguko wa nje ya Dodoma, yenye urefu wa Kilometa 112.3 sehemu ya Ihumwa Dry Port - Matumbulu - Nala (km 60), kuhakikisha anakamilisha barabara hiyo ifikapo mwezi Desemba, 2024.
Bashungwa ametoa agizo hilo Septemba 29, 2023, jijini Dodoma wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo ambapo pamoja na mambo mengine amemsisitiza mkandarasi huyo kuongeza spidi kwenye ujenzi wa madaraja mawili ambayo yanaonekana kuchelewa ujenzi wake.
“Sipepesi macho kwenye usimamizi wa mikataba, kufanya kazi kwa ubora na kasi ndio kipimo chako, ukizembea kwenye kazi hii usahau kupewa kazi nyingine za ujenzi kwenye Sekta hii nchini”, amesema Bashungwa.
Ameahidi kutembelea tena mradi huo ifikapo Desemba mwaka huu ili kuona uetekelezaji wa maagizo yake na kumsisitiza Mkandarasi huyo kufanya kazi usiku na mchana ili uweze kukamilika kwa wakati kulingana na maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Bashungwa ameuagiza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), kushirikiana na Shirika la Reli (TRC), kurudisha haraka mawasiliano ya barabara ya lami eneo la Mkonze na Nala ambalo lilibomolewa kwa ajili ya ujenzi wa reli ya SGR kwani wananchi wamekuwa wakipata kero kutokana na changamoto katika maeneo hayo.
Bashungwa amewataka wakandarasi nchini wanaotekeleza miradi ya ujenzi kuhakikisha wanatekeleza miradi hiyo kwa mujibu wa Mkataba na kusisitiza kutokuwa na huruma kwa yeyote atakayekiuka mikataba hiyo.
Bashungwa amemuagiza Mhandisi Mshauri Mzawa wa kampuni ya Inter-Consult kumsimamia mkandarasi wa kampuni ya China Civil Engineering Corporation (CCEC) anayetekeleza sehemu ya Nala - Veyula - Mtumba (km 52.3), kutoa vifaa vya usalama kwa wafanyakazi wake ili kuepukana na madhara yanayoweza kutokea maeneo ya kazi.
Katika hatua nyingine, Bashungwa amewaagiza Mameneja wa TANROADS wa mikoa yote nchini kuhakikisha wanazibua mifereji ya barabara zilizo chini ya Wakala huo kabla ya mvua hazijaanza ili zisiwe chanzo cha kuleta mafuriko, sambamba na hilo Waziri huyo amempongeza Meneja wa TANRODS Mkoa wa Dar es Salaam kwa kufanya matengenezo na kuzibua barabara na mifereji katika mkoa huo.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Eng. Mohamed Besta ameeleza kuwa mpaka sasa sehemu ya mradi kutoka Nala – Veyula – Mtumba (km 52.3) umefika asilimia 54.3 na sehemu inayoanzia Ihumwa Dry Port – Matumbulu – Nala umefika asilimia 50 na sasa wakandarasi wanaendelea na kazi mbalimbali za ujenzi wa makalavati na madaraja makubwa mawili.
Mradi wa Barabara ya Mzunguko wa nje ya Dodoma (Km 112.3), unagharimiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa gharama ya shilingi Bilioni 221 na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2024.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akitoa maelekezo kwa mkandarasi wa Kampuni ya Avic wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya Dodoma yenye jumla ya urefu wa kilometa 112.3; sehemu ya Ihumwa Dry Port - Matumbulu - Nala (km 60), Septemba 29, 2023 jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akiangalia kiatu cha mmoja wa Wafanyakazi katika mradi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya Dodoma yenye urefu wa kilometa 112.3; sehemu ya Nala -Veyula – Mtumba (km 52.3), Septemba 29, 2023 jijini Dodoma. Amemsisitiza Mkandarasi China Civil Engineering Corporation kuwanunulia vifaa vya usalama wafanyakazi wake.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya mzunguko wa nje ya Dodoma (km 112.3) inayojengwa kwa kiwango cha lami. Ujenzi wake unagharimiwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa gharama ya shilingi Bilioni 221.